Thursday, October 12

MVUA ZALETA MAAFA TABORA, WATANO WAPOTEZA MAISHA

Na Tiganya Vincent, RS-Tabora

WATU watano wakazi wa Wilaya ya Igunga wamefariki duniani katika matukio mawili tofauti kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Tabora.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora Wilbroad Mtafungwa amesema hayo leo wakati wa mkutano  na waandishi wa habari. Alisema kuwa katika tukio la kwanza mnamo tarehe 11 mwezi huu, watu wanne wamefariki dunia baada ya kuangukiwa na ukuta wa nyumba waliyokuwa wakiishi kufuatia mvua zilizonyesha kwa kipindi cha siku mbili.

Kamanda Mtafungwa alisema waliofariki kwa kuangukiwa na ukuta wanatoka kijiji cha Igogo kata ya Nanga na aliwataja kwa majini kuwa ni Kagwa Makenza(80) ambaye pia ni mmiliki wa nyumba iliyosababisha maafa hayo, wengine ni Sande Dule (6), Butonda Shija(3) na Mbula Dule mwenye miezi miwili.

Alisema watoto wote watatu walifariki dunia wakati wakipata matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga.

Katika tukio la Pili , Kamanda Mtafungwa alisema katika kijiji cha Bulyang’ombe kata ya Nanga mtoto Zenga Tano (5) alifariki dunia baada ya kupigwa na radi mnamo tarehe 10 mwezi huu wakati amelala na wazazi wake.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Igunga John Mwaipopo alitoa pole kwa familia za waliopatwa maafa na kuwashauri wakazi wa Igunga kufuata utalaamu wa ujenzi wakati wa ujenzi wa nyumba zao ili kuepuka maafa zaidi.

Alisema kuwa ushauri huo ni pamoja na ujenzi katika sehemu ya miinuko kwa ajili ya kujikinga na maafa zaidi.

No comments:

Post a Comment