Afisa mkuu mtendaji wa tume ya uchaguzi nchini Kenya Ezra Chiloba anatarajiwa kuchukuwa likizo ya wiki tatu na hatoshiriki katika uchaguzi wa marejeo wa Alhamisi kulingana na gazeti la Daily Nation nchini Kenya.
Kulingana na duru katika tume hiyo ya IEBC bwana Chiloba alifanya uamuzi huo wa kibinafsi wa kutoshiriki ili kujenga upya imani ya washikadau ambao wamelalamika kuhusu maafisa wa tume hiyo.
Kulingana na gazeti hilo afisa huyo amekuwa chini ya shinikizo kubwa kutoka muungano wa upinzani Nasa kujiuzulu, huku mgombea wa urais wa muungano huo Raila Odinga akiitisha maandamano ya kumlazimisha kuondoka pamoja na maafisa wengine ikiwatuhumu kwa kusimamia vibaya uchaguzi wa Agosti 8 ambapo rais Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi.
Matokeo ya uchaguzi huo hatahivyo yalifutiliwa mbali na mahakama ya juu ambayo iliamua kwamba haukufanyika kulingana na sheria.
Kulingana na Daily Nation Bwana Chiloba anachukua likizo baada ya mwenyekiti wa tume hiyo wafula Chebukati kutaka maafisa waliotajwa baada ya uchaguzi huo kufutiliwa mbali kung'atuka.
Mahakama ya juu ilisema kuwa haikupata ushahidi kuhusu makosa yaliofanywa na maafisa lakini wanasiasa wamelalamika na kuishutumu tume hiyo kwa kujaribu kufanya udanganyifu katika uchaguzi huo mbali na wizi wa kura.
Uamuzi huo wa kuchukua likizo ulijadiliwa na mwenyekiti na bwana Chiloba anaamini kwamba kutokuwepo kwake hakutaathiri maandalizi ya tume hiyo kusimamia uchaguzi ulio huru na haki .
No comments:
Post a Comment