Makani aliyasema hayo jana wakati wa matembezi ya hisani kuadhimisha miaka 40 ya Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET), yalioanzia viwanja vya Karimjee hadi Leaders, Kinondoni.
Makani ambaye kabla ya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyotangazwa Jumamosi na Rais John Magufuli alikuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, alisema wahandisi ndiyo wenye jukumu la kufanya kazi yao ionekane nzuri yenye kiwango iwapo watajitokeza na kupaza sauti.
Alisema kazi ya viongozi wa Serekali ni kufungua milango na kwamba, iwapo kutakuwa na udanganyifu jamii itawaangalia wahandisi kwa sababu ndiyo wasomi na wenye taaluma.
Hata hivyo, Makani alisisitiza kuwa Serikali haitaweza kufikia uchumi wa viwanda kama wahandisi wa ndani hawatashirikishwa.
“Niendelee kusisitiza katika mpango mkakati wa Serikali uwe wa mwaka mmoja au mitano, lazima wahandisi wahusike ili kufikia uchumi wa viwanda,” alisema Makani.
Aliongeza kuwa changamoto kubwa wanayoipata katika taasisi ya wahandisi ni kukosa mitaji, ikiwamo ya kununulia vifaa vya teknolojia mbalimbali za uhandisi.
Naye Rais wa IET, Ngwisa Mpembe alisema matembezi hayo yana lengo la kuhamasisha vijana kupenda masomo ya sayansi na kuchangisha fedha ili kununua vifaa vya maabara.
Mpembe alisema kuwa lengo lao katika matembezi hayo ni kupata Sh50 milioni ili kutekeleza azma ya kuwasaidia wanafunzi kufanya vizuri kwenye masomo ya sayansi.
Aliongeza kuwa tayari wameanza kupita shule mbalimbali ambazo zinaendesha mashindano ya kuandika insha, ambayo yatafungwa Ijumaa hii na mshindi atatangazwa.
Mpembe aliwataka wanafunzi kushiriki mashindano hayo na kujenga tabia ya kupenda masomo ya sayansi katika kufikia uchumi wa viwanda.
No comments:
Post a Comment