Tuesday, August 29

Bomoabomoa mpya ya kufa mtu yaja


Dar es Salaam. Kama ulidhani kuwa bomoabomoa ya Tanroads iliyoanzia Kimara hadi Kiluvya ikitarajiwa kuzikumba nyumba takriban 1,300 ni kubwa utakuwa umekosea. Sasa inakuja nyingine ya ‘kufa mtu’ hii ikiwahusu waliojenga katika hifadhi ya Bonde la Mto Msimbazi wilayani Ilala na inatarajiwa kuzikumba zaidi ya nyumba 17,000 kuanzia vilima vya Pugu hadi Daraja la Selander.
Hivi sasa wakazi wa Kimara hadi Kiluvya walio ndani ya hifadhi ya Barabara ya Morogoro (mita 121.5 kutoka katikati ya barabara), wameanza kuondolewa.
Wakati operesheni hiyo ikiwa imeshika kasi, jana Ofisa Mipango Miji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Charles Mkalawa aliyeambatana na Mwanasheria Mwandamizi wa Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi ya Mazingira (Nemc), Heche Suguti alisema nyumba hizo ni miongoni mwa zilizowekewa alama ya X katika bomoabomoa iliyositishwa mwaka jana.
“Tulipositisha mwaka jana baadhi ya wakazi walikimbilia mahakamani na wengine waliomba kubomoa wenyewe nyumba zao. Hata hivyo, Serikali ilishinda kesi lakini watu wakaendelea kujenga katika hifadhi ya Mto Msimbazi,” alisema Dk Mkalawa.
Alisema eneo la Bonde la Mto Msimbazi liliwekewa mpango mwaka 1945 uliokwenda sanjari na katazo la watu kutojenga wala kuishi, lakini alisema utafiti umebaini kuwa watu walianza kuvamia na kujenga kuanzia mwaka 1990 wakati mpango huo umeshawekwa.
Bomoabomoa hiyo huenda ikawezesha mpango wa Serikali uliotangazwa bungeni mapema mwaka 2011 na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka kwamba imelitenga Bonde la Mto Msimbazi kuwa bustani ya mapumziko.
Profesa Tibaijuka ambaye alikuwa akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2011/12, alisema kutengwa kwa bonde hilo kumetokana na ukweli kuwa Jiji la Dar es Salaam lenye wakazi wengi, halina sehemu ya kupumzikia.
Alisema kuwa kuzingatia hali hiyo jiji, kwa kushirikiana na halmashauri za manispaa za Kinondoni na Ilala, wameandaa mpango wa kuboresha eneo hilo.
Alisema eneo hilo linahusisha kata za Buguruni, Hananasif, Jangwani, Kinondoni, Kigogo, Magomeni, Mchikichini, Tabata, Upanga Magharibi na Vingunguti.
Alisema eneo hilo litatumika kwa shughuli za michezo, burudani na matumizi mengine ya kawaida na kwamba kwa kuzingatia hatua hizo, hakutakuwa na suluhu kwa wananchi waliovamia na kujenga katika bonde hilo na kwamba wale ambao wanaendelea kufanya shughuli zao ndani ya eneo hilo wanapaswa kuondoka mara moja.
Profesa Tibaijuka (wakati huo)alisema wakazi waliojenga katika Bonde la Msimbazi, kuanzia Daraja la Selander, Muhimbili, Jangwani hadi Vingunguti wanatakiwa kuondoka mara moja kabla ya Serikali kuwaondoa kwa nguvu.
Baada ya kauli hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Bonaventure Baya alikaririwa akisema kuwa baraza lake lilikuwa na mpango wa muda mfupi wa kati ya Januari 2016 hadi Juni 2016 wa kufanya usafi katika eneo lote kisha kuweka mipaka katika kingo ili lisivamiwe tena.
“Serikali itaandaa mpango wa muda mfupi wa matumizi ya Bonde la Msimbazi na tayari waziri wa ardhi alikwishaagiza wataalamu wakae na kubuni nini kitafanyika baada ya kusafisha eneo lote,” alisema.
Alisema baada ya Juni ndipo ungeandaliwa mpango wa muda mrefu chini ya wizara ya ardhi wa kulifanya bonde hilo kuwa la burudani kwa wakazi wa Dar es Salaam.
Hakuna fidia
Jana, Dk Mkalawa alisema hakuna mwananchi atayelipwa fidia katika mchakato huo na kwamba wangeweza kulipwa endapo eneo hilo lingekuwa bado halijaandaliwa mpango wa kuliendeleza.
“Kisheria mvamizi wa eneo husika hatakiwi kupewa taarifa, badala yake unakwenda kumtoa moja kwa moja. Lakini Serikali imekuwa ya kistaarabu na yenye huruma na inawabembeleza kwa kuwapa taarifa za kuondoka,” alisema Dk Mkalawa.
