Hayo yamesemwa leo Jumanne wilayani Lushoto na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo Makani, akiwa kwenye ziara ya kikazi ya siku moja wilayani humo kwa ajili ya kutatua migogoro mbalimbali katika maeneo ya uhifadhi.
Alisema sekta ya utalii nchini imekuwa ikitegemea sana wanyamapori na kusahau vivutio vingine kama vile misitu ya asili ambayo ndani yake kuna mimea na viumbe hai mbalimbali adimu duniani na ambavyo hupatikana Tanzania pekee.
“Tumezoea zaidi utalii wa wanyamapori… lakini utalii wa misitu unaweza kuzidi hata wa wanyamapori. Kwenye misitu yetu ya asili tunajivunia mimea adimu ya asili na viumbe hai mbali mbali kama vile ndege, vyura, vipepeo, mijusi na kadhalika. Tunachotakiwa kufanya ni kutunza misitu yote ya asili, tuiboreshe na kuitangaza ili kupata watalii wengi zaidi na pato la Taifa liendelee kukua,” alisema Makani.
Kwa mujibu wa tovuti ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Tanzania ina jumla ya Hifadhi za Misitu ya Asili 100, idadi ambayo ni kubwa ukilinganisha na hifadhi za taifa ambazo zipo 16 pekee. Pamoja na upekee wake, idadi hiyo kubwa inatoa fursa pana ya kuendeleza sekta ya utalii nchini.
Akizungumzia mafanikio, Makani alisema sekta hiyo inachangia asilimia 17.2 ya pato la taifa na asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za kigeni.
Alisema pamoja na faida hizo, sekta hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya uharibifu wa misitu ya asili ambayo ni muhimu kutafutiwa suluhu ya kudumu ili kunusuru misitu hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Januari Lugangika, alisema wilaya yake inakabiliwa na changamoto mbalimbali za uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji wa miti ya asili, uchimbaji wa madini kwenye maeneo ya hifadhi, uchomaji moto misitu na uhaba wa watumishi.
Katika ziara yake hiyo wilayani Lushoto, Naibu Waziri Makani alitembelea pia Hifadhi ya Mazingira Asilia Magamba na Shamba la Miti la Shume.
No comments:
Post a Comment