‘Wenye hasira kali’ hao wamekatisha uhai wa watu 479 kuanzia Januari mpaka Juni mwaka huu.
Mkoa wa Dar es Salaam unatajwa kuwa kinara kwa matukio ya mauaji yanayotokana na wakazi wake kujichukulia sheria mkononi.
Hali hiyo ilibainishwa jana jijini hapa na Mtafiti wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fundikira Wazambi wakati wa uzinduzi wa ripoti ya hali ya haki za binadamu kwa kipindi cha nusu mwaka kuanzia Januari hadi Juni, 2017.
“Katika ripoti yetu tumebaini ndani ya kipindi hicho watu kadhaa wameuawa kwa sababu mbalimbali, ikiwamo tuhuma za ushirikina na watu kujichukulia sheria mkononi.
Alinukuu ripoti ya polisi kuwa jumla ya watu 479 wameuawa nchini kutokana na watu kujichukulia sheria mkononi.
Taarifa hiyo inaonyesha kuwa Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa matukio hayo kwa kuwa na vifo 117, ukifuatiwa na Mbeya (33), Mara (28) na Geita (26).
Mkurugenzi wa LHRC, Dk Helen Kijo Bisimba alisema kituo hicho pia kimepokea malalamiko kutoka kwa wananchi wakidai kuteswa na wengine wameuawa kwa tuhuma za mauaji yanayofanyika Kibiti, Mkuranga na Rufiji mkoani Pwani.
“Kuna vifo tisa ambavyo vinahusisha vyombo vya dola, ingawa Jeshi la Polisi katika taarifa yake inaonyesha ni mtu mmoja pekee ndiyo aliuawa akiwa mikononi mwa polisi,” alisema.
Akizungumzia hali ya usalama wa watoto alisema kuna unyanyasaji mkubwa na matukio ya ukatili hasa wa ngono na hadi Juni matukio 121 yameripotiwa.
Kutokana na matukio hayo, LHRC imetoa ushauri kwa Serikali na Bunge kushughulikia kwa kuzingatia changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika sheria.
Dk Bisimba alisema kuna mambo kadhaa yanayotendeka nchini kinyume cha haki za binadamu na sheria.
“Ripoti inaonyesha kuwa hali ya haki za binadamu ni mbaya kwa kipindi cha nusu mwaka 2017 ikilinganishwa na miaka iliyopita, hii imesababishwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za kiraia na za kisiasa, hususani haki ya kuishi na kuminywa kwa uhuru wa kujieleza,” alisema Dk Bisimba.
“Kutokana na hayo tuliyobaini tuna mapendekezo mengi ikiwamo, Wizara ya Katiba na Sheria kuhakikisha sheria zinazobana uhuru wa kujieleza kama huduma ya habari na sheria ya makosa ya mtandaoni zinafanyiwa marekebisho haraka,” alisema.
No comments:
Post a Comment