Thursday, November 9

AU kuvijengea uwezo vyombo vya usalama Somalia

Francisco Madeira
Umoja wa Afrika (AU) unataka kuwepo msaada wa haraka na muwafaka kwa ajili ya vyombo vya usalama vya taifa, Somalia, wakati AU ikijiandaa kupunguza vikosi vyake nchini humo.
Mjumbe maalum wa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (SRCC) Somalia, Balozi Francisco Madeira, ameshauri kuwa ni muhimu kuwepo uratibu mzuri na unaoendena na wakati ili kulinda kile kilichofikiwa katika ulinzi hivi sasa nchini Somalia.
Pia ameshauri kuwa vyombo vya usalama vya Somalia vijengewe uwezo kamili wa kusimamia jukumu la ulinzi wa nchi yao, wakati majeshi ya Umoja wa Afrika yatakapoondoka Somalia.
Ujumbe wa AU nchini Somalia umetangaza kwamba utaondoa wanajeshi 1,000, wanaopambana na waasi wa vikundi vya Kiislam vyenye misimamo mikali nchini humo, mwisho wa mwaka 2017.
Shirika la habari la AFP limeripoti kwamba mjumbe huyo maalum wa Umoja wa Afrika nchini Somalia, Madeira, alisema katika taarifa hapo jana, kwamba jeshi la kitaifa litachukua jukumu la usalama wa nchi hiyo.
Majeshi ya Amisom yalipelekwa nchini Somalia mwaka 2007, ili kuilinda serikali iliyoungwa mkono na jumuiya ya kimataifa dhidi ya mashambulizi ambayo yamekuwa yakitekelezwa na kundi la kigaidi la Al-Shabaab. Mwaka jana, Umoja wa Afrika ulitangaza azma ya kuondoa wanajeshi wapatao 22,000, na kukabidhi jukumu la ulinzi kwa jeshi la kitaifa la Somalia.

No comments:

Post a Comment