Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga kusikiliza kwa siku nne mfululizo, kesi ya kuhujumu uchumi inayowakabili washtakiwa watatu akiwemo raia wa China.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Salvius Matembo, Philemon Manase na raia wa China anayedaiwa kuwa ni Malkia wa Pembe za Ndovu, Yang Feng Glan (66) ambao kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya kuhujumu uchumi kwa kujihusisha na biashara haramu ya Meno ya Tembo yenye thamani ya Sh 13 bilioni, kinyume cha sheria.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu
Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shahidi baada ya pande wa utetezi na ule wa mashtaka kuiomba mahakama hiyo isikilize ushahidi kwa siku nne mfululizo.
Hata hivyo maombi hayo yalikubaliwa na Hakimu Shahidi ambaye alisema kuwa kesi hiyo itaendelea na ushahidi wa upande wa mashtaka kuanzia Oktoba 17 hadi 20.
Awali, Wakili wa Serikali Paul Kadushi aliiambia mahakama hiyo kwamba kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi lakini mashahidi wawili ambao walipaswa kutoa ushahidi wao jana, wapo mkoani kikazi, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa pamoja wanakabilia na kesi ya uhujumu uchumi kwa kujihusisha na biashara ya Meno ya Tembo yenye thamani ya Sh 13 bilioni.
No comments:
Post a Comment