Hayo yamo katika maelezo ya mshtakiwa wa saba, Ally Mussa Majeshi yaliyosomwa mahakamani na shahidi wa 10 wa upande wa mashtaka, Sajini Atway Omary baada ya kupokelewa kama kielelezo.
Maelezo hayo yalisomwa baada ya Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo, kutoa uamuzi mdogo wa kukataa pingamizi la upande wa utetezi kupinga maelezo hayo yasipokelewe kama kielelezo.
Jopo la utetezi linaloundwa na mawakili Hudson Ndusyepo, Majura Magafu, Emmanuel Safari na John Lundu walikuwa wakipinga wakisema mshtakiwa aliyatoa baada ya kuteswa na polisi.
Baada ya kutupilia mbali pingamizi hilo na kuungana na hoja za mawakili wa Serikali, shahidi huyo wa 10 akatakiwa kuyasoma maelezo hayo neno kwa neno.
Akisoma maelezo hayo, shahidi huyo ambaye ndiye aliyeyaandika katika Kituo cha Polisi Kigoma Oktoba 5, 2013, alisema mshtakiwa alimweleza kuwa waliahidiwa kulipwa Sh17 milioni kila mmoja kwa kumuua Msuya.
Kwa mujibu wa maelezo hayo, mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Sharifu Mohamed ndiye anayedaiwa kusimamia mpango huo na alihusika kuwakodi kwa ahadi ya kuwalipa kiwango hicho.
Katika maelezo hayo, mshtakiwa huyo amenukuliwa akisema Agosti 2013 akiwa nyumbani kwake Babati, alipigiwa simu na mshtakiwa wa pili Shaibu Jumanne akimtaka aende jijini Arusha.
Mshtakiwa huyo anaeleza kuwa Arusha alifikia katika nyumba ya kulala wageni ya mshtakiwa wa kwanza na kukutana na Jumanne na mshtakiwa wa nne, Jalila Zuberi au Said.
Siku hiyo hakuambiwa chochote bali siku iliyofuata aliongezeka mshtakiwa wa sita, Sadik Mohamed au Msudani na ndipo Sharifu alipowajulisha kuhusu mpango wa kumuua mfanyabiashara huyo.
Katika maelezo hayo, alinukuliwa akisema kuwa yeye alipangiwa kazi ya kwenda Hoteli ya SG inayomilikiwa na marehemu Msuya ili kumuuzia madini aina ya Tanzanite ambayo yangemvuta kuingia katika mtego.
“Baada ya kufika, nilimuuzia jiwe moja kati ya matatu niliyopewa na Sharifu kwa Sh3 milioni nikamwambia yaliyobaki nipo na mwenzangu na tukakubaliana kufanya biashara kesho yake,” alinukuliwa na kuongeza:
“Agosti 7, 2013 nilipangiwa kumtoa Msuya kutoka ofisini kwake hadi maeneo ya Kia (Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro) eneo la Mjohoroni ambako tungefanya biashara.”
Siku hiyo Majeshi aliondoka Arusha akiwa na Jabir na Sadik wakitumia gari aina ya Toyota Noah ikiendeshwa na mshtakiwa wa tatu, Mussa Mangu hadi maeneo ya Kia ambako walimshusha ili kumsubiri Erasto.
Akiwa hapo, bilionea Msuya akiwa na gari lake aina ya Range Rover alifika na kuondoka na mshtakiwa Majeshi kuelekea mji wa Bomang’ombe wilayani Hai ili kumfuata mshtakiwa wa tano, Karim Kihundwa.
Majeshi ananukuliwa akisema walipofika Bomang’ombe hawakumkuta Karim na alipowasiliana naye, alimweleza tayari alikuwa ameshafika eneo la Mjohoroni ambako Msuya aliuawa.
“Tulimkuta Karim pale Mjohoroni akiwa amevaa fulana nyekundu na suruali ya khaki akiwa ame-park (ameegesha) pikipiki kama mita 100. Erasto (Msuya) aliteremka na kumfuata Karim,” Majeshi ananukuliwa katika maelezo hayo.
Anaeleza kuwa baada ya kukutana na Karim, walikubaliana warudi kwenye gari (Ranger Rover) kwa ajili ya kufanya biashara. Msuya alipogeuka ili aende kwenye gari, Karim alitoa bunduki aina ya SMG.
“Msuya alipomuona Karim ametoa bunduki alijaribu kukimbia kuelekea kwenye gari lake, lakini Karim alimfyatulia risasi nyingi,” ananukuliwa mshtakiwa huyo katika maelezo hayo yaliyosomwa na shahidi wa 10.
Anasema baada ya kumuua, yeye na Karim waliondoka kwa kutumia pikipiki aina ya Toyo ambayo ilipata pancha na alipofika Sanya Juu alikodi pikipiki nyingine.
Alipoulizwa katika maelezo hayo kiwango walicholipwa kwa kazi hiyo, mshtakiwa alijibu kuwa kila mmoja alikuwa ameahidiwa Sh17 milioni, lakini hadi jana yake (alipokuwa anahojiwa) hakuwa amelipwa chochote.
Katika maelezo hayo, anasema alikuwa hajui sababu za kuuawa Msuya na kwamba katika kufanikisha mpango huo, Sharifu alinunua pikipiki na kuwapa kila mmoja simu mpya na laini.
Baada ya kumaliza kusoma maelezo hayo, wakili wa Serikali, Kassim Nassir alifunga kumhoji shahidi huyo na mawakili wa utetezi walipata fursa ya kumhoji.
Wakili Ndusyepo: (Akirejea maelezo ya mshtakiwa). Naomba fungua ukurasa wa sita. Ni kweli wakati unamuuliza maswali alichokkuwa akikujibu ndicho ulichokuwa unaandika?
Shahidi: Ni sahihi.
Wakili Ndusyepo: Je, kuna swali uliuliza: “Baada ya kufika marehemu akakuchukua hapo Kia mlikwenda wapi”. Ni kweli uliuliza hilo swali?
Shahidi: Ni kweli.
Wakili Ndusyepo: Ufahamu wa kuuliza: “Alipokuchukua hapo Kia mlikwenda wapi” uliupata wapi?
Shahidi: Yeye mwenyewe alinijbu.
Wakili Ndusyepo: Unasema nini tukikwambia tayari ulihusika katika mahojiano mengine na ulikuwa unampandikizia majibu mshtakiwa utasemaje?
Shahidi: Hilo siyo kweli.
Wakili Magafu: Kati ya Majeshi, Karim na Sadick ni yupi mliyeanza kumkamata?
Shahidi: Karim na Sadick ndiyo walianza kukamatwa.
Wakili Magafu: Unaweza kukumbuka Sadick na Karim walikamatwa kule Kaliua (Tabora) lini?
Shahidi: Septemba 13, 2013.
Wakili Magafu: Mlifanikiwa kuwahoji mlipowakamata?
Shahidi: Mimi sikuwahoji.
Wakili Magafu: Uliwahi kuwasikia walichokuwa wanakisema kwenye mahojiano?
Shahidi: Hapana.
Wakili Magafu: Utakubaliana na mimi kuwa katika maelezo yako ulisema mliwahoji?
Shahidi: Ni pale tulipowakamata
Wakili Magafu: Ni nani alikwambia Ally Majeshi aliwahi kukamatwa na kupelekwa gerezani hadi umuulize hilo swali?
Shahidi: Ni yeye mwenyewe aliniambia.
Wakili Magafu: Ebu soma hilo swali ulilomuuliza.
Shahidi: Nilimuuliza katika shughuli zako za kilimo uliwahi kukamatwa na kupelekwa gerezani?
Wakili Magafu: Kabla ya hilo swali ulimuuliza swali gani?
Shahidi: Alinieleza alimaliza darasa la saba, lakini hakufaulu.
Wakili Magafu: Nenda kwenye lile swali linalohusu taarifa za mauaji ya Erasto Msuya.
Shahidi: Nilimuuliza: “Ulipata wapi taarifa za mpango wa kumuua Erasto Msuya?”
Wakili Magafu: Hilo swali ni nani alikwambia mshtakiwa wa saba alihusika katika mauaji hadi umuulize hilo swali?
Shahidi: Yeye mwenyewe ndiye alisema hivyo.
Wakili Magafu: Katika hayo maelezo umeibuka tu na hadithi ya Sadick. Je, kwenye hayo maelezo kuna mahali popote anaposema siku ya kwanza alikutana na Karim?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili Magafu: Ebu tusaidie, uliwahi kumuuliza Karim kama walikuwa wanafamihana na Majeshi?
Shahidi: Sikuwahi kumuuliza.
Wakili Magafu: Soma pale ulipoandika walipokutana siku ya kwanza. Kuna jina la Karim?
Shahidi: (Baada ya kusoma) Hakuna. Hapa hajamtaja.
Wakili Magafu: Uliwahi kumuuliza mshtakiwa kwa nini waliamua kumuua marehemu (Msuya)?
Shahidi: Alisema hata yeye hajui
Wakili Magafu: Uliwahi kumuuliza ni kwa nini hakuwauliza wenzake sababu za kumuua marehemu?
Shahidi: Wala sikumuuliza.
Wakili Magafu: Utakubaliana na mimi kuwa mpaka sasa hivi hapo ulipo hujui sababu ya mauaji ya Erasto Msuya?
Shahidi: Sijui.
Wakili Safari: Nikikwambia habari hizo ulizoandika uli-take advantage (fursa) ya kile alichokueleza Jalila kwa sababu ni ndugu na Majeshi?
Shahidi: Mimi sikuwahi kumhoji Jalila.
Wakili Safari: Katika maelezo yako hayo, uliwahi kumuuliza fedha ile ya marehemu aliyokuwa anunulie madini siku ile ilikwenda wapi?
Shahidi: Sikuuliza hilo.
Wakili Safari: Marehemu alikuwa anakwenda kufanya biashara, kwa nini hukuuliza hilo swali?
Shahidi: Sikuuliza.
Wakili Safari: Nikikwambia hayo uliyoandika uliambiwa na mabosi zako baada ya kuchukua fedha ya marehemu utasemaje?
Shahidi: Siyo kweli.
Wakili Safari: Kwa kutoongelea fedha ya marehemu, unakubaliana na mimi wakati wote uliowataja kwenye hayo maelezo uliyoyaandika, ulifanya hivyo kwa maelekezo ya Samwel (shahidi wa tisa)?
Shahidi: Siyo kweli.
Naye Wakili Nundu aliomba apewe maelezo ya shahidi huyo aliyoyaandika polisi baada ya kumaliza kazi ya kukamata washtakiwa ili kuonyesha mkanganyiko wa kile anachokisema.
Wakili Nundu alisema anaomba maelezo hayo kwa kuegemea vifungu 154 na 164 (1) (c) vya sheria ya ushahidi, lakini baada ya upande wa mashtaka kupinga, wakili huyo aliondoa hoja yake.
Msuya aliyekuwa akimiliki vitega uchumi kadhaa ndani na nje ya Arusha, aliuawa kwa kwa kupigwa risasi Agosti 7, 2013 maeneo ya Mijohoroni wilayani Hai.
No comments:
Post a Comment