Siku chache zimesalia kura mpya ya urais ipigwe mnamo Oktoba 26. Lakini, swali kuu ni je, uchaguzi huo utafanyika ama la?
Hii ni kwa sababu muungano wa National Super Alliance (Nasa) unaoongozwa na Raila Odinga na aliyekuwa makamu wa Rais Kalonzo Musyoka, unasisitiza kuwa zoezi hilo halitafanyika bila marekebisho machache kufanyiwa tume ya uchaguzi (IECB).
Fauka ya hayo, Nasa inataka kampuni ya Al-Ghurair ambayo ilipewa zabuni ya kuchapisha karatasi za kura na kampuni ya OT-Morpho iliyopewa kandarasi ya miaka miwili kusimamia na kununua mashine ya kupigia kura ya kielektroniki maarufu kama KIEMS, zisitumike.
Malalamiko ya Nasa ni kwamba, kampuni hizi mbili zilishirikiana na baadhi ya makamishna, wafanyakazi na Mtendaji Mkuu wa IEBC, Ezra Chiloba kuiba kura.
“Hii ni kama kupelekwa kichinjioni ilhali tunajua waliohujumu kura bado wana nafasi ya kufanya hivyo tena.
Nasa inamlenga Chiloba ambaye wanadai ni kizingiti kikuu cha upigaji wa kura iliyo wazi na huru. Muungano huu umeapa hautashiriki kura hiyo hadi mahitaji na malalamiko yao yapate suluhu.
Muungano huu ambao unaamini ushindi wa mgombea wake wa urais Raila Odinga aliporwa ushindi, umeapa utaendelea kufanya maandamano kushinikiza Chiloba ang’atuke.
Maelfu ya wafuasi wa Nasa wameitikia wito wa Raila na viongozi wenza kuandamana nchini kote kila Jumatatu, Jumatano na Ijumaa hadi Chiloba aondoke.
Hatua hii ya Nasa imekuwa kizugumkuti kwa IEBC na chama cha Jubilee cha Rais Uhuru Kenyatta. Wabunge wa Jubilee ambao wana uwingi bungeni na seneti wameanza mchakato wa kurekebisha baadhi za kanuni za uchaguzi na kuzua kizungumkuti kingine.
Jubilee sasa inakusanya maoni kutoka kwa umma kuhusu ni vipengele vipi kati ya vipengele 12 vilivyopendekezwa vinavyofaa kuondolewa ama kupewa uzito zaidi.
Hoja hiyo inaungwa mkono tu na wabunge wa Jubilee kwa sababu wabunge na maseneta wote wa upinzani wamesusia Bunge na seneti hadi uchaguzi mpya ufanywe. Wanadai hawatambui urais wa Uhuru Kenyatta kwa sababu kura ya Agosti 8 iliibwa na sasa amepoteza nguvu za kuongoza nchi baada ya Mahakama ya Juu kutupilia mbali ushindi wake na kusema kura mpya ifanywe chini ya miezi miwili.
Wabunge na maseneta wa Nasa hawakuudhuria sherehe za ufunguzi wa Bunge mwezi mmoja uliopita wakisema Uhuru si rais halali. Ni kura hii mpya ambayo imeleta matatizo na mikinzano kati ya upinzani na chama tawala cha Jubilee. Kila upande unavuta kamba…hatimaye, kamba inaweza kukatika.
Yanayoendelea Kenya wakati huu si mazuri. Jubilee inataka kubadilisha kanuni za kura ikidai inalenga kufunga mianya ambayo ilisababisha kasoro zilizosababisha ushindi wa Uhuru kufutwa na Mahakama ya Juu huku majaji wanne kati ya sita wakikubaliana na hoja za Nasa kuwa Uhuru aliibiwa kura na IEBC, Al-Ghurair na OT-Morpho.
Nasa bado inalia kwa sababu kampuni hizi mbili pamoja zitashiriki kwa njia moja au nyingine katika uchaguzi wa Oktoba 26. Chiloba naye na maofisa wengine wa tume hiyo hawajaadhibiwa ingawa mkuu wa mashtaka ya umma Keraiko Tobiko ameanzisha uchunguzi wa wale wanaoshukiwa walihujumu kura ya Agosti 8.
Pia, Tobiko amesema ofisi yake inamchunguza ajenti mkuu wa Jubilee, Daves Chirchir kwa sababu barua pepe yake ilitumiwa mara nyingi kuingia kwenye tarakilishi za kupigia kura na kubadili ama kufuta Fomu muhimu za 34A na 34B. Hizo ni stakabadhi muhimu sana katika usimamaizi wa kura na zikikosekana ama zikikosa kusainiwa na maofisa wanaosimamia upigaji wa kura katika maeneo Bunge na vituo vya kupigia kura, basi zoezi hilo hushamiri doa.
Kutokana na mizozo kati ya mirengo hii mbili za siasa nchini, kuna hofu nchi inaweza kukumbwa na ghasia.
