NA BASHIR YAKUB -
1.UKOROFI WA WASIMAMIZI WA MIRATHI.
Baadhi ya wasimamizi wa mirathi ni wakorofi. Baada ya kuteuliwa kwa jukumu hilo hawapendi kugawa mali ili kila mtu achukue chake. Inapaswa kufahamika kuwa mali si za msimamizi wa mirathi . Mali ni za warithi halali isipokuwa msimamizi ni kiongozi tu. Kwa maana hii anawajibika kusikiliza warithi wanasema nini ili mradi kile wanachosema kisipingane na sheria.
Wakati mwingine warithi wanataka wagawiwe mali zao ili kila mtu endelee na maisha yake lakini msimamizi hataki tena bila sababu za msingi. Hili linakuwa si sawa isipokuwa kama kuna sababu za msingi za kufanya hivyo.
Sababu zaweza kuwa labda anayetaka kugawiwa mali ni mtoto mdogo asiyeweza kumiliki mali kwa wakati huo, ni mtu asiye na akili timamu kwa muda huo, kuna shauri mahakamani kuhusu hiyo mirathi linaendelea, mali hazijakusanywa zote, kuna ugomvi kwa warithi kuhusu mali ambao utaathiri mgao nk.
2. WAJIBU MKUU WA MSIMAMIZI WA MIRATHI.
Kifungu cha 108(1) cha Sheria ya Usimamizi na Uendeshaji wa Mirathi, Sura ya 352 kinaeleza wajibu wa jumla wa msimamia mirathi. Kifungu kinasema kuwa kazi kubwa ya msimamizi wa mirathi ni kukusanya, mali na madeni ya marehemu,kutunza mali hizo, kusimamia gharama za mazishi na msiba, na kugawa mali kwa wanaostahili. Na kazi hii yote ifanyike kwa uadilifu mkubwa.
Kwahiyo kumbe moja ya kazi ya lazima na ya kisheria ya msimamizi wa mirathi ni kugawa mali kwa warithi. Huu ni wajibu ambao msimamizi anawajibika kuutekeleza. Na atagawa kwa mujibu wa wosia au sheria husika kama hakuna wosia. Hagawi anavyotaka yeye. Nani apate nini halipo katika hiari yake.
3. MUDA WA KUGAWA MALI KWA WARITHI.
Kifungu cha 107 cha Sheria ya Usimamizi na Uendeshaji wa Mirathi kinasema kuwa ndani ya miezi sita tokea kuteuliwa kwa msimamizi wa mirathi, msimamizi huyo anatakiwa kupeleka taarifa(inventory&account) mahakamani akionesha ni namna gani amekusanya mali za marehemu, madeni, amelipa gharama kama zipo na kwa namna gani amegawa kwa wahusika.
Kwahiyo kazi ya kugawa yafaa ifanyike ndani ya miezi sita. Hii ina maanisha inaweza kufanyika hata ndani ya mwezi mmoja tokea kuteuliwa ikiwa atakuwa amekamilisha taratibu zote.
Kifungu kinasema ikiwa ndani ya miezi sita hajapeleka taarifa (inventory&account) mahakamani na kuna sababu za msingi na za kisheria za kutofanya hivyo basi iwe ndani ya mwaka mmoja. Ikiwa ndani ya mwaka mmoja itashindikana kwasababu za msingi na za kisheria basi anaweza kuongezewa muda na mahakama hadi miezi mingine sita.
Pamoja na hayo sheria hiyo imetoa uhuru kwa mahakama kutoa amri au agizo la kugawa mirathi kwa warithi halali katika muda ambao itaona unafaa na kupendeza. Kuna muda mahakama inaweza kuamrisha hata ndani ya wiki tatu mali iwe imegawiwa na taarifa imerejeshwa mahakamani.
Mara nyingi amri za namna hii hutolewa kutegemea na udharula wa mazingira husika na kinachohitajika.
4. NINI UFANYE IKIWA MSIMAMIZI HATAKI KUGAWA MALI.
Ikiwa msimamizi hataki kugawa mali na hakuna sababu za kisheria zinazomzuia kugawa basi lipo jambo moja unaweza kufanya.
Ni kutoa taarifa katika mahakama ambayo imemteua/kumthibitisha.Utapeleka malalamiko yako hapo halafu ataitwa kwa wito(summons) na atatakiwa aoneshe sababu(show cause) kwanini hagawi mali kama sheria inavyotaka. Haufungui kesi ila unapeleka tu taarifa.
No comments:
Post a Comment