Thursday, August 24

Ghorofa, hoteli za kifahari kubomolewa

Hoteli ya Dolphins ya jijini Tanga likiwa

Hoteli ya Dolphins ya jijini Tanga likiwa imewekewa alama ya X ikitakiwa kubomolewa kwa madai ya kujengwa katika eneo ambalo ni hifadhi ya reli. Zaidi ya nyumba 100 zikiwamo hoteli, maghala na makazi zinatakiwa kubomolewa. Picha na Burhani Yakub 
Tanga. Bomoabomoa iliyoendeshwa jijini Dar es Salaam na Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco), sasa inahamia Tanga ambako zaidi ya nyumba 100 zikiwamo hoteli, maghala na makazi zitabomolewa.
Tayari kazi ya uwekaji alama za X inayotekelezwa na wataalamu kutoka Rahco imekamilika huku ikizusha vilio kwa wamiliki.
Majengo hayo yanadaiwa kujengwa katika hifadhi ya reli na maeneo yaliyokuwa yamewekwa wazi kwa ajili ya matumizi ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRL).
Bomoabomoa hiyo itazikumba nyumba zilizopo mitaa ya Usagara, Central Baker na Chuda, huku wamiliki wakipewa notisi ya siku 30 kubomoa.
Miongoni mwa majengo yaliyowekwa X ni duka maarufu la Central Baker, hoteli za Malindi, Dolphine, Dakau Annex, Misisipi, Loliondo, Nyinda Tourist, Kanan, Macarious, Malibu Kiboma na maghala ya kuhifadhia bidhaa yaliyopo Gofu.
Wakati wa uwekaji wa alama hizo, wataalamu wa Rahco wanafanya kazi chini ya ulinzi wa Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), huku wananchi wakiwa wamekusanyika kushuhudia.
Mkuu wa kundi la wataalamu kutoka Rahco, Enock Mgonja alisema walianza kazi hiyo Agosti 15 na itachukua wiki mbili kukamilika.
“Tunaweka X kwenye nyumba zilizojengwa ndani ya hifadhi ya reli na maeneo yaliyokuwa yamesahaulika kwa kipindi kirefu, hivyo kuvamiwa. Waliojenga wanatakiwa ndani ya siku 30 wabomoe wenyewe,” alisema.
Mgonja alisema tayari kazi imefanyika Dar es Salaam, Morogoro, Kigoma na maeneo mengine yenye reli na baada ya Tanga wataelekea Kilimanjaro.
“Hatuna lengo la kuwaonea waliowekeza lakini sheria iko wazi. Nitumie nafasi hii kuwaeleza wanaojua wapo eneo la reli wabomoe haraka,” alisema.
Wananchi walia
Baadhi ya wamiliki wa majengo walisema hawajatendewa haki kwa sababu maeneo hayo walipewa kwa njia halali na mamlaka za Serikali na hawakuelezwa kama ni hifadhi ya reli.
“Tumechukua mikopo mikubwa kwenye benki tuwekeze katika hoteli kwa lengo la kujiandaa na uwekezaji mkubwa unaokuja Tanga,” alisema Mkurugenzi wa Hoteli ya Dolphine, Anna Ismail.
Naye Hassan Jumaa (75), ambaye nyumba yake ipo Mtaa wa Chuda alisema hatua hiyo itasababisha afe kwa shinikizo la moyo kwa sababu hana sehemu ya kwenda kutokana na kustaafu miaka mingi hana fedha za kujengea nyingine.

No comments:

Post a Comment