Tuesday, October 10

ASKARI WALIOKAMATWA KWA RUSHWA KUANZA KUJITETEA

ASKARI watatu wa Jeshi la Polisi wanaokabiliwa na mashtaka matano ya kuomba na kupokea rushwa, wanatarajia kuanza kujitetea Oktoba 17, mwaka huu baada ya kusomewa hoja za awali.
Hatua hiyo ilifikiwa mwishoni mwa wiki katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, baada ya upande wa mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwasomea hoja za awali washtakiwa.
Washtakiwa hao  ni askari PF. 20078  Mathias Nkayaga (31) ambaye ni Mkaguzi Msaidizi wa Polisi na mkazi wa Mbezi Mwisho, F. 919  D/ Sajenti  Philbert Nemes (39) mkazi wa Kambi ya Polisi Kurasini na  F. 3539 Koplo Emmanuel Ndosi ( 37) mkazi wa Survey Mlalakuwa.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Takukuru, Devotha Mihayo, uliwasomea hoja za awali washtakiwa wote watatu.
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Ritha Tarimo, aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 17, mwaka huu kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya washtakiwa hao kuanza kujitetea  baada ya kusomewa hoja za awali na upande wa mashtaka.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa kwa pamoja walitenda kosa hilo Februari  27, mwaka huu  katika Kituo cha Polisi  Oysterbay, Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam.
Wakili Mihayo alidaiwa kuwa siku ya tukio, washtakiwa waliomba rushwa ya Sh milioni 25 kutoka kwa mfanyabiashara, Juhudi Kyando, kama kishawishi cha kuzuia uchunguzi kuhusu tuhuma za kusafirisha meno ya tembo.
Katika shtaka la pili, ilidaiwa katika Kituo cha Mabasi cha Fire (Faya)   Wilaya ya Ilala, washtakiwa walipokea Sh milioni nane kama sehemu ya malipo ya Sh milioni 25 walizoomba kwa mlalamikaji.
Katika shtaka la tatu, katika Benki ya CRDB tawi la Lumumba  Dar es Salaam,  washtakiwa walijipatia Sh milioni 10  kama sehemu ya malipo ya Sh milioni 25 walizomuomba mlalamikaji huku shtaka la nne ni kujipatia Sh milioni saba.
Wakili huyo alidai  katika shtaka la tano, Februari 28, mwaka huu katika eneo la Tabata Bima, washtakiwa hao walijipatia Sh milioni moja kutoka kwa Kyando  kama sehemu ya malipo ya Sh milioni 25 walizoomba.

No comments:

Post a Comment