Mkuruguenzi Mtendaji wa chama hicho Lutgard Kagaruki amesema leo Septemba 19 kwamba kuongezeaka kwa kilimo cha zao hilo kunahatarisha afya za watanzania.
Kagaruki amesema baadhi ya kampuni za tumbaku zimefungua ofisi Tanzania wakati katika nchi nyingine kampuni za aina hiyo zimeshtakiwa kuuza bidhaa za tumbaku ambazo wanajua fika kwamba ni hatari kwa afya.
“Hizi ni bidhaa ambazo kwa makusudi zinachochewa zilete utegemezi kwa haraka zaidi,’’ amesema.
“Kampuni nyingine zimeshitakiwa kwa kuwahonga viongozi ndani ya Africa Mashariki hususan Kenya, wasipitishe sheria madhubuti ya kudhibiti matumizi ya tumbaku. Inasikitisha kuona kampuni kama hizi, zimepokelewa kwa mikono miwili hapa Tanzania,’’ ameongeza Kagaruki
Tanzania iko nyuma ya nchi nyingine za Afrika Mashariki, Afrika na dunia kiujumla katika utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa Kudhibiti Tumbaku (World Health Organisation Framework Convention on Tobacco Control – WHO FCTC).
Mpaka sasa nchi 180, ambazo ni zaidi ya asilimia 90 ya wakazi wote duniani zimeridhia Mkataba huu. Tanzania iliridhia Mkataba huu Aprili 2007, hivyo ina wajibu wa kuutekeleza kikamilifu.
“Nchi ambazo zimetekeleza huu Mkataba kikamilifu, magonjwa yanayosababishwa na tumbaku yamepungua ,’’ amesema.
Magonjwa hayo ni pamoja na saratani, magonjwa ya moyo, kisukari na magonjwa sugu ya kifua – yote yakiwa ni magonjwa yasiyoambukiza.
Kagaruki amesema Tanzania ni nchi pekee ndani ya Afrika Mashariki ambayo haina sheria madhubuti ya kudhibiti matumizi ya tumbaku.
“Isitoshe Zanzibar wanayo Sheria na Kanuni madhubuti za kudhibiti Tumbaku zinazoendana na matakwa ya Mkataba,’’ amesema.
“Tunawaomba viongozi wetu waone na kukubali kuwa tumbaku ni janga la kitaifa na halina faida kwa mkulima wala kwa Taifa, bali faida ni kwa kampuni za tumbaku tu.” amesema
“Hivyo wajiunge na wenzao ndani ya Afrika Mashariki, Afrika na Dunia kwa ujumla, kuongoza mapambano dhidi ya tumbaku, huku wakiwasaidia wakulima kujikita kwenye mazao mbadala na kuwapatia masoko bora na ya uhakika kwa mazao hayo,’’ anasema Kagaruki.
“Inasikitisha sana kuona hata wale wakulima waliobadilika na kulima mazao mbadala, mazao yao kwa sasa hivi yanakosa masoko, huku hamasa zikiendelea kwa nguvu kutaka kuwarudisha kwenye kilimo cha tumbaku,’’ amesema.
“Tuna shaka kama kweli hizi siyo njama za kampuni ya tumbaku. Ukweli ni kwamba, ongezeko la kilimo na biashara ya tumbaku nchini, litasababisha ongezeko la matumizi ya tumbaku na hivyo ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza,’’ ameongeza.
No comments:
Post a Comment