Kanali Lubinga anatoa kauli hiyo wakati wa mahojiano na mwandishi wa gazeti hili yaliyofanyika hivi karibuni ofisini kwake katika Ofisi ndogo za Makao Makuu ya CCM, barabara ya Lumumba jijini Dar es Salaam, kuhusu utendaji wa Serikali na madai ya kuingiliwa utendaji wa mihimili mingine ya dola kama Bunge na Mahakama.
Anasema kwa muda mrefu mihimili mingine ilikuwa ikifanya kazi kwa mazoea jambo ambalo lilikwamisha kasi ya uwajibikanji.
Kanali Lubinga anasema Rais wa awamu ya nne alijitahidi kuongeza idadi ya majaji, lakini kazi ya umalizaji wa kesi haikuendana na idadi hiyo.
“Mahakama zilikuwa hazitimizi wajibu wake. Watu wamekuwa ovyo, leo hii hata watu waliofanya kazi bila vyeti wanataka walipwe unajiuliza walipwe wamefanya nini?” anahoji Kanali Lubinga ambaye kabla ya uteuzi wake alikuwa msemaji wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
Anasema hata kwa upande wa Bunge siyo kweli kwamba Serikali imekuwa ikitia mkono baadhi ya maamuzi bali kinachotokea ni baadhi ya wabunge hawaheshimu kanuni na sheria zilizopo na pindi wanapoadhibiwa hufikiri vyinginevyo.
“Bunge lina taratibu zake, uki-misbehave utachukuliwa hatua ikiwamo kutolewa nje. Sasa kuna watu wanafikiri pale ni sehemu ya kucheza, hapana hatuwezi kwenda hivyo,” anasisitiza Kanali Lubinga.
Katiba mpya siyo kipaumbele
Akizungumzia mchakato wa Katiba mpya ambao kwa kipindi kirefu umekwama, Kanali Lubinga anasema kwa sasa chama chake kinaangalia matatizo ya msingi ya wananchi wake na kwamba suala la Katiba siyo kipaumbele chao.
Anasema Kwa sasa chama chake kinataka Serikali yake itekeleze matakwa ya wananchi na kushughulikia matatizo ya msingi ya Watanzania na siyo Katiba mpya.
Kauli hiyo ya Kanali Lubinga inafanana na ile iliyowahi kutolewa na mwenyekiti wa chama hicho Taifa na Rais John Magufuli ambaye alisema kuwa kwa sasa Serikali yake haioni sababu ya kuendelea na mchakato wa Katiba mpya kwa kuwa siyo kipaumbele chake.
Rais Magufuli alinukuliwa akisema kuwa kwa sasa Serikali yake ina mambo mengi ya kutekeleza kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi wake na kwamba suala la Katiba lisubiri.
Kanali Lubinga anasema CCM sasa inatimiza wajibu kulingana na ilani yake iliyoinadi kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na kuhakikisha inatimiza ahadi zake kwa Watanzania.
Zanzibar hakuna mgogoro
Kanali Lubinga anasema kilichotokea Zanzibar ni suala la mtazamo na kwamba hakuna tatizo la msingi.
“Hakuna tatizo la msingi, matatizo ya Zanzibar ndiyo harakati za kisiasa za kuchukua madaraka. Ni yale yale yaliyopo Uingereza lakini pia yaliyoikumba Marekani katika kipindi cha uchaguzi mkuu wake mwaka huu.”
Kanali Lubinga anasema kuwa Tanzania ina mapungufu lakini huwezi kuyaita matatizo kama ilivyo kwa nchi nyingine na kwamba mapungufu hayo yameshapatiwa utatuzi.
Akizungumzia mikataba mbalimbali ambayo hivi karibuni Serikali iliivunja, Kanali Lubinga anasema gharama ya kuvunja kitu chochote kilichozoleka mara nyingi inaweza kuzua sintofahamu.
Kanali Lubinga anasema unapofanya mabadiliko mara nyingi huleta shida kutokana na fikra za watu kuamini kilichopo, lakini baada ya matokeo watu hukubaliana nayo.
“Watu wakubali mabadiliko. Kila mmoja anajua kuna baadhi ya mikataba imeingiwa kwa manufaa ya ama kikudi au mtu fulani, je, kuna anayeridhika na hali hiyo ya mikataba? Anahoji Kanali Lubinga.
Pia, Kanali Lubinga anasema mambo ambayo anatamani uongozi wa Rais Magufuli uyafanye ni pamoja na kuandaa vijana ili wame viongozi wa baadaye.
