Mwanasiasa wa upinzani Tanzania Tundu Lissu apigwa risasi na watu wasiojulikana
Mwanasiasa wa upinzani nchni Tanzania Tundu Lissu amepigwa risasi na watu wasiojulikana jijini Dodoma, katikati mwa Tanzania.
Mwanasiasa huyo amekimbizwa hospitali ya mkoa wa Dodoma na kupokea huduma ya kwanza na taarifa zinasema kuna mipango ya kumsafirisha hadi Nairobi kwa matibabu zaidi.
Rais wa Tanzania John Magufuli kupitia kwenye Twitter amesema amesikitishwa sana na kushambuliwa kwa mbunge huyo.
Ameandika: "Nimepokea kwa masikitiko tukio la kupigwa risasi Mh. Tundu Lissu, namuombea kwa Mwenyezi Mungu aweze kupona haraka. Aidha, vyombo vya dola viwasake wale wote waliohusika na tukio hili la kinyama na kuwafikisha ktk mikono ya sheria."
Kwa mujibu wa taarifa ya chama kikuu cha upinzani CHADEMA kwa vyombo vya habari, tukio hilo lilitokea wakati mbunge huyo wa Singida Mashariki akiwa nyumbani kwake.
Chama hicho kimelaani vikali tukio hilo.
Wakati huo huo, Chama tawala cha CCM, kupitia Katibu wao wa Itikadi na Uenezi,imesema kimepokea kwa mstuko mkubwa kushambuliwa kwa mbunge huyo wa upinzani.
"Chama cha Mapinduzi (CCM) kinalaani tukio hilo la kikatili na lisilo na utu tunalitaka Jeshi la Polisi kuwatafuta, kufanya uchunguzi wa tukio hili na kuchukua hatua kali za kisheria kwa wote waliohusika."
Kamanda wa polisi mkoani Dodoma, Kamishna Msaidizi, Jires Mroto ameiambia BBC kuwa wameanza uchunguzi wa tukio hilo.
"Tunaomba wananchi wenye taarifa ya uhalifu huu, waweze kujitokeza" amesema Kamanda Mroto.
Hivi karibuni, mbunge huyo kutoka chama cha upinzani cha CHADEMA, amekuwa akikamatwa mara kwa mara na polisi akishutumiwa kufanya uchochezi.
Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, akithibitisha tukio la leo alisema, amesema "yupo hospitali, bado anajaribu kupambana kuokoa maisha yake"
Gazeti la Mwananchi nchini Tanzania, limemnukuu Mganga mkuu wa hospitali ya Dodoma akisema wakili huyo ana majeraha ya risasi miguuni na tumboni.
No comments:
Post a Comment