Sifa hizo zilitolewa jana na katibu mkuu wa wizara hiyo, Profesa Elisante Ole Gabriel alipotembelea ofisi za MCL zilizopo Tabata Relini, Dar es Salaam.
MCL ni wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen, Mwanaspoti na MCL Digital, ambacho ni chombo cha habari cha mtandaoni.
Akizungumza na waandishi baada ya ziara hiyo, Profesa Gabriel alisema amefurahishwa na jinsi MCL inavyofanya kazi zake za kuhabarisha, akisema kitendo cha kutoa nafasi kwenye gazeti la Mwananchi kwa ajili ya Serikali kuweka makala zake za “Tunatekeleza” kinafaa kuigwa na vyombo vingine.
“Hili ni jambo la kizalendo linalofanywa na MCL kutangaza shughuli za Serikali, naviomba vyombo vingine vya habari kuiga mfano huu,” alisema.
Safu hiyo huchapishwa kila siku ya Jumamosi ikieleza jinsi Serikali inavyotekeleza mikakati yake ya kuelekea uchumi wa viwanda.
Katibu huyo pia alisifu kitendo cha MCL kuwa na kitengo cha Swahili Hub, kinachohusisha vyombo vyote vya kampuni mama ya Nation Media Group (NMG) kwa ajili ya kukuza lugha ya Kiswahili.
Alishauri kuwepo na mawasiliano na Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) ili kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Pia alisema MCL imejenga jina zuri katika habari na kwamba uwekezaji uliofanywa ni mkubwa na kutaka wafanyakazi waulinde kwa kuwajibika.
“Malengo ya kila mwekezaji ni kupata faida, hivyo viongozi na wafanyakazi mfanye kazi kwa weledi ili kulinda jina zuri ambalo mmelijenga kwa muda mrefu,” alisema.
Alisema ni rahisi kubomoa jina hilo kuliko kulijenga.
“Fedha zilizowekezwa hapa zinatakiwa kurudi hivyo chapeni kazi lakini uongozi pia uwawekee wafanyakazi mazingira bora ya kazi,” alisema.
Pia aliutaka uongozi wa MCL kuwaendeleza kielimu wafanyakazi wake ili wawe na tija katika utendaji wa kazi.
“Mkidhani kwamba kuwaendeleza wafanyakazi ni gharama kubwa, basi jaribuni kutowaendeleza muone,” alisema.
Profesa Gabriel alisema lengo la ziara yake ni kuweka uhusiano mzuri kati ya Serikali na vyombo vya habari.
“Ni lazima jamii ielewe kwamba Serikali ni kama mzazi na vyombo vya habari ni kama mtoto hivyo ni muhimu kuwa na mahusiano mazuri,” alisema.
Akijibu moja ya maswali kuhusu sheria zinazokandamiza uhuru wa habari, katibu mkuu huyo alisema Serikali huwa haina nia hiyo.
“Hata tunapochukua uamuzi wa kukifungia chombo cha habari huwa hatufurahishwi. Tunakifungia chombo cha habari huku tukijiuliza na kusikitika kwa nini kimeshindwa kufuata sheria na kanuni zilizopo,” alisema.
Alitaka wadau wa habari kuisoma Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, akiisifu kuwa “ni tamu kuliko pipi”.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Francis Nanai alisema kampuni hiyo itaendelea kufanya kazi kwa kufuata maadili ya kazi na uzalendo
“Tutaendelea kuwa wazalendo kwa kuwapasha wananchi habari zenye kufuata utamaduni na maadili ya Taifa letu,” alisema.
Alisema kumekuwapo na madai kutoka kwa baadhi ya watendaji wa Serikali kuwa wameelekezwa wasitoe matangazo kwa baadhi ya vyombo vya habari na kutaka suala hilo liwekwe bayana au yatolewe kwa haki.
Nanai pia alishauri Serikali kuangalia namna ya kuweka nguvu katika ujenzi wa viwanda vya karatasi zinazotumika kuchapishia magazeti ili kupunguza gharama za kuagiza nje.
“Tuna magazeti ambayo muda ukishapita yanaweza kutumika kutengeneza bidhaa nyingine, hii itatusaidia kuongeza mapato ya kampuni na kodi kwa Serikali,” alisema.
Katibu huyo alisema amepokea mapendekezo hayo.
No comments:
Post a Comment