Mbelwa alisema hayo alipoulizwa na Mwananchi, mambo mazuri ambayo Tanzania inaweza kujifunza kutoka China licha ya tofauti ndogo za kisiasa zilizopo baina ya mataifa haya mawili.
Kwenye majibu yake, Mbelwa alisema mfumo wa siasa za China, zamani ulikuwapo nchini ambapo chama tawala (CCM) kilishika hatamu za uongozi kabla ya mfumo wa vyama vingi haujaruhusiwa japo wananchi wengi walipenda kuwapo na chama kimoja.
Akitambua mema na changamoto za mifumo tofauti ya siasa, balozi huyo alisema, kwa mtazamo wake, yapo mambo ya msingi ambayo ingefaa Tanzania ijifunze kutoka China bila kujali mtindo unaofuatwa.
“Mambo hayo ni pamoja na kuwa na malengo ya pamoja ya kitaifa ambayo kila mtu anayatambua, anayaheshimu, anayazingatia na kuyatekeleza. Nchi inapojiwekea Mpango wa Maendeleo wa Taifa ulioridhiwa na wananchi wote kupitia wawakilishi wao bungeni, basi utekelezaji wake unakuwa hauna mjadala,” alisema.
Alifafanua kwamba, haijalishi katika utekelezaji wake kuna maumivu gani, kwa kuwa wananchi wote wameridhia basi hakuna kuangalia nyuma hadi malengo husika yatakapotimia. Licha ya malengo ya kitaifa, jambo jingine aliloshauri kujifunza kutoka China ni kufanya kazi kwa bidii. Alisema China inaongozwa na moja ya kauli mbiu isemayo ‘maneno matupu, hudhuru Taifa, kufanya kazi kwa bidii huleta neema kwa jamii.”
“Ninaamini hayo mawili wananchi wote tukijifunza na kuyafuata kama Taifa, tutaweza kupiga hatua ya maendeleo,” alisisitiza balozi huyo aliyeanza kuliwakilisha Taifa Bara Asia, Februari 20.
Kwa sasa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) kina mkutano wake wa 19 unaotarajiwa kutoa mwelekeo wa Taifa na kuhakikisha linakuwa na jamii yenye maisha bora.
China inatambua kwamba mafanikio yake hayawezi kuwa endelevu (sustainable) pasipo kuwepo dunia yenye uchumi tulivu, amani na usalama. Kwenye mkutano huo CPC itatoa mwelekeo wa kukuza ushirikiano wa kimataifa na kuendeleza utandawazi.
“Tanzania inayo nafasi nzuri ya kunufaika na fursa za biashara, uwekezaji, mikopo na misaada kutoka China katika kipindi cha miaka mitatu ijayo,” alisema.
Fursa
Ukiacha mambo hayo mawili, alisema Watanzania mmoja mmoja wanaweza kunufaika na fursa za kijasiriamali zilizopo nchini China kutokana na ushirikiano wa kiuchumi unaendelea kuimarishwa baina ya mataifa hayo.
Kwa siku za karibuni, mikataba kadhaa za Watanzania kuuza bidhaa zao nchini humo imesainiwa kati ya Tanzania na China na balozi huyo anasema kuna fursa nyingi za kuwanufaisha wananchi watakaozichangamkia.
Anasema kati ya Februari hadi Oktoba, mataifa haya yamesaini mkataba wa kuruhusu bidhaa za muhogo mkavu kutoka Tanzania kuingia katika soko la China ambayo ni fursa kubwa inayoweza kuwaondoa wananchi wengi hususan wa vijijini kutoka kwenye umasikini.
Mihogo ni muhimu nchini humo baada ya kufanya mabadiliko ya sera zake. Alisema Septemba 3, Tume ya Mipango ya China ilipitisha azimio la kupunguza matumizi ya nishati ya petroli na makaa ya mawe na kujielekeza kwenye nishati mbadala ifikapo mwaka 2020.
Mabadiliko hayo yanaongeza mahitaji ya muhogo kwa ajili ya chakula na nishati na katika mpango wa kuhakikisha mkakati huo unatekelezwa kwa wakati Serikali ya China inayo kampuni inayonunua bidhaa hizo kutoka nje ya nchi na kuelimisha jumuiya za wafanyabiashara juu ya mahitaji ya muhogo.
