Njombe. Mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila umezikwa jana katika Kijiji na Kata ya Milo, Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe.
Katika mazishi hayo yaliyoshuhudiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, ndugu, jamaa na marafiki, waombolezaji walimzungumzia Mchungaji Mtikila wakisema Taifa limempoteza mtu aliyekuwa mstari wa mbele katika harakati za kutetea masilahi ya Taifa.
Jaji Mtungi alisema Mtikila atakumbukwa kwa mambo mengi aliyoyafanya katika Taifa, kwani ni mtu aliyekuwa anapambana kusimamia kitu anachokisimamia.
Alisema marehemu hakuwa mtu wa kupenda njia za mkato kupata kitu, ndiyo maana alikuwa tayari kufungua kesi kuona matokeo ya kitu anachokisimamia.
Alisema Mtikila alikuwa anatetea haki na pia alikuwa anatetea amani ya nchi, jambo linalopaswa kuigwa na kila Mtanzania.
Dada wa marehemu Veronica Mtikila, alisema familia ilikuwa inamtegemea kama alivyokuwa akitegemewa katika kupigania masilahi maskini na wanyonge.
“Kifo hiki kimetushtua sana, alitusaidia kama familia... lakini tunamwachia Mungu,” alisema Veronica.
Marafiki waliosoma pamoja na Mtikila wanaoishi katika Kijiji cha Milo, Noel Haule na Peter Msigwa walisema tangu akiwa shuleni, marehemu alifahamika kutokana na misimamo na harakati zake za kutetea wenzake.
Walisema hata alipokuwa mwanasiasa na mwanaharakati, hawakushangaa kutokana na misimamo yake tangu akiwa mdogo.
“Alikuwa na ushawishi mkubwa tangu akiwa mdogo, alikuwa anaweza kushawishi wengine na wakamwelewa, lakini zaidi alikuwa anapenda kutetea haki,” alisema Msigwa na kuongeza: “Taifa limepoteza mtu muhimu ambaye alikuwa anaikumbusha Serikali kurekebisha mambo pale ilipokuwa inakwenda kinyume.”
Mtikila alifariki dunia Oktoba 4, katika ajali ya gari iliyotokea katika Kijiji cha Msolwa, Chalinze mkoani Pwani alipokuwa akitokea Njombe kwenda Dar es Salaam.
MUNGU AMUWEKE MAHALA ANAPOSTAHILI. AMEN
No comments:
Post a Comment