Tuesday, April 3

Tiangong-1: Chombo cha anga za juu cha China chaanguka Pacific

Radar image of TiangongHaki miliki ya pichaFRAUNHOFER
Image captionChombo hicho cha China kwa jina Tiangong-1 kilifuatiliwa kwa mitambo ya rada
Chombo cha anga za juu cha China kilichoacha kutumika Tiangong-1 kimemeguka vipande vingi kikiingia anga ya dunia na kuanguka maeneo ya bahari kusini mwa Pacific.
Chombo hicho kiliingia anga ya dunia saa 00:15 GMT Jumatatu, idara ya anga za juu ya China imetangaza.
Tiangong-1 ilirushwa angani mwaka 2011 kufanyia majaribio teknolojia ya kuunganisha vyombo mbalimbali anga za juu na pia vyombo vya kuzunguka kwenye mzingo wa dunia.
Chombo hicho ni sehemu ya juhudi za China za kuunda kituo cha anga za juu kitakachokuwa kinadhibitiwa na binadamu katika anga za juu kufikia mwaka 2022.
Kiliacha kufanya kazi Machi 2016.
Tunayoyafahamu kuhusu eneo ambalo kilianguka?
Maafisa wanasema tu kwamba kilianguka "juu ya Pacific Kusini".
Wataalamu wa anga za juu wa Marekani wamesema wametumia teknolojia ya kufuatilia mzingo wa dunia kuthibitisha kuingia ardhini kwa Tiangong-1.
Mtaalamu wa anga za juu Jonathan McDowell kutoka Harvard ameandika kwenye Twitter kwamba huenda chombo hicho kimeanguka kaskazini magharibi mwa Tahiti.
Wataalamu walitatizika kubaini hasa ni wapi chombo hicho kingeanguka.
Idara ya anga za juu ya China ilikuwa awali imekadiria kimakosa kwamba chombo hicho kingeanguka karibu na Sao Paulo, Brazil muda mfupi kabla ya chombo hicho kuingia anga ya dunia.
Shirika la Anga za Juu la Ulaya lilisema mapema kwamba uwezekano mkubwa ni kwamba chombo hicho cha Tiangong-1 kingeanguka baharini.
ESA walisisitiza kwamba uwezekano wa mtu kugongwa na vifusi vhya vyombo hicho ulikuwa "chini ya mara milioni kumi ya uwezekano wa mtu kupigwa na radi."
Haijabainika ni kiasi gani cha vifusi hivyo kimeanguka ardhini.

Mbona chombo hiki kikaanguka hivi?

Tiangong kilifaa kusitisha shughuli yake ya kuizunguka dunia kwa utaratibu na mpangilio fulani.
Ni chombo kilichokuwa na urefu wa mita 10 (futi 32) na uzani wa zaidi ya tani 8 na ni kikubwa zaidi ya vyombo vyote vilivyoundwa na binadamu ambavyo vimewahi kuanguka kutoka anga za juu.
Lengo lilikuwa kutumia vifaa vinavyokipa chombo hicho msukumo kukielekeza hadi maeneo ya mbali yasiyo na watu maeneo ya Bahari ya Kusini.
RoketiHaki miliki ya pichaAFP
Image captionChina ilikituma chombo cha Tiangong-1 angani mnamo 2011
Lakini kabla ya hilo kufanyika, ghafla mfumo wa kukidhibiti ulikumbwa na hitilafu na wataalamu wa China wakapoteza udhibiti.
Mashirika 13 ya anga za juu ya mataifa mbalimbali, yakiongozwa na Shirika la Anga za Juu la Ulaya (ESA), yalifuatilia njia ya Tiangong na kujaribu kuiga tabia yake kadiri kilivyokaribia kuingia ndani ya anga ya dunia huku kikiendelea kuizunguka.
Presentational grey line
Tiangong maana yake ni 'Kasri la Mbinguni'
Tiangong-1 space lectureHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionMwanananga Wang Yaping alitoa mhadhara unaokumbukwa sana kwa watoto akiwa moja kwa moja kutoka chombo cha Tiangong-1 kikiwa anga za juu
  • Chombo hiki kirirushwa mwaka 2011 kufanyia majaribio utaratibu wa kutuma vyombo vingine na kuviunganisha vikiwa anga za juu
  • Makundi mawili ya wanaanga yalizuru chombo hicho wakitumia vyombo vidogo kwa jina Shenzhou - mwaka 2012 na 2013
  • Walijumuisha wanaanga wa kwanza wa kike kutoka China Liu Yang na Wang Yaping
  • China inapanga kutuma chombo cha anga za juu cha kudumu katika mwongo mmoja ujao
  • Imeunga roketi inayobeba kuinua vitu vya uzani wa juu sana kwa jina Long March 5 kwa ajili ya kazi hiyo
Presentational grey line
Graphic
Ndicho chombo kikubwa zaidi kuwahi kuanguka kutoka angani?
Tiangong ni miongoni mwa vyombo vingine vikubwa vilivyowahi kuanguka bila kudhibitiwa, lakini bado kineachwa nyuma na vyombo vingine.
Chombo cha Skylab cha Marekani kilikuwa na uzani wa tani 80 kilipoanguka, ingawa kiliweza kudhibitiwa kwa kiasi fulani, mwaka 1979.
Kilianguka Australia Magharibi ardhini lakini hakuna aliyejeruhiwa.
Chombo cha Nasa cha Columbia nacho kilikuwa na uzani wa tani 100 kilipoanguka mwaka 2003.
Tena, ardhini hakuna aliyegongwa na vifusi vyake ambavyo vilitapakaa majimbo ya Texas na Louisiana.
Mtaalamu Jonathan McDowell kutoka Kituo cha Fizikia ya Anga za Juu cha Harvard-Smithsonian anasema kwa kukadiria, 50 ni chombo cha 50 kwa ukubwa.
Watu wakishikilia magazeti yenye picha ya mChina wa kwanza kwenda katika anga za mbali kwenye ukurasa wa mbeleHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionMchina wa kwanza aliyefanya safari ya anga za mbali 2003 alikuwa shujaa wa taifa

