Tuesday, October 24

Sura mbili za Odinga uchaguzi wa marudio wiki hii


Nairobi, Kenya. Kukiwa na dalili zote kwamba uchaguzi wa marudio wa rais ulioamriwa na Mahakama ya Juu utaendelea Alhamisi wiki hii bila kizuizi iwapo hakutakuwa na pingazimi la kisheria, kiongozi wa muungano wa Nasa, Raila Odinga anatafsiriwa ‘kuvaa sura’ mbili tofauti.
Odinga ambaye alijitoa siku chache zilizopita kuwania urais katika uchaguzi huo, hivi sasa anataka maridhiano yafanyike huku pia akisisitiza uchaguzi huo usifanyike.
Hata hivyo, mpinzani wake Rais Uhuru Kenyatta wa muungano wa Jubilee amekwishatangaza kuwa hatakubali maridhiano yoyote na Odinga mpaka hapo uchaguzi utakapomalizika.
Akizungumza baada ya kukutana na mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati katika jengo la Anniversary Towers mjini Nairobi, Odinga alisema kwamba ‘anatafakari’ iwapo ashiriki ama la katika uchaguzi huo.
Katika mkutano huo uliochukua takriban dakika 40, mwanasiasa huyo alitoka akiwa na ari mpya kuhusiana na mchakato wa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika wiki hii.
“Ikiwa mashauriano sahihi yatafanyika na ikiwa marekebisho sahihi yatazingatiwa na hofu ambazo tumezitoa zitashughulikiwa, basi tutafikiria kushiriki uchaguzi huo,” alisema Odinga.
Sura nyingine ya Raila ni ile ya kusisitiza kwamba uchaguzi huo hautafanyika akidaiwa kujiandaa kuwahamasisha wafuasi wake waugomee.
Katika mikutano mbalimbali ya hadhara aliyoifanya amekuwa akisisitiza kwamba, Oktoba 26 ni siku ya wafuasi wake kupumzika majumbani mwao kwa kuwa hakuna uchaguzi. Pia, amesema siku moja kabla ya uchaguzi atatoa mwongozo kwa wafuasi wake ambapo wadadisi wa mambo wanadhani huenda akawataka wasijitokeze kupiga kura au wafanye maandamano ambayo wameyasitisha.
Wakati Raila akisema hayo, wadadisi wa mambo wanasema mwanasiasa huyo huenda akabadili ‘gia angani’ dhidi ya Rais Kenyatta hata kabla ya Alhamisi kwa kuwa wanasiasa hao ni ‘marafiki’ linapokuja suala la masilahi ya Taifa lao. “Huitana kila wakati iwapo kuna mgogoro nchini,” anasema mmoja wa wachambuzi wa mambo ya kisiasa nchini humo .
Akizungumza katika Siku ya Mashujaa, Kenyatta alisema mgogoro wa kisiasa uliopo ni lazima umalizwe kwa masilahi ya Taifa.
Akizungumzia uchaguzi huo Jumatano iliyopita, mwenyekiti wa IEBC, Chebukati alisema hawezi kuthibitisha iwapo kutakuwa na uchaguzi huru na wa haki.
Hata hivyo, Chebukati alisema kwamba tume yake inaendelea kukamilisha taratibu za uchaguzi huo na itazingatia maelekezo yote yaliyotokana na hukumu ya Mahakama ya juu iliyotengua uchaguzi wa Agosti 8.

No comments:

Post a Comment