Sunday, October 15

Ushabiki wa Kisiasa: Kansa Inayotafuna Taifa


Tunatembea katika kipindi kizito na kigumu kwa mtazamo wa kutojithamini kama Taifa. Tumefikia kiwango cha juu (ijapo siyo cha mwisho) cha uharibifu wa Taifa na tunadhani kwa kufanya hivyo tunajipeleka kwenye mafanikio.
Tumejinyima haki ya kujivunia uzuri wa amani yetu na imekuwa lugha kama ya kawaida baadhi ya wanasiasa kujinasibu kuwa wako tayari kumwaga damu zao. Suala la kujichanganya kuzungumza ujinga huu, linaweza kuota mizizi na likaharibu Taifa, ni heri kulaumiwa sasa kuliko kusubiri sana.
Tumeandika namna wanasiasa wetu wanavyopotea na jinsi ilivyo rahisi wao kuondoka kabisa kwenye medani za kisiasa. Tumetambua wajibu wetu kwa Taifa na tumeamua kuwajibika. Wajibu wetu ni kuona Taifa liko salama. Tumejiaminisha kwa umma na umma umetuamini kwamba tutatumia kalamu zetu kuelimisha, kuonya, kufariji na kamwe, hazitatumika kufurahisha magenge na kupoteza umma.
Mwalimu wangu Mzumbe, Profesa Kamuzora alinifundisha, namna ya kukuza weledi na taaluma ni kuandika na kusoma. Na kuandika yenye tija, kunaleta mantiki kuliko kuandika chochote.
Tunaandika makala ambazo haziwafurahishi wengi na hatuna namna zaidi ya kufanya hivyo. Katika taaluma ya utawala inaaminika, meneja anayefurahiwa na wote huyo nafasi yake ni getini ili awafungulie wote na wafurahie huduma yake. Tukizichukua makala zetu kama sehemu ya utawala wa fikra na mitazamo ya kisiasa na kiuchumi katika Taifa, tunahesabu nukta muhimu kwamba tumefanikiwa. Gazeti la Mwananchi limefanikiwa kusomwa na wengi, na ni weledi utakaowafanikisha zaidi na nitajivunia kuwa sehemu ya mafanikio yao, na nawashukuru kubeba mafanikio yangu.
Taifa linatafunwa na kansa ya ajabu na isiposhughulikiwa kule wanakohubiri kwamba tunaweza kuelekea, tukiwadharau wanaweza kutupeleka. Si mara moja kuwasikia wanasiasa wakisema Tanzania ni sawa na ilivyokuwa Burundi, au ilivyo Sudani Kusini au kwingineko na wanasema haya kwa minajiri tu ya kutaka waungwe mkono. Wanakosoa kila utendaji wa Serikali na hakuna namna wanaridhika na lolote, huo ndio uzandiki unapotufikisha Taifa katika kiwango cha kujiangamiza ikiwa tutawavumilia.
Waongo na wajivuni wamevamia siasa za Tanzania, na haya tunayaona kuwa ni zao la ujenzi wa mfumo haramu kwenye siasa halali za taifa. Ukimsikia mwanasiasa anatuhumu vyombo vya ulinzi na usalama kwamba vinahatarisha uhai wake, kisha kesho anaomba kulindwa na vyombo hivyo hivyo, hata kama wewe si mtaalamu wa magonjwa ya akili utajiridhisha tu, kuwa hapo kuna ukichaa. Wamelizushia Taifa mambo ya hovyo, na wamefanya hayo wakiwa ardhi ya ugenini, hatusemi kwamba walifanya kwa kujifurahisha, ni mpango halisi unaotakiwa kudhibitiwa.
Ujinga wa kupenda unatupotosha
Tumejielekeza sana kwenye ushabiki wa yale tunayoyasikia au ambayo wale tunaowafuata wanasema. Tumejiaminisha katika masuala ambayo kwa uhalisia wengi hawana ufahamu nayo kabisa au ufahamu wao umekuwa juu juu tu.
Tulipouliza; hivi mabadiliko tuliyohubiri 2015 tulimaanisha nini?, wengi waliishia kujichanganya na kelele za wanasiasa bila kujipa ufahamu zaidi kuhusu kelele hizo. Wapo waliojaribu kujenga hoja kuhusu vyama vya siasa vinavyoanzishwa, kwamba vitapata kujulikana vipi endapo havipewi nafasi ya kufanya siasa? Tumelijibu swali hilo kwa ufasaha kabisa kwamba kazi ya Chama cha siasa siyo kujulikana, kazi yake ni kutafuta dola na wakati muafaka wa kutafuta dola upo; kwa sasa ipo njia muafaka ya kujijuza kwa umma, ni kupepea sawa na mwelekeo wa upepo.