Je Tiangong-ni nini?

Uchina ilichelewa kuanza uvumbuzi wake wa anga za juu.
Mnamo 2001, Uchina ilizindua vyombo vyake vya anga kwa kujaribu kuwatuma wanyama mwaka 2003 kwenye chombo cha anga za mbali kwenye mzingo wa dunia, na hivyo kuifanya nchi hiyo kuwa ni ya tatu kufanya hivyobaada ya Muungano wa Usovieti na Marekani.
Mpango wa vituo vya safari za anga za mbali ulianza kwa kukituma chombo cha Tiangong-1 ama "Kasri la Mbinguni", mwaka 2011.
Kituo hicho kidogo kiliweza kuwahifadhi wataalam wa masuala ya anga za mbali lakini kwa muda mfupi wa siku kadhaa. Mchina wa kwanza mwanamke mtaalamu wa anga za juu Liu Yang alitembelea kituo hicho mwaka 2012.
Kilikamilisha huduma zake mwezi Machi 2016, miaka miwili zaidi ya muda kiliopangiwa.

Rais Magufuli akejeli waraka wa maaskofu Tanzania

Magufuli na PadreHaki miliki ya pichaIKULU, TANZANIA
Image captionRais Magufuli alishiriki misa ya sikukuu ya Pasaka katika Kanisa la Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam Jumapili ambayo iliongozwa na Paroko Msaidizi Venance Tegete.
Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli ameupuuzilia mbali waraka wa maaskofu uliotolewa wakati wa kuanza kwa msimu wa Pasaka akisema hauna msingi wowote ule.
Aliendelea kwa kusema pia kwamba mbona hakuna aliyetoa waraka wakati mauwaji ya Kibiti yakiendelea.
Rais Magufuli amesema hayo katika hafla ya kuweka jiwe la msingi wa ujenzi wa rada za kiraia uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Majibu yake kwa waraka wa maaskofu aliyatoa wakati akiwapongeza wasaidizi wake, mawaziri, viongozi wa ulinzi na usalama pamoja na wasaidizi wengine, ambao amewasifu kwa kuendelea kutimiza majukumu yao.
"Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama ndio maana tuko salama leo, ilifikia mahali hata kwenda Kibiti tu ni kazi. Hatukuona mtu yeyote analaani," amesema Dkt Magufuli.
"Kufa kwa Kibiti ni salama, hakuna hata waraka uliotoka. Ingawaje sipendi sana kulizungumzia hili kwa kwa sababu najua halina msingi, wala halitafanikiwa na wala hakuna lolote. Kwa sababu serikali ipo, nimekabidhiwa na wananchi, kuilinda kwa nguvu zote".
Amesisitiza serikali ipo na amekabidhiwa na wananchi na kuapa kwamba atailinda kwa nguvu zote.
Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kujibu moja kwa moja waraka uliotolewa na maaskofu wa kanisa la Kilutheri nchini Tanzania wiki chache, ambao pamoja na mambo mengine ulionya juu ya mwenendo wa demokrasia nchini Tanzania.

