Tuesday, October 10

WAKILI WA LEMA KESI YA UCHOCHEZI AJITOA

Wakili wa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Sheck Mfinanga amejitoa kumtetea katika kesi ya uchochezi inayomkabili kwa madai kuwa haridhishwi na mwenendo wa shauri hilo, ikiwamo Hakimu kugoma kujitoa baada ya kuombwa na upande wa utetezi kutokana na kutokuwa na imani naye.
Wakili Mfinanaga amedai sababu nyingine ni kutopewa nakala za mwenendo wa kesi za uamuzi mdogo uliotolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Arumeru, Desderi Kamugisha Septemba 25, mwaka huu ambapo Lema kupitia Wakili huyo alidai hana imani naye hivyo kumtaka ajitoe.
Amedai baada ya Hakimu kukataa kujitoa na aliwasilisha kusudio la kukata rufaa kupinga uamuzi wa huo na kuomba mwenendo wa kesi usimame ili wapate nafasi ya kukata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, lakini Hakimu hakukubaliana na ombi hilo
“Tuliandika barua Oktoba 2, mwaka huu kukumbusha kupewa nakala hizo lakini hatukupewa, hivyo najitoa kuendelea kumuwakilisha Lema kutokana na mambo hayo,” amedai Mfinanga.
Lema ambaye alikuwepo mahakamani hapo alisema kwa kuwa yeye si mwanasheria anamuomba Hakimu kumpa muda ili atafute wakili mwingine na akikosa atajitetea mwenyewe.
Hakimu Kamugisha alikubaliana na ombi la Lema na kuahirisha kesi hiyo hadi Novemba 14, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment