Monday, October 9

IEBC yataka Mahakama ya Juu ifafanue marejeo ya uchaguzi


Majaji wa Mahakama ya Juu Kenya.
Mahakama ya Juu nchini Kenya itatoa maelekezo Jumatatu katika kesi iliyofunguliwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IECB ambayo inataka ufafanuzi ni jinsi gani ikabiliane na mapungufu iwapo yatajitokeza katika uhakiki wa matokeo ya uchaguzi wa marudio.
Vyama vyote vilifahamishwa Ijumaa kuwa vinatakiwa kufika mahakamani Jumatatu ilikupata muongozo vipi masuala ya uchaguzi yatavyokuwa.
Kupitia kwa wakili Kamau Karori, Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati ameitaka mahakama kutoa ufafanuzi tume ifanye nini kukabiliana na makosa yatakayo jitokeza baada ya uhakiki wa fomu za matokeo ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa Karori, kuna mkangamano juu ya uamuzi uliotolewa na mahakama hiyo Septemba 20, kwa sababu majaji walinang’ania kuwa mwenyekiti ni lazima ahakiki matokeo kabla ya kutangaza mshindi wa kinyang’anyiro cha urais.
Amesema ni muhimu kwa mahakama kutoa ufafanuzi iwapo Chebukati na Tume yake wanaweza kusahihisha makosa ya Fomu namba 34B, wakati matokeo yatapokuwa hayalingani na yale yaliyosajiliwa katika Fomu namba 34A.
Walipofikiwa Jumamosi kuulizwa kuhusu suala hilo, wakili wa Muungano wa upinzani wa NASA Jackson Awele amesema kuwa walikuwa wamepokea nyaraka za mahakama Alhamisi na bado hawajawasilisha maelezo yao mahakamani.
“Bado tunalifanyia kazi suala hili,” alisema.
Mahakama ya Juu, kwa uamuzi wa walio wengi, ilibatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais Agosti 8 ikitaja kuwa ulikuwa umegubikwa na dosari nyingi na kukiuka katiba wakati wa kupeperusha matokeo hayo.
Jaji Mkuu David Maraga, Makamu wake Philomena Mwilu, Majaji Smokin Wanjala na Isaac Lenaola walitoa uamuzi kuwa dosari na uvunjifu wa sheria ulikuwa mkubwa kiasi cha kuathiri matokeo.
Majaji Jackton Ojwang’ na Njoki Ndung’u hawakukubaliana na uamuzi huo.

No comments:

Post a Comment