Nchi za ughaibuni zimesema Raila na Uhuru hawana budi kuzungumza na kuelewana kuhusu masuala yanayozozaniwa na Nasa na Jubilee.
Kupitia kwa mabalozi wao, Marekani, Uingereza na Ujerumani miongoni mwa nchi nyingine, zimewazomea viongozi wanaozozana na kuwaonya watapigwa marufuku kusafiri ughaibuni.
Nasa imeambiwa iache kushinikiza mabadiliko katika IEBC, wachapishaji wa karatasi za kura na usimamizi wa tarakalishi za kupigia kura.
Jubilee haikuzaswa. Mabalozi hao wanataka viongozi wa chama hiki waache kubuni sheria mpya bungeni ikisema hatua hiyo ni kinyume cha Katiba.
Nasa, huku ikiendelea kuonyesha ubabe wao kwenye ulingo wa maandamano licha ya makabiliano na polisi, inasema matamshi ya mabalozi hayatawatingisha hata robo. Maseneta James Orengo na Moses Wetangula wanasisitiza kamwe Nasa hawatalegeza kamba hadi vikwazo vyote vitakavyozuia kura huru na wazi, vitaondolewa. Kwa hivyo, wamesema siku za maandamano zitaongezeka kutoka mbili hadi tatu kila wiki.
Nasa inasema Jubilee inabadilisha kanuni za upigaji kura ili waweze kuiba kura bila wasiwasi. Ikijitetea, Jubilee inasema inajaribu kuweka kanuni zinazoweza kukinga kura isije ikawa na dosari zilizosababisha Nasa kwenda mahakamani na hatimaye, ushindi wa Uhuru kupuuziliwa mbali.
Wadadisi wa siasa wanasema, Rais Uhuru akiweka sahihi yake kwenye mabadiliko hayo, kutakuwa na mizozo zaidi.
Jubilee haitishwi na malalamishi na maandamano ya Nasa kwa sababu wameapa kumuapisha Uhuru ikiwa Raila hatashiriki kwenye uchaguzi wa Oktoba 26.
Migogoro ya Nasa na Jubilee imeathiri uchumi vibaya sana. Wafanyabiashara wanahofia mizozo hii na sintofahamu inayoshamiri katika mazingira ya kisiasa, imedidimiza biashara zao.
Lakini, hali ya kutatanisha ni kuwa hakuna anayetuhumu wizi wa kura. Makanisa nayo yamejifanya kana kwamba kila kitu kiko shwari. Ni Kanisa la Kianglikana tu ambalo linaonekana likishinikiza washikadau wa uchaguzi wafikirie hatma ya baadaye ya nchi kwa kuzingatia kura wazi na huru.
Kwa sababu ya ukabila uliokithiri nchini, hata makanisa sasa aidha yanaegemea Nasa ama Jubilee. Wakristo nao wanafanya vivyo hivyo. Hii si nzuri. Wakristo na makanisa yanafaa kutoegemea upande wowote kwani ufalme wao uko mbinguni. Lakini ni ajabu kwamba katika nchi ambayo asilimia 88 ni Wakristo, ukabila na wizi wa kura zimenawiri.
Hakuna watu wanaoweza kusimama kidete na kusema ukweli wa mambo. Kila mmoja anatetea Jubilee ama Nasa hata kama wanajua vizuri kuwa upande mmoja ama zote zina makosa ambayo yanafaa kutajwa na kurekebishwa.
Nasa na Jubilee wanafaa kuweka tofauti zao nyuma na kuanza kufikiria juu ya nchi. Vyama vinakuja na kwenda; viongozi pia vilevile lakini Kenya itabaki kwa minajili ya vizazi vijavyo.
Nasa isiposhiriki kwenye kura, kwa hakika, Kenya inaweza kuporomoka kwa sababu ya siasa za kijinga. Kuna wale wanaosema, Jubilee wakiapisha Uhuru baada ya Oktoba 26, Raila pia ataapishwa. Kutakuwa na marais wawili kwa nchi moja.
Nasa pia wana ndoto ya kupigania uhuru wa nchi yao itakayoitwa People’s Republic of Kenya.
Hii yamaanisha Kenya itagawanywa mara mbili.
Baadhi ya wanasiasa wa Jubilee wamemsihi Uhuru awe kiongozi wa kihimla ili awaadhibu vikali wanasiasa wanaompinga na kumea pembe.
Tunaona wanasiasa wa upinzani kama vile Johnson Muthama, Babu Owino, Gladys Wanga wakifikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuchochea umma.
Muthama na Owino wanasema wanasingiziwa mashtaka na Jubilee. Pia, mashirika yasiyo ya kiserikali yamefungiwa akunti zao kwa madai kuwa aidha yanaunga mkono upinzani ama yanachangia katika maamuzi yanayofanywa na majaji.
Nalilia nchi yangu!
No comments:
Post a Comment