Thursday, September 28

Madereva wafutiwa leseni


Dar es Salaam. Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Muslimu amewafutia leseni madereva saba kwa makosa ya kuendesha mabasi ya abiria kwa mwendo kasi na hatarishi wa zaidi ya kilomita 90 kwa saa.
Pia, mabasi 11 yamefungiwa kutoa huduma ya kusafirisha abiria kwa makosa ya mwendo kasi.
Mabasi hayo ya kampuni tofauti wamiliki wake wametakiwa kuhakikisha vifaa vya kudhibiti mwendo kasi vinafanya kazi.
Muslimu amesema kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani, Tangazo la Serikali namba 31 la mwaka 2015 kanuni namba 5 ya sheria hiyo anafuta madaraja C na E katika leseni za madereva hao.
Amesema hawataruhusiwa kuendesha magari ya abiria na mizigo kibiashara kwa kipindi cha miezi sita hadi watakaporudi darasani wakasome, watahiniwe na wafaulu ndipo warejeshewe madaraja hayo.
Muslimu amesema operesheni iliyoanza Septemba 18 hadi 24 imewezesha kukamatwa madereva hao ambao wamefikishwa mahakamani na wamekiri makosa.
Amesema madereva hao wamelipa faini ya kati ya Sh100,000 na Sh300,000.
"Kwa madereva hao kutiwa hatiani wamepoteza sifa ya kuendesha magari ya abiria kibiashara. Nimetoa taarifa kwa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na waajiri wao watajulishwa ili wasiendeshe mabasi yao,” amesema.

No comments:

Post a Comment