Alisema wachache waliopewa viwanja ilikuwa ni huruma ya Serikali na kuwataka waliovamia waondoke kwa sababu ni hatari kuendelea kuishi kwenye eneo hilo na ni kinyume cha sheria.
Baadhi ya wakazi waliokuwa wakiishi katika bonde hilo eneo la Jangwani, walipewa maeneo na Serikali huko Mabwepande baada ya kukumbwa na mafuriko mwaka 2012.
Mikoani wajiandae
Akizungumzia operesheni hiyo mpya, Heche alisema haitaishia Dar es Salaam pekee na kwamba itafika hadi mikoani ili kuwaondoa wote waliovamia na kujenga kandokando ya mito na bahari kinyume cha sheria.
Kuhusu Bonde la Msimbazi, alisema halifai kwa makazi ya binadamu kwa sababu linakumbwa na mafuriko yanayosababisha vifo vya Watanzania.
“Mwaka jana tulisitisha operesheni ya kuwaondoa ili kuwapa nafasi ya wao kuondoka. Lakini watu hawa wakiwamo wa Bonde la Mkwajuni wameamua kurudi taratibu na kujenga vibanda vyao, wakati tunawaondoa kipindi hicho, tulitumia mamilioni ya fedha za Serikali ikiwamo kukodi vifaa vya kubomolea nyumba zao.
“Hizi ni fedha za umma haziwezi kutumika bure. Leo tumerudi kuwaeleza tena watu wanaoishi Bonde la Mto Msimbazi kutii agizo lililotolewa na Serikali kuondoka haraka iwezekanavyo kabla hatujaanza operesheni ya bomoabomoa,” alisema Heche.
Alisema bonde hilo lilikuwa na jumla ya nyumba 19,000 na mwaka jana zilibomolewa zaidi 744 na zilizobaki zitafuata katika operesheni inayotarajiwa kuanza wakati wowote.
“Wale wanaokaa katika nyumba hizi ambazo zilishawekwa alama ya X tunawasihi waondoke kabla operesheni haijaanza,” alisisitiza.
Akizungumzia uamuzi huo, mkazi wa Bonde la Mkwajuni, Abdallah Peter alisema hawezi kushindana na Serikali, bali anaomba wapewe maeneo mbadala ya kuishi.
“Serikali ikiamua huwezi kuizuia. Kikubwa ni maandalizi ya tutakapokwenda, wengine hatuna mbele wala nyuma na baadhi yetu kipato kipo chini hatuwezi kumudu gharama za kodi kwa sababu zipo juu,” alisema Peter.
Waziri Lukuvi agongelea msumari
Kauli ya NEMC iliungwa mkono na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ambaye katika mahojiano maalumu aliyowahi kufanya na gazeti hili mwaka jana alisema kutokana na uhaba wa maeneo ya wazi ya kupumzikia, burudani na michezo katika miji mingi nchini hasa Dar es Salaam, wizara yake itaanza kulitumia Bonde la Mto Msimbazi kwa shughuli hizo.
Alisema wananchi waliovamia maeneo hayo ambako kutafanywa bustani ya jiji hawatalipwa fidia na alitoa wito kwa mamlaka na taasisi husika kutoa ushirikiano unaotakiwa kuhakikisha wananchi wanahamishwa.
Hata hivyo, pamoja na mpango huo, Waziri Lukuvi alibainisha changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa shughuli za wizara hiyo kuwa ni pamoja na kuwapo kwa madeni makubwa ya halmashauri zilizokopeshwa fedha katika mfuko wa kupima viwanja.
Alisema kuanzia Julai mwaka 2000 hadi Juni mwaka huu, wizara yake ilitoa mkopo wa Sh1.101 bilioni kwa halmashauri 42 nchini lakini Sh651,758,143 zimerejeshwa huku Sh642,130,579 zikiwa bado.
Katika mradi wa viwanja 20,000 Dar es Salaam, halmshauri husika ilikopeshwa Sh2.62 bilioni ambazo hadi Juni mwaka huu hazijarejeshwa.
Katika kukabiliana na hilo alisema wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha wanashauriana ili halmashauri hizo zirejeshe mikopo yao moja kwa moja kupitia ruzuku zao zinazotolewa na Hazina.
Mbunge hana habari
Alipoulizwa maoni yake kuhusu ubomoaji huo, Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara alisema hana taarifa za kina hivyo hawezi kuzungumza lolote mpaka atakapopata maelezo ya kina.
“Nasubiri nipate taarifa, kwa hiyo kwa sasa siwezi kuzungumza kitu ambacho sijapata maelezo yake kwa undani,” alisisitiza.

No comments:

Post a Comment