Wiki iliyopita Rais John Magufuli alitupilia mbali maombi ya madiwani wa Tanzania ya ongezeko la posho au kipato chao, maombi ambayo waliyatoa kwa Serikali. Magufuli alitoa maamuzi hayo wakati akihutubia mkutano wa ALAT jijini Dar es Salaam.
Kwa rekodi za sasa, madiwani wanalipwa Sh350,000 kama posho ya kila mwezi. Maombi yao kwa serikali yalikuwa walipwe Sh800,000 au 1,000,000 na ndipo Rais Magufuli akayapiga marufuku.
Ukiyatizama malipo ya madiwani kwa mwezi, unagundua kuwa wanazungukwa mara 34 na wabunge, bila kujali kuwa hawa ni kada ya wawakilishi wa wananchi ambapo madiwani ni wawakilishi ngazi ya kata na wabunge ngazi ya majimbo na kazi zao zinapimwa kwa namna wanavyokaa na kutatua matatizo ya wananchi kupitia serikali.
Hoja na Uthibitisho
Nataka ifahamke kuwa Sh350,000 wanazolipwa madiwani kila mwezi kama posho (bila makato) si pesa kidogo. Hizi ni pesa nyingi kushinda hata mishahara ya kima cha chini ya wafanyakazi ambao wanahudumia wananchi kwenye sekta nyeti usiku na mchana, kwa hiyo malipo ya kiasi hicho cha pesa ni makubwa kwa ulinganifu wa mishahara nchini Tanzania.
Ndiyo maana andiko hili linaweza kuwastua baadhi ya watu na wakajiuliza kwa nini msimamo wangu ni madiwani walipwe vizuri zaidi. Msingi wa hoja yangu uko kwenye kategoria ya kazi ya udiwani; udiwani siyo utaalamu, ni kazi ya kujitolea kuwawakilisha wananchi na mtu hafanyiwi mahojiano ili kuwa diwani, anapigiwa kura.
Kategoria ya kazi ya udiwani inawahusu pia wabunge, wabunge ni wawakilishi wa wananchi, kategoria hii inawahusu pia wenyeviti wa mitaa, wenyeviti wa vijiji na wenyeviti wa vitongoji. Kwa leo sitazungumza chochote kuhusu wenyeviti hawa.
Msingi wa malipo ya udiwani ulipaswa kujengwa kwenye kategoria ya kazi hiyo, kazi ya uwakilishi wa wananchi. Hii ni kategoria sawa na wabunge na Rais, japokuwa kwa Tanzania urais una utendaji ndani yake, maamuzi zaidi kuliko uwakilishi peke yake, kwa hiyo kwa sasa tunaweza kumtoa rais kwenye mjadala na tusihoji malipo yake na uhalali wake ili tuwajadili wawakilishi wa moja kwa moja, wabunge na madiwani.
Malipo Tofauti kwa Kazi Moja
Madiwani na wabunge wanafanya kazi moja na tena kwa uzito mmoja na tukubaliane kuwa yapo majimbo mengi ambayo watendaji wake wakuu na wawakilishi wa wananchi wa majimbo hayo ambao hawalali ni madiwani kuliko wabunge, na tukubaliane kuwa sehemu kubwa ya madiwani wanafanya kazi kubwa sana katika kuwawakilisha wananchi na wanawazidi wabunnge kwenye utendaji wa kila siku.
Ukiangalia ripoti mbalimbali za utendaji wa wabunge, unaweza kujiridhisha kuwa zaidi ya nusu ya wabunge hawana mchango mkubwa bungeni, wao ni bendera fuata upepo tu na kwa kweli wanasimamia masuala ambayo si lazima wawe wametumwa na wananchi wao.
Wapo wabunge ambao hukaa mwaka mzima, miaka miwili, miaka mitatu au wakati wao wote wa ubunge bila kuzungumza chochote bungeni na wapo wabunge wengi ambao wakishachaguliwa tu hukimbia majimbo na kuishi Dar es Salaam huku wananchi wao wakiteseka kipindi chote.
Katika muktadha wa uwepo wa aina hizi tofauti za wabunge, mwakilishi mwokozi wa wananchi amebakia kuwa diwani. Sote tunaweza kukubaliana kuwa madiwani wamekuwa na mchango mkubwa na wa moja kwa moja kwa wananchi na maendeleo ya wananchi kuliko wabunge.
Wakati mwingine kumbe mchango wa madiwani haukwepeki kulingana na asili ya kazi yao ya uwakilishi. Diwani ni lazima awe mkazi wa kata ambayo anagombea udiwani na mbunge si lazima awe mkazi wa jimbo analowakilisha. Mazingira haya yanamfanya diwani abanwe zaidi, awajibike zaidi na apambane na matatizo ya wananchi wake bila kukwepa.
Hali hiyo pia inasababisha diwani atumie saa nyingi zaidi kushughulikia masuala ya wananchi kuliko mbunge, na tena hali hiyo inamfanya diwani awe karibu na wananchi kuliko mbunge.
Ifahamike kuwa hapa simaanishi kuwa hakuna wabunge wachapakazi kuliko madiwani, wabunge wa aina hiyo wapo lakini ni wa kuhesabu, sehemu kubwa ya wabunge wa majimbo yote Bara na Zanzibar wanawategemea sana madiwani na utendaji wa madiwani ili wachaguliwe tena katika vipindi vinavyofuata.
