Friday, October 27

SWEDEN YAONESHA NIA YA KUWEKEZA KWENYE MIRADI YA NISHATI

Serikali inatumia mikopo inayoipata kutoka kwa wadau wa Maendeleo kwenye miradi ya uzalishaji na Miundombinu ili iweze kuwa na tija kwa Jamii na Serikali. Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Sweden Nchini Tanzania Bi. Katarina Rangnitt, Jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa, Serikali imejipanga kulipa madeni kwa wadau mbalimbali baada ya madeni hayo kuhakikiwa, hata hivyo amesema kuwa hatua za kukopa zitaangaliwa kwa umakini mkubwa ili kuzuia kuwa na madeni ambayo hayana tija kwa wananchi na Serikali. Tayari baadhi ya madeni yameanza kulipwa na Serikali imeendelea kutimiza ahadi zake ilizozitoa kwa wananchi kwa kuangalia vipaumbele vyenye kuleta matokeo chanya na ya haraka kwa wananchi, utekelezaji wake unazingatia weledi mkubwa ili kuhakikisha kero za wananchi zinatatuliwa kwa wakati.

“Aidha katika kuhakikisha Serikali inaendelea kuwahudumia wananchi ipasavyo, kumekuwa na mikakati ya kuwaongezea watumishi ujuzi ili kuendana na kasi ya maendeleo kuelekea uchumi wa kati kwa kuwa tuna uhaba wa watu wenye ujuzi wa kutosha, hivyo ni vyema wadau wa maendeleo wakalitazama hilo ili kusaidia katika kuharakisha ukuaji wa uchumi”, alieleza Dkt. Mpango.

Kwa upande wake Balozi wa Sweden nchini Tanzania Bi. Katarina Rangnitt amesema kuwa nchi yake inania ya kusaidia kukuza Sekta ya nishati na tayari mazungumzo na Wizara husika yameanza. Alielezea umuhimu wa Sekta Binafsi katika kukuza uchumi wa nchi ambapo amesema nchini mwake wafanyabiashara wanachangia pato la ndani kwa asilimia 50 kwa kuwa kuna biashara huria.

Waziri Mpango amesema kuwa Serikali inafanyajitihada za dhati kuhakikisha kuna mazingira bora ya biashara na ili kufikia huko kumekuwa na majadiliano ya mara kwa mara na wafanyabiashara nchini ambapo kero zao nyingi zimetatuliwa ikiwemo kupungua kwa uwingi wa kodi.

“Siwezi kuwa Waziri wa Fedha ikiwa sitakuwa na wafanyabiashara, kwa kuwa wao ndio wanaolipa kodi zinasosaidia kuendesha nchi”, aliongeza Dkt. Mpango.

Kuhusu utekelezaji wa Demokrasia na Haki za Binadamu, Dkt Mpango amesema kuwa mambo hayo yapo kikatiba na Tanzania inafuata katiba na kuiheshimu hivyo haki za binadamu zinafuatwa kwa mujibu wa sheria na hakuna yeyote anayependa haki zake zivunjwe. Hata hivyo ameeleza kuwa ni vema tamaduni za Mtanzania zikaendelea kuheshimiwa wakati wa utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano wa maendeleo. Alitoa wito kwa jamii kuendelea kutangaza yale mazuri yanayojitokeza nchini yakiwemo ya kukua kwa uchumi kwa kuwa Tanzania itajengwa na watanzania.

 “Inashangaza kuona baadhi ya watu wakieleza mabaya tu ili hali kuna mafanikio mengi yaliyopatikana, tunakaribisha ukosoaji lakini wenye tija” alifafanua Dkt. Mpango.

Pia, alisema Serikali inadhamira ya dhati ya kulinda wawekezaji wa ndani lakini amewataka wawekezaji hao kuungana kwa lengo la kuongeza nguvu na nyenzo bora ili watakapopata fursa ya kujenga miundombinu na mambo mengine, wafanye kwa ubora unaokubalika na wenye tija.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa nne kulia) na Balozi wa Sweden Nchini Bi. Katarina Rangnitt (wa pili kulia) pamoja na Maafisa Waandamizi kutoka pande hizo mbili wakiwa katika mkutano ulioangazia ushirikiano wa maendeleo, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa pili kulia) akizungumzia umuhimu wa kufuata utamaduni wa mtanzania katika kustawisha ushirikiano kati ya Tanzania na Sweden wakati wa mkutano na Balozi wa Sweden Nchini, Bi. Katarina Rangnitt, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Sweden Nchini Bi. Katarina Rangnitt (kushoto) akielezea Sekta ya biashara katika nchi yake inavyofanikisha kuchangia takribani asilimia 50 ya pato la ndani wakati wa Mkutano kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani) katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam, kulia ni Naibu Balozi wa Sweden Bw. Ulf Kallstig ambae pia ni Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano na Maendeleo.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto) na Balozi wa Sweden nchini Bi. Katarina Rangnitt wakijadili jambo baada ya kumalizika kwa mkutano kati ya pande hizo mbili katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment