Thursday, October 5

Juhudi zisizozaa matunda kumtafuta Ben Saanane


Dar es Salaam. Tangu kada wa Chadema Ben Saanane atoweke katika mazingira yasiyoelezeka Novemba 14 mwaka jana, kumekuwa na juhudi tofauti zinazofanywa na chama hicho, familia yake kwa upande mmoja, na vyombo vya dola kwa upande mwingine.
Hata hivyo, juhudi zote hizi ambazo zimehusisha pia mataifa ya nje hazijatoa chembe ya dokezo ni katika mazingira gani mwanasiasa huyo kijana alipotea, yuko wapi, hai ama amekufa.
Taarifa za kutoonekana Saanane zilikifikia chama chake siku tatu tu baada ya kuonekana makao makuu ya Chadema kwa mara ya mwisho Novemba 14 alikoenda kufanya shughuli za kichama.
Hisia ya kwanza iliwaaminisha viongozi wa Chadema na familia yake kwamba inawekekana Ben alikuwa amekwenda Afrika Kusini kutetea tasnifu (thesis) yake ya Shahada ya Uzamivu (PHD) jijini Johannesburg, Afrika Kusini. Hii ni kutokana na ukweli kuwa alishatoa taarifa angesafiri kwenda huko.
Katika hatua ya kwanza, familia ya Ben na viongozi wa Chadema waliripoti suala hilo kituo cha polisi cha Tabata.
Timu ya kumsaka Ben ilikwenda pia ofisi za uhamiaji kujaribu kujua kama katika taarifa zao kuna Mtanzania mwenye jina la Ben Saanane amevuka mipaka na kwenda nje ya nchi.
“Ni kweli tulihakikishiwa Ben hajasafiri kwenda nje ya nchi. Alikuwa bado ndani ya mipaka yetu na systems (mifumo) ya uhamiaji ilituthibitishia hivyo,” anasema John Mrema, mkurugenzi wa uenezi, mawasiliano na mambno ya nje wa Chadema ambaye amekuwa akihusika kwa karibu na juhudi za kumsaka Ben.
Hata hiyo, familia na wanachadema hawakutaka kuishia hapo na waliamua kutuma timu iliyosafiri hadi Afrika Kusini, ambako walitaarifiwa na kujiridhisha kwamba Ben hakuwa amekwenda huko.
Hali hiyo iliwafanya baadhi ya ndugu, kwa kushirikiana na asasi ya vijana inayoitwa Umoja wa Kizazi cha Kuhoji Tanzania (The Union of Thinking Generation (UTG)), ambayo Ben alikuwa katibu wake, walianza kuzunguka katika hospitali zote na vituo vya afya jijini Dar es Salaam wakimsaka Ben.
Timu hiyo iliingia kila chumba cha kuhifadhia maiti na kwenda wodi kwa wodi kuona kama mwili wa Ben unaweza kupatikana. Kazi hiyo ilimalizika bila mafanikio.
Baada ya kujiridhisha kuwa Ben hakuwa amefariki wala kwenda nje ya nchi, timu ya ufuatiliaji ilibisha hodi makao makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
“Kwa sababu Ben alikuwa na simu, tuliamua kwenda TCRA watusaidie kujua aliwasiliana na nani mara ya mwisho na location (eneo) gani anaweza kuwapo. TCRA waliahidi kufanya kazi hiyo kama polisi wangetoa kibali. Tangu wakati huo hadi leo polisi na TCRA wanarushiana mpira tu,” anasema Mrema.
Baada ya kuhisi kile wanachoamini kuwa ni ‘mizengwe’ ya mamlaka husika katika suala la kumsaka Ben, Chadema walianza juhudi za ndani na nje ya Bunge kuzilazimisha mamlaka zilipe uzito suala hilo na kufanya uchunguzi makini.
Desemba mwaka jana, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akiongozana na viongozi waandamizi wa chama hicho, akiwemo Tundu Lissu, mbunge wa Singida Mashariki anayetibiwa nchini Kenya baada ya kushambuliwa kwa risasi mwezi uliopita, walifanya ziara ya wiki tatu barani Ulaya wakijaribu, pamoja na mambo mengine, kushawishi jumuiya ya kimataifa ishinikize juhudi za kumsaka Ben.
Ziara hiyo iliwafikisha makao makuu ya Umoja wa Ulaya (EU) jijini Brussels, Ubelgiji ambako walikutana na baadhi ya wabunge wa Bunge la Ulaya.
Walikutana pia na kamati ya Bunge la Ulaya inayohusika na masuala ya haki za binadamu, masuala ya Afrika na pia walikutana na viongozi wa ngazi za juu wa Kamisheni ya Ulaya.
Ziara hiyo pia iliwakutanisha na wabunge wa Bunge la Mabwanyenye (House of Lords) na Bunge la Makabwela (House of Commons) nchini Uingereza na kuongea na wabunge wa vyombo hivyo wanaohusika na masuala ya haki za binadamu.
Katika ziara hiyo, viongozi wa Chadema walifanikiwa pia kukutana na mkuu wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth).