Upotofu wa Siasa za 2014-15
Wapo wanaoshindwa kuelewa na kujipa maarifa ya mambo madogo kabisa katika siasa, mfano uwepo wa Ukawa. Na tumeshindwa kuelewa kwa nini hata hawajajifunza tu kutoka Kenya ili angalau tu wajue tofauti ya Ukawa yao na miunganiko ya huko ugahibuni. Niwajulishe na kama walikuwa hawajui, Ukawa ilikufa siku ya Uchaguzi Mkuu, baada ya hapo aliyepata kapata na aliyekosa kakosa, wanajidanganya kwamba Ukawa ipo kwa kudumu, ndipo wanaposhindwa hata kushauri mshirika mwenzao wa Ukawa CUF namna bora ya kuondokana na kadhia waliyo nayo badala yake wanailaumu Serikali kwamba inaikandamiza CUF. Wangejifunza kutoka Kenya kidogo tu, wangeyajua haya.
Ujinga wa kupenda, unawafanaya wanasiasa wanakuwa waongo ndiyo maana unamsikia mbunge anajirekodi na kutangaza eti amefuatiliwa Iringa, na kwingineko na kwa ujuzi hafifu anataja wengine wanaofuatiliwa, lakini uzito kichwani unamfanya ashindwe kusema sababu za kufuatiliwa. Kupenda, kunawafanya wanasiasa wanaamka na uongo na wanajiweka katika mazingira ya kutofikia kutoa ushahidi eti, vielelezo vya rushwa wanataka wampe Rais! Tangu lini Rais ni taasisi ya kuchunguza rushwa? Tunatamani siasa, lakini za aina hii hapana. Tunajengewa mazingira ya kutukanana bila sababu na kwa jinsi hii, vijana wanaanza kugawika kwa sababu wajanja wameamua kuwatumia. Rushwa ipelekwe Takukuru na siasa zipelekwe vyamani, hapo ujanja utakwisha.
Wanasiasa vijana na siasa zetu
Katika Bunge la 11, Uchaguzi Mkuu wa 2015 uliwezesha vijana wengi kupenya na kuingia humo. Vijana wamekuwa chachu ya mijadala ya Bunge, lakini wengine wamejitoa huko na kujielekeza kwenye mambo ya harakati zaidi kuliko kufanya siasa za wakati wao. Vijana walidhani kuingia bungeni ni kwenda kuinyoosha Serikali na kupata sifa nyingi sana. Walichokutana nacho ni kanuni zinazoendesha Bunge zinawanyima fursa ya kuwa maarufu kuliko Bunge, na huo umekuwa mwiba mchungu kwao.
Ipo tofauti kubwa kati ya wanasiasa wa CCM na wale wa upinzani hasa vijana. Mfumo wa CCM unawajenga na kuwarejesha kundini wanaokengeuka. Mfumo unalinda heshima yake, na kwa jinsi hii hata wale wanaodhani kupayuka na kujisemesha wako tayari kufukuzwa uanachama wanadhibitiwa. Kwa mfumi wa CCM ni nadra mtu mmoja kuwa na nguvu kuliko Chama, au kuwa mtovu wa nidhamu kwa kudumu.
Tofauti ya vijana wa CCM na vyama vingine, ni mifumo ya sasa ya vyama vyao. Nasema mifumo ya sasa kwa sababu chama kama Chadema kimepoteza mfumo wake wa udhibiti wa nidhamu ya viongozi wake kilichobaki ni kila mmoja ni mamlaka ya peke yake isipokuwa linapokuja suala la masilahi. Chama cha CUF, tunakosa kukisemea kwa uzuri au kwa ubaya kwa sababu, kama tulivyowahi kusema, kimejipoteza kwa kupata ushauri haramu, hivyo hakina mfumo wa kiutawala unaoweza kudhibiti na kwa sasa wanahangaika na hali yao.
Kwa ajili ya kupenda, tumejikuta hata maovu yanayofanywa na tunaowapenda tunayaona ni sahihi, na hata mema yanayofanywa na tusiowapenda tunayaona ni mabaya. Turejee katika wosia wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alioutoa katika andiko lake la “Tujisahihishe”, tutaiona nuru mpya na siasa njema katika Taifa letu.
Mungu Ibariki Tanzania
Mwalimu Falesy Mohamed Kibassa ni Msomaji wa Magazeti ya Mwananchi, Mtafiti na Mkurugenzi Simu: +255716696265/ Barua pepe fmkibassa@gmail.com

No comments:

Post a Comment