Wednesday, September 27

Watoto watekwa na kutumikishwa, polisi yawaokoa

Polisi mkoani Geita inawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kuwateka watoto na kuwatumikisha kwenye shughuli za ufugaji.
Wanaoshikiliwa wametajwa kuwa ni Edward Lukanya (35) mkazi wa mjini Geita na Karume Kalamu (53) mkazi wa wilayani Nyang'hwale.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Mponjoli Mwabulambo amesema kukamatwa kwa watu hao kumetokana na taarifa iliyotolewa na mtoto mwenye miaka 13 (jina linahifadhiwa) aliyepotea tangu mwaka 2013 ambaye alirejea nyumbani mwanzoni mwa mwezi huu na kueleza maisha aliyokuwa akiishi porini.
Kamanda Mwabulambo amesema tayari polisi imewaokoa watoto wengine wanne waliokuwa wakitumikishwa.
Amesema wanaendelea kuwatafuta watoto wengine zaidi ya 10 wanaodaiwa kuwa kwenye misitu wilayani Geita wakichunga mifugo.
Mtoto huyo akizungumza na gazeti hili amesema mwaka 2013 akiwa njiani kwenda msikitini alisimamishwa na mtuhumiwa Edward aliyemtaka apande baiskeli na aliondoka naye.
Amesema mtuhumiwa alimpeleka kwa mzee Kalamu ili alipwe kazi kwa ujira wa Sh20,000.
Watoto hao inadaiwa huchukuliwa katika mazingira yasiyoeleweka, ambapo mtoto mwingine mwenye miaka 16 aliyeokolewa na polisi amesema hajui alitokaje nyumbani.
Mtoto huyo amesema hakumbuki mwaka aliotoka nyumbani kwao.
Amesema siku ya tukio alikwenda kununua dagaa na akiwa njiani ulivuma upepo mkali na baadaye alijikuta eneo la Kasamwa.
Mtoto huyo amesema alichukuliwa na mwanamume ambaye hakumtambua aliyempeleka kwa mzee Kalamu kuchunga mifugo.

No comments:

Post a Comment