Baadhi wa viongozi wa muungano wa upinzani, NASA, walisema Jumamosi kwamba iwapo rais Uhuru Kenyatta atalishwa kiapo kwa muhula wa pili baada ya uchaguzi wa marudio uliozua utata, basi watamwapisha kiongozi wao, Raila Odinga kama rais.
Wakizungumza katika eneo la Mavoko kaunti ya Machakos, wanasiasa hao, wakingozwa na wakili wa muungano huo na seneta wa kaunti ya Siaya, James Orengo, walisema kuwa watafanya uchaguzi mwingine chini ya kipindi cha siku 90.
Aliyekuwa seneta wa Machakos, Johnston Muthama, alisema muungano huo uko tayari kumuapisha kiongozi wao.
" Wakimuapisha Uhuru, nasi tutamuapisha Raila," Muthama aliuambia umati wa watu uliokusanyika mjini Mavoko.
"Uchaguzi huru na wa haki ni lazima ufanyike ndani ya siku tisini," Orengo alisema.
Haya yalijiri huku tume ya uchaguzi na mipaka, IEBC, ikiendelea kujumulisha kura katika kituo cha kitaifa cha Bomas of Kenya.
Odinga alikiambia kituo cha televisheni cha CNN katika mahojiano ya moja kwa moja Ijumaa kwamba ni Wakenya milioni 3.5 tu ambao walitokea kupiga kura siku ya Alhamisi.
Hata hivyo, naibu wa rais na mgombea mwenza wa Uhuru Kenyatta, William Ruto, alikanusha vikali matamshi hayo ya Raila katika mahojiano na kituo hicho hicho siku ya Jumamosi.
"Raila anasema uongo. Ukweli wa mambo ni kwamba wapiga kura milioni 7.5 walijitokeza kwa zoezi hilo," Ruto alisema.
Kufikia Jumapili asubuhi, IEBC haikuwa imetoa idadi rasmi ya watu wote waliopiga kura.
No comments:
Post a Comment