Thursday, October 19

Sheria iliyopo ina matundu mengi kudhibiti ajali za barabarani

Basi la abiria likiwa  limepata ajali mkoani
Basi la abiria likiwa  limepata ajali mkoani Shinyanga.Picha na Maktaba 
Licha ya kupigiwa kelele na elimu kutolewa kwa muda mrefu, ajali za barabarani zinaendelea kuwa tatizo sugu ambalo dawa yake bado haijapatikana.
Tukiadhimisha wiki ya usalama barabarani, Watanzania wanapaswa kutambua kuwa umefika wakati muafaka wa kukataa ajali zinazoepukika ili kunusuru maisha ya watu wasio na hatia ambao ni nguvukazi muhimu ya taifa.
Kulingana na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), ajali za barabarani zinapoteza maisha ya watu milioni 1.25 kila mwaka huku sehemu kubwa ya vifo na madhara ya ajali hizo yakitokea Afrika, kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwa moja ya nchi hizo.
Kwa Tanzania, inaelezwa karibu watu 4,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na ajali za barabarani.
Septemba mwaka jana, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni alitoa takwimu za ajali kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo kati ya mwaka 2013 hadi 2015. Takwimu hizo zinaonyesha kundi linaloongoza kwa kuathirika na ajali hizo ni abiria ambao kwa kipindi hicho, 3,444 walipoteza maisha na kuwaacha wengine 20,181 wakiwa na majeraha ya aina tofauti.
Watembea kwa miguu ni kundi linalofuatia kwenye orodha ya waathirika wa ajali za barabarani. Watembea kwa miguu 3,328 walipoteza maisha ndnai ya miaka hiyo mitatu huku 8,256 wakijeruhiwa kutokana na ajali hizo.
Wapanda pikipiki 2,493 walipoteza maisha na kuwaacha majeruhi 10,702 kw amiaka hiyo mitatu. Kwa upande wa baiskeli kulikuwa na vifo 1,071 pamoja na majeruhi 2,060.
Wamo wasukuma mikokoteni pia. Kutokana na shughuli zao kulazimika kutumia barabara zenye magari mengi kwa maeneo ya mjini, 81 walifariki na 246 kujeruhiwa.
Ripoti ya Hali ya Usalama Barabarani Duniani iliyotolewa na WHO mwaka 2015 inaonyesha ajali za barabarani zinaongoza katika kusababisha vifo vya vijana wenye kati ya u miaka 15 mpaka 29.
Inaonyesha asilimia 90 ya vifo vya ajali za barabarani vinatokea katika nchi zenye kipato cha chini na kati ambazo zina asilimia 54 ya magari yote yaliyopo duniani hizi sasa.
Kulingana na takwimu hizo ni wazi kuwa nguvu kazi kubwa inapotea kutokana na ajali na kusababisha madhara mengine mengi ikiwemo majeraha yenye maumivu makali, ulemavu wa kudumu, uharibifu wa mali na kuacha familia nyingi zikiwa tegemezi baada ya kuondokewa na watu wanaowategemea.
Fedha nyingi za umma zinatumika kununua na kutengeneza magari ya dharura ya wagonjwa, kutafuta damu kwa ajili ya majeruhi na kupata vitanda vya kutosha hospitalini. Si hayo tu, kiasi kikubwa cha fedha kinatumika kununua dawa na vifaatiba hospitalini kwa ajili ya majeruhi wanaotokana na ajali ambazo baadhi zingeweza kuzuilika endapo mambo kadhaa ya mmsingi yangezingatiwa.
Ripoti hiyo ya WHO inaonyesha ajali hizo nchini huathiri Pato l a Taifa (GDP) kwa wastani wa asilimia tatu kila mwaka. Nguvukazi inayopotea pamoja na majeruhi wanaoachwa ingetumika kwenye shughuli mbalimbali za ujenzi wa taifa ambazo zingekuwa na matokeo chanya katika uchumi wa nchi.
Wakati serikali ya awamu ya tano ikiweka mkazo wa kufikia uchumi wa kati mwaka 2025 kwa kuwa na idadi kubwa ya viwanda ni wazi dhamira hiyo njema itakuwa ngumu kendapo watu wataendelea kupoteza maisha kutokana na ajali. Viwanda vinahitaji kuendeshwa na vijana ambao ndiyo waathirika wakubwa wa ajali hizi.
