Wamesema tatizo linatokana na shambulio hilo kuingiliwa na harufu za kisiasa tangu mwanasheria huyo mkuu wa Chadema apigwe risasi, wakitolea mfano wa zuio la uchangiaji damu, mivutano ndani ya Bunge na zuio la wafuasi wa Chadema kufanya maombi Sumbawanga.
Polisi ilipiga marufuku ya mkusanyiko wa maombezi hayo uliokuwa umeandaliwa na Chadema mjini Sumbawanga kwa madai kwamba utasababisha uvunjifu wa amani.
Baada ya zuio hilo, Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) lilitangaza kufanya maombi kama hayo ya Sumbawanga leo jijini Dar es Salaam huku likiwaalika viongozi mbalimbali wa dini lakini kabla siku ya tukio, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa aliyazuia na kutangaza kutoruhusu mkusanyiko wowote wenye nia ya kumuombea mtu fulani.
Maombi ya Bavicha yamepangwa kufanyika katika viwanja vya TIP, Sinza na tayari viongozi mbalimbali wa Kiislamu na Kikristo wamealikwa kwa ajili ya kuongoza maombi hayo.
Akizungumzia hatua hiyo ya polisi Mwanaharakati wa Mtandao wa TGNP, Gemma Akilimali alisema: “Polisi wanasema siyo tukio la kwanza kutokea, ina maana ya kwamba wananchi waendelee kukaa kimya? Mbona mikusanyiko ya maombi mengine hufanyika uwanja wa Taifa na kwenye matamasha? Alihoji,
Gemma alisema tukio la Lissu limeitikisa nchi, lakini kwa bahati mbaya limehusishwa na siasa tangu mapema. Alisema licha ya Polisi kuzuia mkusanyiko huo, bado wananchi wanayo nafasi ya kutumia nyumba za ibada kufikisha maombi yao.
Hata hivyo, aliwaomba wananchi wasiendelee kushindana na vyombo vya dola na badala yake watumie njia nyingine kupaza sauti zao kuhusu matukio hayo ya uhalifu nchini.
Kwa upande wake Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Gaudence Mpangalla alisema tatizo ni hofu za kisiasa kwamba, endapo mkusanyiko huo utafanyika, Chadema na vyama vya upinzani vitajiongezea umaarufu wa kisiasa kupitia huruma ya wananchi.
Profesa Mpangalla alisema kilichosikitisha zaidi ni pamoja na zuio la wananchi kuchangia damu. “Lissu ni Mtanzania na kiongozi, alishtua Watanzania kwa hiyo kuombewa ni bora, lakini tatizo ni siasa tu, kwamba mikusanyiko itaipa nguvu upinzani,”alisema.
Awali, Bavicha ilisisitiza kwamba haitarajii kuona maombi hayo yakizuiliwa kwa sababu hawaendi kufanya siasa, bali maombi kwa ajili ya Lissu na viongozi wengine wa Taifa kama ambavyo wamekuwa wakitoa wito wa kuombewa.
Profesa Mohammed Bakari kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Bora, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) alisema dalili za kuhatarisha usalama zingeonekana kuanzia siku ya tukio baada ya Lissu kupigwa risasi, lakini wananchi walikuwa na utulivu.
Profesa Bakari alisema zuio hilo ni mwendelezo wa utekelezaji wa agizo la rais la kuzuia mikutano ya hadhara.
“Lakini, polisi wanahofu kunaweza kujitokeza hali ya taharuki watu wakaingiza masuala ya kisiasa ndani yake badala ya lengo lililokusudiwa katika maombi, lakini kwa ujumla hakuna hoja ya msingi kuzuia mkusanyiko huo,”alisema.
Profesa huyo alipendekeza maombi hayo yaendelee katika nyumba za ibaada kwa kuwa hakutakuwa na kizuizi chochote kutoka vyombo vya dola.
No comments:
Post a Comment