Monday, September 11

Waziri Kairuki aagiza watumishi 10 kusimamishwa kazi


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki ameagiza kusimamishwa kazi watumishi zaidi ya kumi wa halmashauri za wilaya za Gairo na Kilosa.
Uamuzi huo unatokana na kulipwa mshahara hewa kwa aliyekuwa mwalimu wa Shule ya Sekondari Dumila ambaye hayupo kazini tangu mwaka 2009.
Kairuki ametoa agizo hilo alipozungumza na wakuu wa idara katika halmashauri hizo. Amesema ni kosa lisilovumilika mtumishi hayupo kazini tangu 2009 lakini ameendelea kulipwa hadi Agosti.
"Kuanzia leo naagiza waliokua maofisa utumishi, waweka hazina na maofisa elimu sekondari wa halmashauri hizi tangu 2009 watafutwe popote walipo na wasimamishwe kazi kupisha uchunguzi dhidi yao," amesema.
Waziri Kairuki ameagiza vyombo vya usalama kumtafuta mwalimu huyo popote alipo ili kurejesha fedha na afikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Awali, ilidaiwa mwalimu huyo aliaga kwenda masomoni katika Chuo cha St. John lakini hakuripoti chuoni.

No comments:

Post a Comment