“Ni lazima tuwaandae vijana, tusiwe one man show. Tangu enzi za baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere chama chetu kilikuwa na utaratibu wa kuandaa vijana ili waje kushika atamu, lakini kwa muda mrefu tulijisahau sasa ni muda muafaka wa kurudi nyuma na kulitekeleza hili.”
Anasema kuwa kwa kuzingatia hilo, tayari chama chake Oktoba 15, mwaka huu kitaweka jiwe la msingi katika ujenzi wa chuo kwa ajili ya kuandaa viongozi hao kitakachojengwa Ihemi, Iringa.
Anasema jambo la pili ni kusimamia Serikali lakini pia kuachana na waovu; “Ni lazima Serikali ijitenge na watu waovu ili iweze kuaminika kwa wananchi wake,”anasisitiza Kanali Lubinga ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Mkoa wa Katavi.
“Ukiwatendea watu maovu malipo ni hapa hapa, hata kama hutayapata wewe moja kwa moja ipo siku kizazi chako kitapata matatizo kwa sababu yako,” anasisitiza kanali Lubinga.
Jeshi limenijenga
Kanali Lubinga anasema kuwa haoni tofauti ya kufanya kazi jeshini na sasa alipo katika siasa kwa kuwa jeshi limemjengea nidhamu ya hali ya juu.
“Kilichobadilika ni kubadili kikosi kimoja kwenda kingine, naweza kusema kuwa awali nilikuwa katika kikosi cha mizinga lakini sasa nipo katika kikosi cha kutembea kwa miguu, tofauti ni ndogo sana kwa kuwa huku kuna nidhamu ya kiraia lakini pia jeshini tulikuwa tukisisitiziwa nidhamu.”
Mimi ni mwanasiasa wa siku nyingi
Kanali Lubinga anasema ili uwe mwanajeshi awali ilikuwa ni lazima uwe mwanachama wa chama cha siasa mpaka pale Tanzania ilipoingia katika mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 iliwalazimu kurudisha kadi hizo na kuzikabidhi.
“Mara baada ya kustaafu kitu cha kwanza kabla ya kubeba sanduku langu nilifuata kadi yangu ili niendeleze mapenzi yangu niliyokuwa nayo kutokana jeshini kutopata fursa hiyo.”
Alipoulizwa iwapo baada ya kustaafu angefuatwa na vyama vya upinzani na kumuomba ajiunge na chama chao asingekuwa tayari kwa kuwa hakuana na mapenzi na vyama hivyo.
Awashauri CUF
Katibu huyo alikishangaa Chama cha Wananchi (CUF) kwa kushindwa kumaliza mgogoro wake na badala yake wamekuwa wakikitupia lawama chama hicho.
Lubinga anasema anakishangaa chama hicho kwa kumrejesha mtu ambaye alikimbia vita na kuruhusu kurudi tena katika chama hicho.
“Hakuna kiongozi wa kweli, wapo pale kwa ajili ya matakwa yao.. Hata mimi nawashangaa mtu anakimbia vita mnamrudidha mnategemea nini? Alihoji Kanali Lubinga bila ya kutaja jina la mtu huyo.
Kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa CUF, kipo kwenye mgogoro mkubwa wa kiutawala uliosababishwa na kurudi kwa profesa Ibrahimu Lipumba kwenye uenyekiti wa chama hicho.
Mgogoro huo baina ya makundi mawili ya wanachama yanayoongozwa na viongozi wa CUF. Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wa chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad baada ya Profesa Lipumba kutangaza kurudi katika nafasi yake ndani ya chama hicho miezi michache baada ya kuandika barua ya kujihuzuru nafasi hiyo.
Lakini Kanali Lubinga alikwenda mbali zaidi na kukusimfu aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema Dk Willbroad Slaa na kusema ni ameonyesha ushujaa mkubwa.
“Dk Slaa ni real man alisimamia msimamo wake, mwanaume wa kweli habadiliki, anageka akiwa kitandani pekee lakini siyo hawa wengine kila siku wanabadilika,”anasisitiza Kanali Lubinga ambaye kabla ya uteuzi wake alikuwa msemaji wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
Hata hivyo, Kanali Lubinga anasema chama chake hakihusiki na mgogoro wa CUF na kwamba hawana haja ya kutafuta mchawi na badala yake wanatakiwa kukiimarisha.
No comments:
Post a Comment