Saturday, August 26

Wabunge waliofukuzwa CUF wagonga ukuta tena mahakamani




Wabunge hao pamoja na madiwani wawili pia wa viti maalumu walikuwa wakiiomba Mahakama Kuu kuzuia kwa muda kuapishwa wabunge walioteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kushika nafasi hizo.
Pia walikuwa wakiiomba mahakama hiyo itoe amri ya zuio la muda dhidi ya wakurugenzi wa manispaa za Ubungo na Temeke, kutoteua madiwani wengine na kuwaapisha, wakati wa kusubiri kumalizika kwa kesi yao ya msingi, waliyoifungua kupinga kuvuliwa uanachama.
Hata hivyo, harakati zao hizo hazikuzaa matunda baada ya mahakama hiyo kutupa maombi hayo kutokana na pingamizi la awali lililowekwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kulizuia Bunge kutekeleza majukumu yake.
AG alikuwa akimwakilisha mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Katibu wa Bunge na wakurugenzi wa manispaa hizo.
Akitoa uamuzi huo, Jaji Lugano Mwandambo alisema anakubaliana na hoja zilizotolewa na wakili mwandamizi wa Serikali, Haruni Matagane kuwa mahakama haina mamlaka ya kulizuia Bunge kwa kuwa hilo ni jukumu lake la kikatiba.
Jaji Mwandambo alisema anakubaliana na hoja za Wakili Matagane kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 4 (1) ya Katiba inayozungumzia mgawanyo wa madaraka, kila mhimili uko huru kutekeleza majukumu yake bila kuingiliwa na mhimili mwingine, kama haukuvuka mipaka ya mamlaka yake.
Alisema kwa mujibu wa Ibara ya 68 ya Katiba, Bunge kuwaapisha wabunge ni moja ya majukumu yake ya kikatiba na kwamba kwa hali hiyo mahakama haina mamlaka ya kuliingilia.
AG katika pingamizi lake alikuwa amewasilisha hoja mbili za pingamizi. Mbali na hoja hiyo ya mamlaka ya Bunge, hoja nyingine ilikuwa ni kwamba kifungu kilichotumika kufungua maombi hayo, hakikuwa sahihi kinachoiwezesha mahakama kuyasikiliza.
Hata hivyo, Jaji Mwandambo hakukubaliana na hoja ya kifungu hicho cha 95 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai waliosema kuwa si sahihi, na badala yake kukubaliana na hoja za wakili wa wabunge hao, Peter Kibatala.
Hata hivyo, Jaji Mwandambo alisema kukubaliana na hoja ya AG kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kulizuia Bunge kuwaapisha wabunge hao wateule, hakumaanishi kuwa maombi yote ya wabunge waliovuliwa uanachama yametupiliwa mbali, isipokuwa hoja hiyo ya kuzuia kuapishwa.
Hivyo, maombi hayo yatasikilizwa Jumatatu, yakihusu nafuu nyingine zinazoombwa kama kutotangazwa kwa nafasi za madiwani wawili waliovuliwa uanachama na kuteuliwa wengine badala yao.
Wabunge hao wamefungua kesi dhidi ya bodi ya wadhamini ya CUF, mwenyekiti na kaimu katibu mkuu wa chama hicho, ambao pia walitoa taarifa ya pingamizi la awali lakini wakati wa usikilizwaji, hawakuweza kuwasilisha hoja zao na hivyo mahakama haikuziingiza sababu zao.
Hii ni mara ya pili kwa wabunge hao waliotimuliwa kugonga ukuta katika maombi yao ya kuzuia kuapishwa kwa wabunge walioteuliwa kuchukua nafasi zao, baada ya kuwekewa pingamizi kuwa kifungu walichokitumia hakikuwa sahihi.
Jaji Mwandambo alikubaliana na hoja hiyo na kuyatupilia mbali maombi hayo, lakini wabunge hao waliyafungua upya baada ya kufanya marekebisho ya kifungu hicho.
Lakini hata baada ya kufungua upya maombi hayo, AG aliwawekea pingamizi jingine kwa hoja zilezile kama za mwanzo
Safari hii, Jaji Mwandambo alitupa mbali pingamizi la Serikali la matumizi ya kifungu kisicho sahihi badala yake akakubaliana na hoja ya mgawanyo wa madaraka wa mihimili mitatu ya nchi.
Wabunge hao pamoja na madiwani walivuliwa uanachama na bodi ya wadhamini ya CUF kwa madai ya kushirikiana na Chadema kutaka kuondoa wanachama wa chama hicho walioitwa kuwa ni wasaliti.
CUF iko kwenye mgogoro wa uongozi tangu mwaka 2016 na juhudi za kujaribu kuondoa tofauti hizo zimeshindikana kutokana na upande mmoja kukataa kukaa meza moja kwa madai kuwa upande mwingine umesaliti chama.

No comments:

Post a Comment