Tuesday, October 3

Bodi ya mishahara yapewa vigezo 10 vya utendaji kazi

Waziri wa Nchi Ofisi ya RaisĀ  Menejimenti ya

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais  Menejimenti ya umma na utawala bora Angela Kairuki akizungumza Leo jijinj Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa bodi ya pili ya mishahara ya maslahi kwa utumishi wa umma. 
Dar es Salaam. Serikali imetoa vigezo 10 vya utendaji kwa bodi ya mishahara na masilahi katika utumishi wa umma (PSRB), inavyotakiwa kuvizingatia katika utekelezaji wa majukumu yake.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa bodi ya pili inayoundwa na watu saba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki amesema katika kutekeleza majukumu yake, bodi hiyo ni muhimu kuvizingatia vigezo hivyo.
Kairuki amesema licha ya vigezo kuwa vingi, ni muhimu kuzingatia malipo ya mshahara na masilahi kwa watumishi wa umma yanapatikana na kuwa endelevu.
Vigezo vingine ni utumishi wa umma kuvutia na kubakiza taaluma zinazohitajika katika kuendesha shughuli zake; utendaji wenye tija unatambuliwa; uwazi, usawa na haki zinazingatiwa.
Pia, kuhakikisha malipo yanayostahili, yanayolipika na endelevu yanatolewa kwa ngazi zote katika utumishi wa umma ili kuvutia na kubakiza vipaji maalumu nchini.
Kairuki amesema vigezo vingine ni matakwa ya mlipa kodi na umma kwa jumla yanapewa kipaumbele dhidi ya masuala mengine wakati wa kubuni na kuendesha vyombo vya masilahi.
Vigezo vingine amesema ni kuepuka upendeleo katika kupanga masilahi kwenye utumishi wa umma na aina yoyote ya ushawishi wa kisiasa katika uamuzi unaohusu mishahara na masilahi.
“Uamuzi au ushauri kuhusu mishahara na masilahi uzingatie hali ya soko la ndani na kikanda, pia viwango vya malipo kisekta visitofautiane sana isipokuwa kwa kuruhusu tofauti kutegemeana na aina ya kazi na majukumu,” amesema Kairuki.
Amesema sekta ya utumishi wa umma ina changamoto nyingi mojawapo ikiwa ni kuboresha masilahi ya watumishi ili kuongeza tija katika utendaji kazi.
“Ni dhahiri Serikali haiwezi kufanya uamuzi sahihi bila ushauri wa kitaalamu unaotokana na utafiti kuhusu kuboresha masilahi ya watumishi wa umma na hiyo ndiyo kazi yenu,” amesema.
Wajumbe wa bodi hiyo ni Mwenyekiti Donald Ndagula, ambaye ni Kamishna wa Uhamiaji mstaafu na makamu wake ni Balozi Charles Mutalemwa ambaye ni katibu mkuu mstaafu.
Wajumbe wa bodi hiyo ni George Mlawa ambaye ni Katibu wa Bunge mstaafu; Gaudentia Kabaka, waziri mstaafu; Jaji mstaafu Regina Rweyemamu; Meja Jenerali mstaafu Zawadi Madawili na Kamishna Mwandamizi wa Polisi mstaafu Jamal Rwambow.

No comments:

Post a Comment