Jumamosi, Julai 15, 2017 Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Atufigwege Kasesela alitembelea kituo cha kulea watoto wenye ulemavu kiitwacho Nyumba Ali kilichopo Wilolesi. Nyumba Ali iliundwa na umoja wa wazazi wenye watoto waishio na ulemavu mkoani Iringa.
Lengo la kuunda umoja huo ulikuwa ni kuwakutanisha wazazi ili waweze kuwa na sauti moja katika kubainisha na kusaidiana katika kutatua changamoto mbalimbali zinazo ikumba jamii ya watoto waishio na ulemavu. Akitoa taarifa Mbele ya Mkuu wa wilaya mratibu wa kituo hicho, Adam Duma alisema wamefungua vituo hivyo viwili kimoja kikiwa Wilolesi na kingine Ngome.
Kituo kimoja kinapokea watoto 35. Wamekuwa wanawafanyia mazoezi ya viungo pamoja na kuwafundisha kazi za mikono mbalimbali watoto wenye ulemavu wa viungo na akili.
Akizungumza na wazazi na walezi wa kituo hicho, Mkuu wa wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alisema “ Nasikitishwa na baadhi ya wazazi ambao wanajaliwa kupata watoto wenye ulemavu na kuwatelekeza hili halikubaliki.
Kila afisa tarafa afanye utafiti nyumba hadi nyumba kubaini kama kuna mtoto mlemavu, Nachukia sana tabia ya baadhi ya wakina baba kukimbia watoto wenye ulemavu na kuwachia wakina mama. Hebu wanaume tuache tabia ya kukimbia watoto wenye ulemavu.” alisema. Pia aliwataka wakina baba wajitokeze kufika kwenye kituo sio kuwachia wakina mama peke yao.
Kituo cha Nyumba Ali kimekuwa kikiendeshwa kwa msaada wa wahisani mbalimbali ambapo mahitaji makubwa ni pamoja na chakula, baiskeli za walemavu pamoja na gharama za uendeshaji.
Katika kituo hiki yupo mtoto aitwaye Zawadi ambaye amesomeshwa hadi kiwango cha darasa la saba, Mtoto huyu hawezi kutumia mikono anatumia miguu kwa shida akisaidiwa na kompyuta na amefanikiwa kuandika kitabu kinacho elezea maisha yake.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Atufigwege Kasesela akizungumza na mmoja wa watoto wanaolelewa katika kituo cha kulea watoto wenye ulemavu kiitwacho Nyumba Ali kilichopo Wilolesi, Wilayani Iringa.bofya hapa kwa picha zaidi
No comments:
Post a Comment