TANZANIA YAHUDHURIA MKUTANO MKUU WA SKAUTI WA DUNIA MJINI BAKU, AZERBAIJAN
Mkutano Mkuu wa Skauti wa Dunia unafanyika nchini Azerbaijan katika mji wa Baku kuanzia tarehe 14 hadi 18 Agosti 2017. Mkutano huu utajumuisha nchi zote wanachama ambao zinafikia nchi 167. Kila nchi inapaswa kutuma wajumbe 6 kuhudhuria mkutano huu, lakini pia waangalizi (Observers) wanakaribishwa.
Ni mkutano mkuu ambao unazungumzia masuala mbalimbali yanayohusu mafunzo kwa vijana skauti, miradi mbalimbali, mafanikio na changamoto mbalimbali zinazokabili nchi wanachama.
Tanzania inawakilishwa na wajumbe 6 muhimu kama Katiba ya Shirikisho la Vyama vya Skauti Duniani (World Scout Bureau) inavyosema, lakini pia ujumbe huo unaongozwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya nne Mheshimiwa DK. Jakaya Mrisho Kikwete, kama Mlezi Mstaafu wa Chama cha Skauti Tanzania. Kwa kawaida Mlezi wa Chama cha Skauti Tanzania ni Rais wa Nchi kwa mujibu wa Katiba ya Chama cha Skauti Tanzania.
Mheshimiwa DK. Jakaya Kikwete amepewa Heshima ya kuwa Msemaji Mkuu (Keynote Speaker) wa ujumbe wa Chama cha Skauti Tanzania.
Ujumbe wa Chama cha Skauti Tanzania tayari umeshaondoka nchini kuhudhuria Mkutano huo, ambapo Mheshimiwa DK. Jakaya Kikwete ameomba kukutana na Viongozi wa Vyama vya Skauti nchi za Afrika kuzungumza na kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu uskauti barani Afrika wakati wa Mkutano Mkuu huo.
Ujumbe wa Chama cha Skauti Tanzania ni pamoja na Skauti Mkuu Mheshimiwa Mwantumu Bakari Mahiza. Kamishna Mkuu Mheshimiwa Abdulkarim Esmail Shah. Naibu Kamishna Mkuu ndugu Rashid Kassim Mchatta. Kamishna Mtendaji Bi. Eline Kitaly. Na Kiongozi wa skauti kutoka mkoa wa Dar es salaam ndugu. Dinesh Rajah.
Chama cha Skauti Tanzania kimetimiza Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake hapa nchini, na sherehe za maadhimisho hayo zilifanyika mkoani Dodoma kuanzia tarehe 21 hadi 28 Julai 2017 ambapo Viongozi mbalimbali wa Kitaifa walialikwa wakiwemo Marais Wastaafu, Mawaziri Wakuu, pamoja na Skauti wenyewe kutoka ndani na nje ya Nchi.
Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa Maadhimisho hayo alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan ambaye alimuwakilisha Rais DK. John Pombe Magufuli.
Tuzo na Nishani kadhaa zilitolewa kwa Viongozi mbalimbali wa Nchi, Viongozi wa Skauti, na skauti wenyewe ambao wameshiriki katika matukio ya ujasiri, michezo na mashindano za stadi za kiskauti.
Maadhimisho ya Miaka 100 ya Skauti Tanzania yalifungwa na Makamu wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi.
Ujumbe wa Viongozi wa Chama cha Skauti Tanzania ambao wanahudhuria Mkutano Mkuu wa Skauti wa Dunia pia utapokea Tuzo na Cheti maalum cha kutimiza Miaka 100 ya uskauti Tanzania, ujumbe huo unatarajia kurejea nchini tarehe 21 Agosti 2017.
IMETOLEWA NA HIDAN .O. RICCO.
KAMISHNA MKUU MSAIDIZI
Rais Mstaafu wa Awamu ya nne Mheshimiwa DK. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa Mkutano Mkuu wa Skauti wa Dunia mjini Baku, Azerbaijan
Rais Mstaafu wa Awamu ya nne Mheshimiwa DK. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa kwenye sherehe za maadhimisho ya miaka 100 ya Skauti nchini zilipofanyika mkoani Dodoma mwezi Julai. Pamoja naye ni Skauti Mkuu Mheshimiwa Mwantumu Bakari Mahiza (kushoto). Kamishna Mkuu Mheshimiwa Abdulkarim Esmail Shah (kulia) na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana
Rais Mstaafu wa Awamu ya nne Mheshimiwa DK. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa Mkutano Mkuu wa Skauti wa Dunia huko Baku nchini Azerbaijan
No comments:
Post a Comment