Maaskofu walisema nini?

Katika waraka wa ujumbe wa Pasaka uliosomwa katika makanisa ya Kilutheri kote nchini Tanzania na kusambaa katika mitandao ya kijamii, baraza hilo liliorodhesha mambo kadhaa ambayo wameyataja kuwa ndio tishio la umoja na amani ya nchi hiyo.
Utekwaji wa watu wa hivi karibuni, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, mauaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi ni baadhi tu ya mambo yaliyotajwa katika waraka huo.
Serikali ya Tanzania mwanzoni ilijibu tu kwa kusema kuwa kwa wakati huo haikuona cha kujibu na kwamba iliwatakia tu waumini kheri ya Pasaka.

Mwanasiasa wa upinzani Kenya Miguna Miguna asafirishwa kutoka Dubai kwenda Canada

Bw MigunaHaki miliki ya pichaAFP/GETTY
Mwanasiasa wa upinzani aliyezuiwa kuingia Kenya wiki iliyopita na kusafirishwa kwa lazima hadi Dubai amewasili nchini Canada.
Bw Miguna Miguna, ambaye ni wakili, alisafiri kwa ndege iliyokuwa ikielekea Toronto, Canada, baada ya kukaa katika uwanja wa kimataifa wa Dubai kwa siku nne.
Mmoja wa mawakili wa mwanasiasa huyo Nelson Havi ameandika kwenye Twitter kwamba Bw Miguna amesafiri kwenda Canada kwa hiari kupitia usaidizi wa ubalozi wa Canada katika Umoja wa Milki za Kiarabu (UAE).
Bw Havi amesema Miguna atafanyiwa uchunguzi wa kimatibabu na "atarejea baadaye".
Gazeti la Nation, limesema afisa mmoja wa serikali amewafahamisha kwamba Bw Miguna aliondoka Dubai akitumia ndege ya Air Canada 57 (ACA57) baada ya kuwasilisha pasipoti yake ya Canada.
Bw Miguna alikuwa amesema hakuwa na pasipoti hiyo alipowasili uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta, Nairobi Jumatatu wiki iliyopita.
Bw Miguna ndiye aliyeidhinisha kiapo cha Bw Raila Odinga alipokuwa anajiapisha kuwa 'Rais wa Wananchi' mwezi Januari.
Bw Miguna Miguna alijaribu kurejea Kenya Jumatatu lakini akazuiwa kuingia baada yake kudaiwa kutowasilisha pasipoti ya Canada ambayo ilitumiwa kumsafirisha kwa nguvu hadi Canada.
Wakili huyo alisisitiza kwamba ni raia wa Kenya na hafai kuzuiwa kurejea.
Taarifa zinasema Bw Miguna, ambaye pasipoti yake ya Kenya ilitwaliwa na polisi kabla ya kuondolewa kwake Kenya mwezi jana, alikuwa ametakiwa kuwasilisha ombi la kupata visa ya kukaa Kenya kwa miezi sita kwa kutumia pasipoti hiyo yake ya Canada.
Alikataa jaribio hilo na badala yake kutoa kitambulisho chake cha taifa kuonesha kwamba yeye ni Mkenya na kutaka aruhusiwe kuingia.
Bw Miguna, aliyekuwa amewasili uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta mwendo wa saa nane adhuhuri, alikesha kwenye uwanja huo.
Maafisa walijaribu kumsafirisha kutoka uwanja huo mara ya kwanza kwa kutumia ndege ya shirika la Emirates ambayo ilikuwa inaelekea Canada kupitia Dubai usiku huo wa Jumatatu lakini hawakufanikiwa.
Bw Odinga alijaribu kumsaidia Bw Miguna kuondoka uwanja wa ndege bila mafanikioHaki miliki ya pichaAFP/GETTY
Image captionBw Odinga alijaribu kumsaidia Bw Miguna kuondoka uwanja wa ndege bila mafanikio Jumatatu
Hata hivyo, walifanikiwa usiku wa kuamkia Jumatano.
Bw Miguna asubuhi aliandika kwenye Facebook kwamba aliamka na kujipata yuko Dubai na kwamba anahitaji matibabu.
Mwanasiasa huyo alisema alisindikizwa na afisa wa idara ya ujasusi na kwamba amemuona daktari uwanja wa ndege.
Bw Miguna alisisitiza kwamba hatasafiri kwenda popote ila kurejea Nairobi.
Serikali imechukua hatua hiyo licha ya kuwepo kwa maagizo ya mahakama ya kuzuia kutimuliwa kwake na ya kuitaka serikali kufanikisha kurejea kwake nchini humo.
Jaji wa Mahakama Kuu George Odunga aliwapata na hatia waziri wa usalama nchini humo, mkuu wa polisi na mkuu wa idara ya uhamiaji ya kukaidi maagizo ya mahakama iwapo wangekataa kumwachilia huru.
Aliwatoza faini ya Sh200,000 (Dola 2,000) kila mmoja.

