Tuesday, September 12

Tucta yahofia uzalishaji kupungua




Katibu Mkuu wa Tucta, Dk Yahya Msigwa
Katibu Mkuu wa Tucta, Dk Yahya Msigwa 


Dar es Salaam. Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) limelaani vitendo vya utekaji wa watoto, mauaji na kushambuliwa kwa risasi Mbuge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Tucta imesema vitendo hivyo vinaweza kusababisha uzalishaji nchini kupungua na wawekezaji kusita kuwekeza.
Katibu Mkuu wa Tucta, Dk Yahya Msigwa amesema leo Jumanne kuwa matukio ya utekaji wa raia, watoto wadogo na mauaji yamewashtua Watanzania.
Amesema Tanzania imezoeleka kuwa ni kisiwa cha amani, yenye watu wanaotofautiana kwa hoja na fikra na imejijengea utamaduni wa kupinga bila kupigana.
"Watanzania hawakuzoea vitendo vya kihuni kama kumpiga mtu risasi mchana kweupe, matendo haya tulikuwa tunayasikia kwenye nchi nyingine na hasa zenye vita ya wenyewe kwa wenyewe au vikundi vya ugaidi," amesema Dk Msigwa.
Amesema yasipokemewa na kulaaniwa matendo ya aina hiyo yatachafua taswira nzuri iliyojengeka kwenye uso wa kimataifa.
Naibu Katibu wa Tucta, Jones Majura amesema kama nchi haina amani ushalishaji utapungua na wawekezaji watasita kuwekeza kwa kuhofia amani ya nchi.
Amesema Tucta ipo pamoja na Serikali katika kuhakikisha uovu unakomeshwa.
"Tunavipongeza vyombo vya dola kwa kazi nzuri, hata hivyo Serikali ifanye kila jitihada kuwabaini wahalifu na kukomesha uhalifu," amesema Majura.

No comments:

Post a Comment