Thursday, August 24

Kiungo wa Yanga afungiwa mwaka mmoja

Dar es Salaam. Kamati ya Katiba,Sheria na Hadhi za wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imemfungia mwaka mmoja kiungo mpya wa Yanga, Pius Buswita.

Kiungo huyo aliyeichezea Mbao msimu uliopita, amefungiwa mwaka mmoja kutokana na kubainika kusaini timu mbili tofauti.
Kamati ya Katika Sheria na Hadhi za wachezaji inayoongozwa na Richard Sinamtwa, inegundua na kubaini Buswita amesaini mkataba na klabu mbili tofauti katika msimu mmoja wa 2017/2018" ilisema taarifa na TFF
Taarifa hiyo ilisema Kamati imebaini kwamba mchezaji huyo aliyechezea Mbao FC ya Mwanza msimu uliopita, amevunja Kanuni ya 66 ya Ligi Kuu  ambayo inaelekeza adhabu ya kufungiwa mwaka mmoja hivyo  mchezaji huyo amefungiwa kucheza mpira wa miguu kwa mwaka mmoja.
Pia kamati hiyo imebaini upungufu katika uwasilishaji wa majina ya wachezaji wa msimu wa 2017/18 kwa timu zote hivyo kuziagiza klabu  zote kuleta majina matatu ya wachezaji wasiopungua 18 na wasiozidi 30 wa kikosi cha timu ya vijana (U20).
Klabu pia  zimeagizwa kuanisha wachezaji wa zamani na wapya na klabu wanazotoka kwa timu zote mbili za wakubwa na vijana huku zikizingatia matakwa ya kanuni kwa kila mchezaji ili aweze kupatiwa leseni.
Matakwa hayo ambayo yamesisitizwa ni kila mchezaji kujaziwa fomu ya utimamu wa mwili, kuwasilisha nakala tatu za mikataba ya wachezaji TFF, Uthibitisho wa kukatiwa Bima, Barua ya Uhamisho kutoka timu ambayo ametoka pia wachezaji wa kigeni  kuwa na Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) na kulipiwa Ada ya ushiriki ya msimu Sh. 2,000,000.
Wakati huo TFf imetangaza kuwa msimu ujao wa 2018/2019  Ligi Kuu Bara itapandisha idadi ya timu kutoka 16 ilivyo sasa hadi 20.

Kamati ya Utendaji ya TFF imefikia uamuzi huo juzi Jumanne katika kikao chake na sasa i inafanya marekebisho ya Kanuni za Ligi Daraja la Kwanza inayotarajiwa kuanza Septemba 16, mwaka huu.
Kwa marekebisho hayo, timu zitakazoshuka daraja msimu ujao kutoka Ligi Kuu Bara zitakuwa mbili huku sita zikipanda daraja kutoka Ligi Daraja la Kwanza.
Hiyo ina maana msimu huu timu mbili zitapanda kutoka katika kila kundi katika ligi daraja la kwanza.
Katika Ligi daraja la kwanza, kundi A lina timu za African Lyon, Ashanti United, Friends Rangers za Dar es Salaam, JKT Ruvu na Kiluvya United za Pwani, Mgambo JKT ya Tanga, Mvuvumwa ya Kigoma na Polisi Moro ya Morogoro.
Kundi B  lina  Coastal Union ya Tanga; JKT Mlale ya Ruvuma; KMC ya Dar es Salam, Mawezi Market ya Morogoro, Mbeya Kwanza ya Mbeya, Mufundi United ya Iringa, Mshikamano na Polisi Dar za Dar es Salaam.
Wakati kundi C lina timu za Alliance School, Pamba na Toto African za Mwanza, Rihno Rangers ya  Tabora, Polisi Mara ya Mara, Polisi Dodoma ya Dodoma, Transit Camp ya Shinyanga na JKT Oljoro ya Arusha.

No comments:

Post a Comment