Wednesday, November 15

Bob Wangwe ahukumia kulipa faini au jela mwaka mmoja



Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu Bob Wangwe ambaye ni mtoto wa mwanasiasa marehemu Chacha Wangwe, kulipa faini ya Sh 5 milioni ama kutumikia kifungo cha mwaka mmoja na nusu jela.
Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatano baada ya kupatikana na hatia katika shtaka la kuchapisha taarifa za uongo kwenye mitandao ya kijamii.
Bob ana taaluma ya sheria na mwanaharakati wa haki za binadamu.
Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi ametoa hukumu hiyo leo Jumatano baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi sita wa  upande wa mashtaka, vielelezo vitano na utetezi wa mshtakiwa mwenyewe.
Amesema kuwa Mei 7, 2016 askari polisi walipata taarifa ya chapisho la mtoto huyo wa Chacha Wangwe, na walianza kumfuatilia na kumkamata kisha walichukua simu na kuipeleka maabara ya polisi ili kuikagua.
Bob hukupinga kuandika maneno hayo lakini alidai kuwa hakuyachapisha katika mtandao wa kijamii bali yalikuwa ni siri kwenye akaunti yake.
Hakimu Shaidi amesema wakati wa ushahidi imeelezwa kuwa simu yake ilipokaguliwa ilionekana ilitumika kuchapisha ujumbe huo kwa jamii na watu walijibu, ikiashiria ujumbe uliwafikia.
“Nidhahiri ulikuwa na nia ya kuchapisha taarifa hiyo, kueleza kile ambacho ulikiona sahihi kama ingekuwa ni ujumbe wako binafsi basi polisi wasingeweza kukutafuta na watu wasingekujibu.” 
Hakimu Shahidi amesema kutokana na hatua hiyo Bob amekutwa  na hatia chini ya kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya 2015.
Bob ameomba apunguziwe adhabu kwa sababu ni mwanafunzi wa masomo ya sheria, pia ni kijana mdogo na ni kosa lake la kwanza kulitenda.
Hakimu Shaidi amesema anakubaliana na hoja za Bob, kwani Mahakama inamuona bado ni mdogo na anapaswa kufanya mambo mengi mazuri katika jamii.
Pia amesema kama yeye ni mwanafunzi wa masomo ya sheria anapaswa kufanya mambo mema katika jamii vitu ambavyo wengine watamuiga.
Mahakama imemhukumu kulipa faini ya Sh 5 milioni ama kifungo cha mwaka mmoja na nusu jela. Hata hivyo alifanikiwa kulipa kiasi hicho cha fedha na kukwepa kifungo.
Katika kesi hiyo namba 167, 2016 Bob alikuwa anakabiliwa na shtaka la kuchapisha taarifa za kupotosha katika ukurasa wake wa mtandao wa Facebook.

No comments:

Post a Comment