Thursday, October 5

EU yaridhishwa usanifu, ujenzi wa makumbusho ya Olduvai Gorge


Ngorongoro. Jumuiya ya Ulaya (EU) imesema imeridhishwa na usanifu na ujenzi wa makumbusho ya Olduvai Gorge.
Jumuiya hiyo imefadhili mradi huo ili kusaidia kuhifadhi historia ya chimbuko la mwanadamu.
Makumbusho hayo yalizinduliwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan mwanzoni mwa wiki hii. Yanatajwa kuwa ni makumbusho ya kipekee duniani kutokana na kuhifadhi sehemu kubwa ya historia ya chimbuko la binadamu.
Meneja wa miradi wa EU, Alexa Haden amesema EU ambayo imefadhili asilimia 80 ya usanifu na ujenzi wa makumbusho hayo uliogharimu Sh1.7 bilioni imefarijika kuwa sehemu ya mradi huo mkubwa.
Amesema jumuiya itaendelea kufadhili miradi ya utunzaji wa tamaduni, utalii na maendeleo ya jamii katika maeneo mbalimbali nchini.
Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya Tumaini Civil Works, Tumainiel Mbwambo ambao wamejenga majengo hayo, amesema wametumia zana zinazopatikana eneo la Ngorongoro.
Amesema makumbusho hayo yamejengwa mithili ya maboma ya Kimasai kwa kutumia malighafi nyingi zinazopatikana Ngorongoro, hivyo kuwa sehemu ya kivutio kwa watalii.
“Miongoni mwa makubaliano ya ujenzi ilikuwa ni kutumia malighafi zinazopatikana hapahapa na tumetumia, yakiwemo mawe hivyo kuvutia watalii,” amesema.
Amesema kutokana na ujenzi kutekelezwa na kampuni ya wazawa, Serikali imepata kodi ya zaidi ya Sh200 milioni na Watanzania wamepata ajira kuanzia kazi ya michoro hadi ujenzi.
Akizungumzia usanifu wa makumbusho hayo, Profesa Manuel Rodrigo wa Chuo Kikuu cha Madrid nchini Hispania amesema  usanifu wa kumbukumbu zilizowekwa ndani ya eneo la Olduvai utawezesha zidumu kwa zaidi ya miaka 50.
“Kumbukumbu zilizopo katika eneo hili zimehifadhiwa kisasa zaidi na zitadumu kwa zaidi ya miaka 50 kutokana na usanifu bora uliofanyika,” amesema.
Mhandisi Joshua Mwankunda, meneja wa idara ya urithi wa utamaduni katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) amesema usanifu na ujenzi wa makumbusho hayo unatarajiwa kuwa kivutio cha utalii.
Mwankunda amesema NCAA imejipanga kutangaza makumbusho hayo ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha katika kipindi kifupi gharama za usanifu na ujenzi wa makumbusho hayo zinarudi, hivyo kuongeza mapato ya Serikali.

No comments:

Post a Comment