Wednesday, October 18

Picha za Lissu mtandaoni zaibua hisia


Dar es Salaam. Picha za Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu zilizoanza kusambaa mitandoni saa kumi jioni leo Jumatano Oktoba 18,2017 zimeibua hisia kutokana na maendeleo ya afya yake.
Lissu ambaye pia ni mwanasheria wa Chadema anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi nyumbani kwake Area D mjini Dodoma, Septemba 7 mwaka huu.
Katika kurasa za kijamii za Mwananchi za Facebook, Twitter na Instagram watu mbalimbali wametoa maoni kuhusu picha hizo, wengi wakionekana kuguswa na maendeleo ya afya yake.
Josephat Mwambola amesema, ‘‘Watu wasiojulikana watambue kuwa Mungu yupo na anawajua ipo siku atawaweka hadharani na kuwaadhibu zaidi ya walivyomuumiza Tundu Lissu ambaye ni mtetezi wa kweli wa wanyonge hapa nchini Tanzania.’’
Babuu Makundi ameandika, “Sifa na utukufu ni kwa Mungu wetu aliye juu Mungu ana makusudi na uhai wa Lissu.”
“Mungu akisema ndiyo hakuna wa kuzuia. Akisema hapana hakuna wa kupinga. Jeshi la mbinguni lilisimama juu yake. Ukimtafakari Mungu. Huwa hachunguziki. Ana makusudi na mwanaye Lissu. Nami nasema asante Yesu,” ameandika Renatha Joely.

No comments:

Post a Comment