Itoshe tu kusema kwamba diwani anafanya kazi ya ziada kwenye kata yake na analipwa Sh350,000 na mbunge ambaye anafanyiwa kazi kubwa na diwani kwa ngazi ya kata analipwa mara 34 ya diwani. Hapo ndipo hoja yangu imekaa na inahitaji tafakuri ya taifa zima.
Kwa nini tunamlipa diwani pesa kidogo wakati tuna uhakika yeye ndiye anamwakilisha mwananchi kwa ukaribu zaidi, yeye ndiye analala na kuamka na wananchi kwenye kata, yeye ndiye anazibua mitaro nao kila siku, yeye ndiye anahudhuria misiba yote ya kwenye kata yake n.k.
Maamuzi Kuhusu Maendeleo ya Kata
Kiwadhifa, diwani ndiye mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata. Fedha zote zinazotoka Halmashauri zinakwenda kwenye kamati hii ambayo huamua matumizi yake kulingana na mchanganuo wa maombi yake na makubaliano ya kata na halmashauri juu ya vipaumbele vya kata husika.
Katika ngazi hiyo ya kata kuna tenda nyingi mno ambazo hutolewa kwenda kwa watu mbalimbali kushughulikia masuala ya miundombinu, elimu, afya na mengineyo. Madiwani wanapaswa kufanya maamuzi ya kifedha yenye thamani ya mabilioni ya Kitanzania katika ngazi yao na wao ndiyo wenye dhamana ya usimamizi wa miradi yote kwenye kata na hawa ndiyo watu ambao tunawalipa Sh350,000 kwa mwezi.
Halafu mbunge ambaye hapelekewi moja kwa moja mabilioni ya pesa na kuyasimamia (anafanya hivyo kwa njia zisizo za moja kwa moja kupitia utaratibu wa kuisimamia serikali na kupitisha bajeti ya serikali) lakini uhusika wa diwani kwenye pesa ni wa moja kwa moja kuliko ule wa mbunge kwenye kuisimamia serikali kifedha.
Rushwa, Kutoridhika na Uovu
Katika moja ya hotuba za Rais John Pombe Magufuli wakati akiwa mgombea wa CCM mwaka 2015 (wakati wa kampeni) alisisitiza kuwa wafanyakazi wa serikali wanaingia kwenye ushawishi wa kupokea rushwa kwa sababu mishahara yao ni midogo, nimerudia kuangalia video ya hotuba hiyo ya mgombea wa CCM wa wakati huo na kujiridha pasipo na shaka kuwa kumbe Rais wetu anatambua fika kwamba kumlipa mwanadamu vizuri ni kumuondolea vishawishi na kumfanya asimamie kazi yake kwa weledi, kujitoa na kwa uvumilivu mkubwa zaidi.
Kwa kuzingatia hotuba hiyo hiyo ya Rais, namkumbusha kuwa madiwani wanaingizwa kwenye vishawishi vingi mno kwenye kazi zao na wanajikuta wanapokea rushwa ili kutoa tenda na kusimamia masuala mengi ya maendeleo ya kata zao na sababu kubwa kuliko zote ni malipo kiduchu ya pesa za mwezi wanazopewa.
Hatuwezi kusema kuwa Sh800,000 – 1,000,000 walizoomba ati wakipewa ndiyo hawatachukua rushwa katika ngazi yao ya maamuzi, tunachoweza kusema ni kuwa wakilipwa fedha hizo walau tutaondoa sehemu fulani ya kundi la madiwani ambao wamekuwa wakijihusisha na rushwa na upendeleo kwenye kutoa tenda za miradi ya mabilioni na mamilioni kwa sababu tu ya kutoridhika na posho zao za mwezi.
Kubwa kuliko yote kuwalipa madiwani vizuri ni njia mojawapo ya kuwatia moyo zaidi kuwawakilisha wananchi na kutatua kero zao kupitia serikali za mitaa, ni njia pia ya kuzifanya serikali za mitaa ziwe na nguvu kwa sababu wanaoziunda wana nguvu ya kiuchumi ambayo ni muhimu mno katika kujenga uhuru wa wawakilishi wa wananchi.
Hoja yangu
Lengo la hoja hii ni kuamsha mjadala wa kitaifa juu ya umuhimu wa kuzilipa kada za watumishi wa umma na wawakilishi wa wananchi kwa uwiano unaofanana. Yaani mshahara wa Rais usitofautiane sana na wa mbunge, mshahara wa mbunge usitofautiane sana na wa diwani. Na njia ya kulitatua jambo hili ni aidha kupandisha mishahara ya madiwani na kushusha ya wabunge kidogo au kupandisha mishahara ya madiwani ikaribie ile ya wabunge na kuwafanya madiwani wawajibike zaidi kwa wananchi wa kata zao.
Hoja hii haina maana ya kutetea malipo makubwa kwa wanasiasa, ina maana ya kuikumbusha serikali na taifa letu kwamba madiwani ni watu muhimu kwelikweli katika maisha ya moja kwa moja ya wananchi na kwamba kudharau vipato vyao ni kuwavunja moyo na kuwafanya wajisikie kama wawakilishi nusu wa wananchi.
Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kijamii na Kisiasa, Mtafiti, Mwanasheria na ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi CUF. Simu; +255787536759/ Barua Pepe; juliusmtatiro@yahoo.com/ Tovuti; juliusmtatiro.com.
No comments:
Post a Comment