Wednesday, October 11

Mpinzani aponda Serikali, Mahakama ya Katiba


Lusaka, Zambia. Rais wa chama cha upinzani chaUnited Party for National Development (UPND), Hakainde Hichilema ameishambulia serikali na akaiita Mahakama ya Katiba kuwa ya walarushwa.
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake New Kasama jana, Hichilema amesema Rais Edgar Lungu anaongoza genge la wahalifu ambalo linaendesha mipango ya kifisadi nchini.
Alisema watu waliokuwa wanamsema kwamba amepunguzwa makali baada ya kukaa kwa miezi kadhaa mahabusu watajisikitikia wenyewe kwani kwa sasa ni madhubuti zaidi. Pia alisema ataheshimu kufanya majadiliano na Rais Lungu.
"Ila siku hizi wala sisemi kwa kuzunguka, nasema wazi kwamba Jaji Anne Sitali ni fisadi, Palan Mulonda ni fisadi, Mungeni Mulenga pia fisadi. Hii ndiyo sababu tunatoa wito kuwa Mahakama ya Katiba ifumuliwe," amesema.
Mahakama ya Katiba imejitengenezea wigo kwamba maamuzi yake mtu hawezi kukata rufaa lakini ndiyo ilisaidia rufa juu ya mawaziri waliobainika wakihudumu kinyume cha sheria baada ya Bunge kuvunjwa.
Hichilema amesema idara ya mahakama inapaswa kuvunjwa na kutimuliwa wote kwa kuwa imevamiwa na sura za kifisadi.
Kadhalika kiongozi huyo wa UPND amemshutumu Spika wa Bunge la Taifa Patrick Matibini akimwita kuwa ni wakala wa chama tawala cha Patriotic Front.
"Ikiwa kuna genge la wezi basi lazima awepo kiongozi wa genge hilo na sote tunamfahamu kiongozi huyo ni nani," amesema.
Hichilema amesema mjadala uliopendekezwa na Jumuiya ya Madola ulikuwa muhimu kwa ajili ya kusaidia kurejesha uhusiano mzuri kati ya serikali na upinzani. Alisema alishtushwa kusikia baadhi ya watu wakimtaka akae kimya licha ya kutopatiwa ufumbuzi masuala kadhaa kuhusiana na uchaguzi mkuu wa mwaka 2016.
Hichilema alisema watu wanaweza kumlaumu kwa kuanzisha mashambulizi dhidi ya serikali kuhusiana na matokeo ya uchaguzi lakini hatanyamaza. Alisema Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zambia, Jaji Esau Chulu lazima ajiuzulu na afuate nyayo za mkurugenzi wa ECZ Priscilla Isaacs ambaye mkataba wake haukuhuishwa.

No comments:

Post a Comment