Tuesday, October 10

Madini,Maliasili bado pasua kichwa

Rais John Magufuli akitangaza mabadiliko katika

Rais John Magufuli akitangaza mabadiliko katika Baraza la Mawaziri, Ikulu jijini Dar es Salaam juzi. Picha na Ikulu 
Dar es Salaam. Wizara za Maliasili na Madini zimeendelea kuwa kinara wa kuondoa mawaziri kwa sababu tofauti baada ya Rais John Magufuli kuamuacha Profesa Jumanne Maghembe katika mabadiliko aliyoyafanya juzi.
Maghembe, ambaye katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu uliopita alikuwa akikosolewa na chama chake cha CCM kuhusu utendaji wake, anaingia katika orodha ya mawaziri walioshika wizara hiyo na baadaye kuondolewa kwa ama kuachwa au kulazimishwa kujiuzulu.
Profesa Maghembe pia anaingia katika orodha ya mawaziri waliowahi kushika Wizara za Maliasili na Utalii pamoja na Nishati na Madini, ambazo zimekuwa chungu kwa wanaozishika, hasa katika kipindi cha takriban miaka 12 ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne na ya Tano.
Katika mabadiliko aliyofanya juzi yaliyotokana na kutenguliwa kwa uteuzi wa Profesa Sospeter Muhongo, aliyekuwa Waziri wa Madini, George Simbachawene (Tamisemi) na Edwin Ngonyani (naibu waziri, Ujenzi), Rais ameongeza wizara mbili, ameacha mawaziri wanne, kupandisha wanne na kuteua 14 wapya, wengi wakiwa ni manaibu.
Wizara ya Nishati na Madini, ambayo imekuwa ikikumbwa na kashfa za mara kwa mara kutokana na mikataba ya umeme na madini, sasa imetenganishwa baada ya ripoti za uchunguzi wa usafirishaji mchanga wa madini nje ya nchi, uendeshaji, usimamizi na udhibiti wa almasi na Tanzanite kubainisha ubovu wa mikataba, udhaifu wa sheria na udhaifu katika uendeshaji biashara ya madini.
Katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Maghembe amedumu tangu ateuliwe na Rais Magufuli mwaka 2016 baada ya aliyemtangulia, Lazaro Nyalandu kuachwa.
Nyalandu, ambaye alikuwa naibu waziri, aliteuliwa kuwa waziri kamili baada ya Balozi Khamis Kagasheki alipolazimika kujiuzulu kutokana na utekelezaji mbovu wa Operesheni Tokomeza iliyolenga kupambana na ujangili baada ya mauaji ya tembo kukithiri.
Wizara hizo mbili ndizo zinashikilia sekta nyeti katika uchumi, utalii na madini zikichuana katika kuliingizia Taifa mapato, huku nishati ikihusika na miradi mikubwa ya umeme ambayo imesababisha nchi kuingia hasara kutokana na mikataba mibovu.
Madini yalichangia asilimia 3.3 ya Pato la Taifa mwaka 2014 na asilimia nne kwa mwaka 2015, wakati kwa mwaka 2014, Maliasili na Utalii iliingiza dola 2 milioni za Marekani ambazo ni asilimia 25 ya fedha za kigeni na asilimia 17 ya Pato la Taifa. Utalii unaajiri takriban watu 600,000.
Lakini sekta hizo ndizo zimekuwa zikikumbwa na kashfa kama ya uingiaji mkataba mbovu wa uzalishaji umeme wa IPTL, Richmond, usafirishaji mchanga wa madini kwenda kuyeyushwa nje, usimamizi mbovu wa dhahabu, almasi na Tanzanite.
Wizara ya Maliasili imekuwa ikikumbwa na kashfa kama za mauaji ya wanyamapori, hasa tembo, utoaji ovyo wa vibali vya kuwindia na vitalu, utoaji holela wa uvunaji magogo na usafirishaji wa wanyama mwitu kwenda nje wakiwa hai.
Dk Hamisi Kigwangalla sasa ataongoza wizara hiyo ya maliasili na utalii, wakati Angellah Kairuki ataongoza Wizara ya Madini na Dk Medard Kalemani ataongoza Nishati.
“Uamuzi wa kutenganisha wizara ya Nishati na Madini unatokana na unyeti wa sekta hizo katika kukuza uchumi wa Taifa na dhamira yake (Rais) ya kusimamia rasilimali hizo kwa maendeleo ya Watanzania,” anasema mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Samuel Msanda, mmoja wa watu waliohojiwa na Mwananchi kuhusu suala hilo.
“Bahati mbaya hatujanufaika na rasilimali za nchi kwa muda mrefu kwa sababu ya mikataba mibaya tuliyosaini. Hata akija mtakatifu, hawezi kusimamia wizara ya nishati na madini chini ya mikataba mibovu tukaona matokeo chanya.”
Mwanazuoni huyo alibainisha kuwa mabadiliko hayo yatakuwa na tija kwa sababu kila mtu sasa anajua dhamira ya Rais Magufuli.
Maoni kama hayo yalitolewa na Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Benson Bana aliyesema yanalenga kuimarisha safu yake ya utendaji kwa kuongeza nguvu.
“Kilikuwa kilio cha muda mrefu kutaka sekta za nishati na madini zisimamiwe na wizara tofauti ili kuongeza ufanisi. Taifa hili lina rasilimali nyingi, kwa hiyo zinahitaji usimamizi wa karibu,” alisema Profesa Bana.
Kuhusu kuachwa kwa mawaziri wawili, Profesa Maghembe, Profesa Bana alisema viongozi hao sasa wamezeeka na hawawezi kuendana na kasi ya Rais Magufuli.
Hata hivyo, mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu alikuwa na mtazamo tofauti, alisema Serikali inarudi kulekule kwa kuwa na wizara nyingi ambazo zinaongeza gharama za uendeshaji.
Profesa Baregu pia alikosoa uteuzi wa Dk Kalemani akidai kwamba amekuwa kwenye wizara hiyo kwa muda mrefu wakati maovu mengi yakitendeka.
Lakini Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu) aliupokea vizuri uamuzi wa kutenganisha sekta hizo, akisema Serikali ndiyo iliyokuwa ikikosea.
“Serikali yenyewe ndiyo ilifanya makosa makubwa kwa kukubali kupewa masharti ya jinsi gani uchimbaji wa madini ufanyike,” alisema.
“Serikali ilikuwa haina hisa hata moja kwenye kampuni za madini, wageni walimiliki kwa asilimia 100.”
Hata hivyo, mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa alikosoa hatua ya Rais Magufuli kuongeza wizara kwa madai kwamba anajichanganya mwenyewe kwa kurudia kitu ambacho alisema hatakifanya.
Msigwa alisema haoni tija yoyote kwenye mabadiliko hayo ya mawaziri kwa sababu hayajazingatia weledi. Akitoa mfano wa Dk Kigwangalla ambaye ni daktari wa utabibu, kupelekwa Maliasili na Utalii akisema ni matumizi mabaya ya rasilimali.
“Kabla hujabomoa ukuta jiulize kwanza kwa nini wenzio waliujenga. Yeye anabomoa ukuta tu, ni ninavyoona huko mbeleni tutakuwa na wizara nyingi zaidi kuliko hizi,” alisema Msigwa ambaye pia ni kamishna wa Bunge.

No comments:

Post a Comment