Friday, October 27

Wakenya wahesabu kura, hasara ya mgawanyiko


Nairobi, Kenya. Wakati maofisa wakiendelea kujumlisha kura, Wakenya wanahesabu hasara ya mgawanyiko mkubwa katika uchaguzi wa jana uliogubikwa na mambo kadhaa yakiwemo upinzani kususa na maandamano yaliyoishia kwa watu wanne kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa.
Uchaguzi wa marudio kwa kura ya urais uliofanyika Alhamisi uliathiriwa na vurugu kutoka kwa wafuasi wa National Super Alliance (Nasa) wanaoongozwa na Raila Odinga wakijaribu kuzuia usifanyike lakini waliishia kupambana na polisi waliowafyatulia risasi, kupigwa kwa mabomu ya machozi na kurushiwa maji ya kuwasha na kupigwa risasi.
Uchaguzi huo umefanyika miezi miwili baada ya mgogoro wa kisiasa uliodumu miezi miwili ulioanza baada ya Mahakama ya Juu kubatilisha matokeo ya Agosti 8 yaliyompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta kutokana na “ukiukwaji wa taratibu”.
Hata hivyo, ingawa uamuzi huo awali ulisifiwa kwamba unaimarisha demokrasia katika moja ya mataifa yenye uthabiti zaidi Afrika Mashariki, athari zake zimekuwa kubwa na kuitambukizi Kenya katika wiki kadhaa za maandamano ya hasira, chuki za kisiasa na vitisho dhidi ya maofisa wa uchaguzi.
Hatua ya Odinga, mpinzani mkuu nchini humo kususia uchaguzi wa marudio kwa madai kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) imeshindwa kufanya mabadiliko muhimu kuhakikisha uchaguzi huo unakuwa huru, haki na wa kuaminika, imemwacha Kenyatta akiwa na uhakika wa ushindi.
Lakini wakati maofisa wakihesabu kura, baadhi yao wakiwa wamejifungia chini ya ulinzi mkali wa polisi, maswali magumu yanaibuka juu ya kuaminika kwa uchaguzi uliosusiwa na idadi kubwa ya watu 19 milioni waliokuwa wamejiandikisha.
Makadirio ya wapigakura waliojitokeza kwa mujibu wa IEBC wanafikia asilimia 48. Ikiwa idadi hiyo itathibitishwa litakuwa anguko kubwa kwani katika uchaguzi wa Agosti asilimia 80 ya waliojiandikisha walijitokeza.

No comments:

Post a Comment