Tuesday, October 10

Mwakilishi ahoji sababu za wingi wa ajali Z’bar

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar, Mohamed Ahmada Salum 
Zanzibar. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imesema sababu kuu za ajali za mara kwa mara ni uzembe wa baadhi ya madereva na kutozingatia alama za barabarani.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar, Mohamed Ahmada Salum aliyasema hayo jana katika kikao cha Baraza la Wawakilishi wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Chake Chake, Suleiman Sarahan Said aliyehoji kwanini sheria za usalama barabarani zilizopo hazijasaidia kutatua suala la ajali za barabarani.
Pia mwakilishi huyo alisema sababu anayoiona ni ukosefu wa alama za barabarani na hivyo Serikali kutoa adhabu kwa madereva ni sawa na kuwaonea.
Akijibu swali hilo, Salum alisema pamoja na uwapo wa uhaba wa alama za barabarani, lakini uzembe wa madereva ndilo tatizo kubwa.
“Pamoja na hilo lakini suala la sheria linamwajibikia kila mmoja wetu, hivyo hatutakuwa tayari kuona uzembe unafanyika kisha tusimchukulie hatua za kisheria dereva kwa kosa lake la makusudi,” alisema Salum.
Hata hivyo mwakilishi huyo alisema kuwa licha ya uchache wa alama hizo lakini katika baadhi ya maeneo zipo isipokuwa kinachofanywa na baadhi ya madereva hao ni kuzipuuza na kusababisha ajali. Alisema kuwa pamoja hali hiyo kuna baadhi ya watu wamekuwa wakiharibu miundombuni ya barabara kwa makusudi, hali ambayo nayo huchangia kutokea kwa ajali.
Alisisitiza kwamba si jambo la kufurahisha kuona Serikali inafanya jitihada kubwa kujenga miundombinu kwa manufaa ya wananchi, lakini liwepo kundi ambalo linaiharibu. “Tunashirikiana na polisi kutoa elimu kwa madereva na wananchi juu ya matumizi sahihi ya barabara ili kila mmoja awajibike kwa mujibu wa nafasi yake,” alisema Salum.

No comments:

Post a Comment