Akiwa nchini China kuhudhuria mkutano mkuu wa 86 wa Taasisi ya Polisi ya Kimataifa (Interpol), Boaz alikaririwa na gazeti moja la Serikali akisema kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vina uwezo wa kuchunguza matukio ya uhalifu, yakiwamo mauaji na utekaji bila kusaidiwa na vyombo vya nje.
Hata hivyo, Sheikh Ponda aliyempigia simu jana mwandishi wetu, alisema kauli iliyotolewa na DCI haina ukweli.
“Kuna matukio mengi ya mauaji na maiti zimekuwa zikiokotwa, kuna utekaji hadi sasa wengine hawajulikani walipo,” alisema Sheikh Ponda na kuongeza:
“Tunashangaa kumsikia DCI akizungumzia uhodari wa Jeshi la Polisi katika kuchunguza matukio ya uhalifu, wakati tuna maswali mengi tunajiuliza.”
Alisema hadi sasa wananchi hawafahamu alipo Ben Saanane, ambaye ni Mkuu wa Idara ya Sera na Utafiti wa Chadema aliyetoweka tangu Novemba mwaka jana.
Sheikh Ponda alisema China ni nchi yenye maendeleo katika masuala ya ulinzi na usalama, hivyo ni vizuri wawakilishi wa Tanzania kwenye mkutano huo wakaeleza changamoto za usalama zinazotokea nchini ili wasaidiwe kuongeza ujuzi wa kukabiliana na uhalifu.
Kauli ya Sheikh Ponda imekuja wakati viongozi wa Chadema wakiitaka Serikali iruhusu vyombo vya nje kuchunguza tukio la kupigwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Kauli ya Mwigulu
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba alisema matukio mengi ya uhalifu yanaendelea kuchunguzwa na akataka jamii kutoa taarifa ambazo zitasaidia kukamatwa kwa wahusika.
Pia, Nchemba alisisitiza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vina uwezo wa kuchunguza matukio yote, hivyo wachunguzi kutoka nje ya nchi hawahitajiki.
No comments:
Post a Comment