Tuesday, October 31

Tarime kutoa shukrani kwa Mungu kwa ajili ya Lissu


Tarime. Chadema wilayani Tarime imechangisha Sh3.1 milioni kwa ajili ya matibabu ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tindu Lissu, ikisema imeuona mkono wa Mungu kupitia kwake.
Chama hicho kimesema kupitia hilo, wanachama watapita kwenye makanisa na misikiti kutoa shukrani kwa Mungu.
Mbunge huyo anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi katika makazi yake eneo la Area D mjini Dodoma Septemba 7,2017.
Katibu wa Chadema Mkoa wa Mara, Chacha Heche akizungumza leo Jumanne Oktoba 31,2017 wakati wa kuchangisha fedha hizo amesema chama hicho hakihubiri chuki bali upendo, amani na maendeleo kwa wananchi.
"Tumeuona mkono wa Mungu kwa kumrudisha kwetu Mheshimiwa Lissu, tutapita kwenye makanisa na misikiti kutoa shukrani kwa Mungu," amesema Heche wakati wa mkutano wa uchangiaji uliofanyika makao makuu ya Chadema wilayani Tarime. Sh3,134,500 zimekusanywa.
Mwenyekiti wa Chadema wilayani Tarime, Lucas Ngoto amesema, "Ni ukweli usiopingika kuwa Lissu hakuponywa na wanadamu, risasi alizopigwa ni nyingi lakini Mungu amekubali aendelee kuishi nasi hadi leo," amesema.
Peter Magwi ambaye ni katibu wa Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko amewataka wanachama na wapenda amani na maendeleo waendelee kutoa michango kusaidia matibabu ya Lissu.
"Maandiko katika vitabu vitakatifu yanasema usiogope. Watanzania tusiogope, tushauri na tukosoe kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu, kizazi cha sasa na  kijacho," amesema Magwi.

No comments:

Post a Comment