Licha ya sababu tofauti zinazochangia kutokea kwa ajali za barabarani, nyingi husababishwa na uzembe wa madereva na udhaifu wa sheria iliyopo.
Kwa muda mrefu wadau na wanaharakati wa masuala haya wamekuwa wakipigia kelele kubadilishwa kwa Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 ili iwe msaada katika kupambana na ajali zinazoendelea kugharimu maisha ya watu kila kukicha.
Mwanasheria wa Chama cha Wanawake Wanasheria (Tawla), Mary Richard anasema kuna maeneo yenye mapungufu kwenye sheria hiyo ambayo yanashindwa kudhibiti udhaifu uliopo unaochangia ajali.
Nataja baadhi ya mmaeneo hayo kuwa ni vifungu vinavyozungumzia kudhibiti mwendokasi, ulevi, vizuizi vya watoto, mikanda na matumizi ya kofia ngumu.
Anasema sheria haijawataja abiria wanaopanda kwenye gari binafsi kufunga mkanda hali inayoweza kusababisha madhara makubwa ajali itakapotokea.
Anasema sheria hiyo inamtaja dereva na abiria aliyekaa kiti cha mbele kufunga mkanda hivyo kuwa dhaifu kwani ajali ikitokea haichagui madhara yaende kwa nani.
Pia sheria hiyo haijagusia chochote kuhusu vizuizi vya watoto. Licha ya kuwa watoto nao hupanda kwenye vyombo vya moto yakiwamo magari lakini hakuna mahali popote kwenye sheria ilipoelekeza vyombo hivyo kuwa na vizuizi maalum kwa ajili ya watoto.
Pamoja na sheria kutambua pikipiki kama chombo cha usafiri haijamlazimisha abiria kuvaa kofia ngumu, inaelekeza hivyo kwa dereva pekee yake.
Lakini, anaeleza, kila mmoja anafahamu madhara yanayowakuta abiria kwenye ajali za bodaboda. Wakati mwingine, dereva mwenye kofia hupona huku abiria wake akipoteza maisha au kujeruhiwa zaidi.
“Hata hivyo hakuna mchanganuo wowote kuonyesha ni aina gani ya kofia ngumu anatakiwa kuvaa mtu anayepanda pikipiki kwani si zote zinaweza kuhimili ajali ya barabarani inapotokea,” anafafanua Mary.
Kuhusu kiwango cha ulevi ambacho hakimruhusu dereva kuendesha gari, Kifungu cha 45 cha sheria hiyo kinamkataza mtu aliyekunywa zaidi ya kipimo kilichowekwa ambacho ni 0.08g/dl.
Mary anasema kiwango hicho ni kikubwa kikilinganishwa na kilichowekwa kimataifa ambacho ni 0.05g/dl kwa dereva mzoefu na 0.02g/dl kwa dereva asiye na uzoefu wa kutosha.
Kuhusu mwendokasi, anasema sheria ya sasa haijaeleza kwa kina.
“Kifungu cha 51(8) kinatambua maeneo machache katika kuzuia mwendokasi, ni muhimu sheria itamke maeneo yote na si ya mjini tu. Itamke wazi kuhusu maeneo ya makazi, shule, nyumba za ibada, maeneo ya michezo na mbuga za wanyama,” anasema Mary.
Mkurugenzi wa Tamwa, Edda Sanga anaunga mkono hoja ya kufanyika kwa mabadiliko ya sheria hiyo.
Anasema ipo haja ya kuunga mkono mabadiliko ya sheria hiyo kunusuru maisha ya wananchi na kusaidia kukuza uchumi wa taifa hata mwananchi mmoja mmoja.
“Kuendelea kutokea kwa ajali zinazosababisha vifo ni ishara mbaya, ipo haja ya kuweka mkazo katika kusukuma mabadiliko haya ya sheria yafanyike haraka iwezekanavyo,”
Kufanikish ahilo, anawaomba wabunge kuifanyia mabadiliko sheria hii ya mwaka 1973 kwa maslahi ya wananchi na rasilimali za taifa.
Licha ya kudhuru maisha, ajali huchangia uharibifu wa mali na wakati mwingine kuhatarisha mmaisha ya wanyamapori waliopo kwenye hifadhi tofauti za taifa ambako barabara kuu hukatisha.
Elimu ya kutosha inahitajika ili kila mmoja atekeleze wajibu wake awapo barabarani na kupunguza ajali zinazotokea.






No comments:

Post a Comment