Monday, October 16

Wafuasi wa Nasa waandamana Nairobi


Nairobi, Kenya. Wafuasi wa upinzani wamerudi mitaani kuendelea na maandamano yao kushinikiza marekebisho ya uchaguzi, hata baada ya kiongozi wa National super allience Raila Odinga, kujiondoa katika uchaguzi wa marudio wa urais.
Maandamano ya wafuasi wa Nasa yalifanyika mitaa ya Kisumu, Mombasa na Nairobi, bila kujali katazo la serikali la kutoandamana katika maeneo muhimu ya kibiashara ya miji hiyo mitatu.
Biashara kando kando ya barabara ya Moi zilifungwa wakati polisi wakiwatawanya waandamanaji waliotiwa hamasa na mkutano wa hadhara uliohudhuliwa na Odinga Jumapili.
Wakati wa mkutano huo wa hadhara, Odinga na viongozi wenzake wenye misingi ya ushirikiano Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula walisisitiza wito wao wa kufanya maandamano kila siku kuanzia wiki hii.
Waandamanaji wamepita barabara ya Moi wakielekea ofisi za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) polisi walipowarushia mabomu ya kutoa machozi.
Maduka ya Migori, ofisi na hoteli zilifungwa wakati waandamanaji wa Nasa walipokuwa wakiandamana mitaani.
Waandamanaji wakiongozwa na Mbunge wa zamani wa Migori, John Pesa wakiigiza kubeba jeneza lenye mwili wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa IEBC, Ezra Chiloba. Polisi waliwatazama kwa mbali bila ya kuingilia.

No comments:

Post a Comment