“Waliahidi ku-press government (kuishinikiza Serikali) kwa njia za kidiplomasia kutafuta majibu kuhusu suala la Ben,” anasema Mrema.
Tayari viongozi wa Chadema wamelifikisha suala la Ben Saanane kwa wawakilishi wa balozi mbalimbali nchini ili kuishinikiza Serikali kuongeza nguvu ya kumsaka Ben.
Sakata la kupotea kwa Ben Saanane lilichukua sura mpya mwezi Aprili wakati ofisi ya Kamishna wa Haki za Binadamu ya UN yenye makao yake makuu Geneva, Uswisi iliposema iko tayari kutuma timu ya uchunguzi.
Uamuzi huo ulifikiwa katika mkutano ulioitishwa na ofisi hiyo Kanda ya Afrika uliohusisha nchi za Sudan, Rwanda, Burundi Kenya, Uganda, Ethiopia, Djibouti na Tanzania.
Suala hilo liliibuka baada ya wajumbe wa mkutano huo kuonyesha kuguswa na suala hilo na kutaka kujua undani wake, lakini hakukuwa na taarifa za kina.
Baada ya ujumbe wa Chadema kumaliza ziara ya Ulaya, ulirejea nchini na kuamua kuelekeza nguvu katika kutumia Bunge kushinikiza uchunguzi huo.
Mwezi Aprili, katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu ambacho hufanyika kila Alhamisi, Mbowe aliilamikia Serikali kwa kutolitolea maelezo na kutolipa uzito unaostahili suala la kupotea Ben.
Mbowe alisema ukimya wa Serikali uliwafanya waamini kwamba ama Serikali haitaki au imeshindwa kufanya uchunguzi na kuitaka iruhusu wachunguzi wa nje.
Akijibu rai hiyo ya Mbowe, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema Serikali inalifuatilia kwa karibu suala hilo huku akikitaa ombi la kukaribisha wachunguzi wa nje.
“Nikuhakikishie tu kwamba taifa letu lina uwezo wa ndani wa kufanya ufuatiliaji wa kutambua matukio ya mtu kufariki au kutoweka na kubaini vyanzo na namna ya kudhibiti matukio hayo. Serikali haina kikomo cha uchunguzi kutegemea aina ya tatizo. Muda utategemea vyombo vyetu vinapata msaada na jamii na vyanzo vingine na teknolojia ambayo tunaitumia ili kupata majibu,” alisema Waziri Mkuu.
Wiki chache baadaye, sakata la kutoweka Ben liliibuka kwa nguvu bungeni na kusababisha mvurugano mkubwa kiasi cha Bunge kuzuia suala hilo kujadiliwa kwa maelezo kuwa tayari lilikuwa mikononi mwa vyombo vya upelelezi.
Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Hassan Zungu alilazimika kuzuia kusomwa hotuba ya Waziri Kivuli wa Habari, Joseph Mbilinyi kutokana na kugusia suala la kupotea kwa Ben Saanane.
Hotuba hiyo ilijaa viambatanisho vya maandishi ya Ben Saanane kwenye mitandao ya kijamii kabla ya kupotea kwake.
Baadaye, zuio hilo lilikumba pia hotuba za Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani, Godbless Lema na Lissu.
Kiu ya majibu ya uchunguzi wa kupotea Ben haijakoma takriban mwaka mzima sasa tangu kutoweka kwake.
Mwishoni mwa mwezi Agosti, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Siro alisema katika mahojiano na kituo cha televisheni cha ITV kuwa jeshi hilo limeunda timu ya upelelezi kufuatilia kupotea kwa Ben.
“Kazi yetu kubwa ni kupeleleza. Natoa rai kwa yeyote mwenye taarifa za kutusaidia kupata mwelekeo atupe. Kimsingi tumeunda timu yetu ya watu kadhaa wenye weledi mbali mbali kuhakikisha huyu bwana mdogo anapatikana au tujue amekwenda wapi,” alisema Sirro.
Na wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba amesema Serikali haijui kama Ben Saanane amekufa ama yu hai huku akiahidi Jeshi la Polisi litaendelea kumtafuta ili kujua kilichotokea.
Akiongea katika kipindi cha Clouds 360 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Clauds, Mwigulu alisema: “Ni ngumu kusema kama Ben Saanane yuko hai au amefariki kwa sababu bado hatujui nini kilimpata.”
“Nchemba anasema hawezi kujua kama Ben Saanane amekufa au yuko hai kwa sababu hajui alipo. Hii inazidi kutupa shaka hasa wanapokataa kuleta wachunguzi wa nje wakati wanakiri wameshindwa kupeleleza.
“Tafsiri yetu ya kukataa watu wan je kuja kuwasaidia kutatufa raia wao ni kwamba wanajua alipo,” anasema Mrema.
Kesho tutaona machungu yanayosababishwa na kupotea kwa Ben Saanane

No comments:

Post a Comment