Wajumbe wa kampuni hiyo wameshakutana na jumuiya ya wafanyabiashara nchini na kueleza malengo yao ili kufanikisha utekelezaji wa mkataba huo. Kampuni hiyo ilielezea kwa kuanzia, wakati wowote kuanzia sasa, ipo tayari kununua tani 300,000 za muhogo mkavu.
“Hii ni fursa ambayo wajasiriamali hawana budi kuichangamkia. Aidha, siku za karibuni kumekuwa na ongezeko la mahitaji ya bidhaa nyinginezo za kilimo kama ufuta na korosho,” alisema.
Kuvutia uwekezaji
Rais John Magufuli mara kadhaa amekuwa akisisitiza diplomasia ya kiuchumi na kuwataka mabalozi wa Tanzania kulitangaza Taifa na kuvutia wawekezaji. Mbelwa anasema kama ilivyo kwingineko, naye amekuwa akitafuta fursa za uchumi kwa manufaa ya Taifa.
Kwa kuzingatia Mpango wa Taifa wa Maendeleo mwaka 2016/2020 wa kujenga uchumi wa viwanda, anasema ubalozi unavutia uwekezaji kutoka China. Kati ya Februari hadi Oktoba, anasema ubalozi umeandaa ziara sita za wawekezaji kuja Tanzania huku ukishiriki kwenye mikutano 10 ya kuvutia uwekezaji.
Ubalozi umefanikiwa kuzikutanisha taasisi za fedha za Tanzania na mfuko maalum wa China kuwawezesha wajasiriamali wa Afrika kupata mtaji uliotengewa Dola 10 bilioni za Marekani (zaidi ya Sh22 trilioni). Fedha hizo zinakopeshwa benki za Afrika ili kuwakopesha wajasiriamali.
“Tayari Benki ya Maendeleo ya Kilimo na Exim zimekutana na mfuko huo kuangalia namna wanavyoweza kupata fedha. Jambo la msingi ni kwamba mikopo hiyo itatolewa kwa riba nafuu,” alisema.
Kwenye utalii, alisema wanashirikiana na wadau wa sekta hiyo kutangaza vivutio vilivyopo nchini. Katika utekelezaji wa hili, alisema ubalozi umeshiriki kwenye maonyesho matano ya utalii nchini China kati ya Februari na Oktoba na umeanza mazungumzo na taasisi inayoendesha mitandao ya kijamii China, Tencent ili kutangaza vivutio hivyo mubashara.
“Mamlaka za Usafiri wa Anga nchini imeanza mazungumzo ya kuweka mazingira ya ndege kuanzisha safari za moja kwa moja kutoka China hadi Tanzania na kinyume chake,” alisema.
Mafanikio
Licha ya fursa ya Tanzania kuuza muhogo mkavu China na kutangaza vivutio vya utalii kiasi cha kufanikisha kuileta timu ya wacheza filamu wa China kutembelea Tanzania ubalozi umefanikisha mkutano wa jukwaa la biashara kati ya China na Tanzania uliohudhuriwa na wafanyabiashara wapatao 400.
“Lakini huo ni mchakato tu, nitafurahi nitakapoona watalii kutoka China wanaongezeka kutoka 30,000 hadi 100,000 ndani ya miaka mitano ijayo na kuchangia ajira na kuongeza mapato ya fedha za kigeni,” alisema.
Ndani ya muda huo, Mbelwa alisema amefanikisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kuanzisha ushirikiano na vyuo vikuu vitatu vya China utakaowezesha waalimu wake kupata ufadhili wa masomo ya juu kabla hakijaanzisha programu za pamoja za uhandisi wa reli na nyinginezo.
Vilevile, ameishawishi Kampuni ya Ukaguzi ya Mizigo ya China (CCIC) kuijengea uwezo Shirika la Viwango nchini (TBS) kukagua ubora wa bidhaa kutoka nchini humo na kwingineko zikiwamo za ndani.
“Jambo pekee ninaloweza kujivunia ni kuwashawishi wafanyabiashara wa Kitanzania wanaoishi China kuungana na kuunda jumuiya yao. Nilipokutana nao Machi niliwapa pendekezo. Ninafurahi wameanzisha na matunda yake yameanza kuonekana,” alisema.
No comments:
Post a Comment