Friday, October 13

Afariki dunia mgodini

KAMANDA WA POLISI MKOA WA GEITA, MPONJOLI LODSON.

MCHIMBAJI mmoja amefariki dunia na mwingine kunusurika baada ya kufukiwa na kifusi cha udongo katika mgodi wa dhahabu usio rasmi wa Bingwa, katika kijiji cha Rwamgasa wilaya na mkoa wa Geita usiku wa kuamkia jana.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Lodson, alisema jana kuwa aliyefariki ni Fikiri Paulo (27), mkazi wa kijiji cha Mlanda wilayani Chato ambaye mwili wake ulitolewa shimoni akiwa ameshaaga dunia.

Mwili huo ulitolewa shimoni na wachimbaji wadogo, kwa mujibu wa mkurugenzi wa mgodi wa Bingwa, Hussein Nyanzala.

Nyazala alisema walikesha wakiendesha zoezi la kuufukua mwili wa marehemu kuanzia saa 5:00 usiku ajali ilipotokea hadi saa moja asubuhi ya jana.

Kamanda Mponjoli alimtaja manusura wa ajali hiyo kuwa ni Musa Evarist (19), mkazi wa kijiji cha Mpomvu.

Alisema Evarist aliokolewa muda mfupi baada ya kufukiwa na kifusi wakati wakichimba mwamba.

Chanzo cha ajali hiyo kinadaiwa kuwa ni kukatika kwa gema la udogo wa mwamba wa mawe katika shimo walimokuwa wakichimba vijana hao.

Baada ya gema kukatika, imeelezwa, kifusi kulifukia wachimbaji hao.

No comments:

Post a Comment