Kukamatwa kwa Miguna mara ya kwanza

Bw Miguna alikamatwa na polisi kwa mchango wake katika kuapishwa kwa Bw Odinga kuwa "rais wa wananchi", hafla iliyofanyika uwanja wa Uhuru Park, Nairobi mnamo 30 Januari.
Bw Miguna, ambaye pia ni wakili, ndiye aliyetia saini hati ya kiapo ya Bw Odinga.
Serikali ilikuwa imeeleza hatua hiyo ya kiongozi huyo wa upinzani kuwa uhaini wa hali ya juu.
Bw Odinga anadai kwamba alimshinda Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu wa 8 Agosti ambao matokeo yake yalifutiliwa mbali na Mahakama ya Juu kwa sababu ya kutokea kwa kasoro nyingi.
Mahakama iliamuru uchaguzi mpya ufanyike lakini Bw Odinga akasusia uchaguzi huo mnamo 26 Oktoba.
Bw Miguna amesambaza picha anazosema ni zake akiwa hospitalini kumuona daktari uwanja wa ndege DubaiHaki miliki ya pichaHISANI
Image captionBw Miguna alisambaza picha anazosema ni zake akiwa hospitalini kumuona daktari uwanja wa ndege Dubai punde baada ya kufikishwa Dubai
Chini ya Kifungu 17 cha Katiba ya Kenya, mtu aliyezaliwa nchini Kenya anaweza tu kuupoteza uraia wake iwapo itabainika kwamba aliupata uraia huo kwa njia ya ulaghai, au ibainike kwamba mtu huyo au wazazi wake walikuwa raia wa nchi nyingine, au ibainike kwamba mtu huyo alikuwa na umri wa zaidi ya miaka minane alipogunduliwa akiishi Kenya.
Serikali ya Kenya imekuwa ikisisitiza kwamba chini ya katiba ya zamani, Wakenya hawangekuwa na uraia wa nchi mbili.
Serikali inasema hatua ya Bw Miguna ya kupata pasipoti ya Canada mwaka 1988 ina maana kwamba aliupoteza uraia wa Kenya wakati huo.
Ingawa Bw Miguna aliwasilisha maombi na akapewa pasipoti ya Kenya mwaka 2009, serikali inasema pasipoti hiyo ya Kenya si halali kwa sababu hakufichua kwamba wakati huo alikuwa raia wa Canada pia.
Serikali imesema mwanasiasa huyo hakuwasilisha tena ombi la kuruhusiwa kuwa raia wa Kenya katiba ilipofanyiwa marekebisho mwaka 2010 na Wakenya wakakubaliwa kuwa na uraia wa nchi mbili.
Bw Miguna amekuwa akisisitiza kwamba hakuwahi kuukana uraia wake wa Kenya na kamwe hawezi kufanya hivyo.
"Katiba iko wazi kabisa: hakuna mtu yeytoe anayeweza au anayeweza kudai kuufuta uraia wa Mkenya aliyezaliwa nchini Kenya," alisema awali.
Presentational grey line

Matukio makuu mzozo kuhusu Miguna

30 Januari: Miguna aidhinisha hati ya kiapo cha Raila Odinga kuwa 'Rais wa Wananchi'
2 Februari: Atangaza kwamba amekamatwa na polisi Nairobi
6 Februari: Afurushwa kutoka Kenya na kupelekwa Canada
16 Machi: Odinga waambia wafuasi wake kwamba baada ya mapato yake na Bw Kenyatta, Miguna anafaa kuruhusiwa kurejea Kenya bila masharti
26 Machi: Arejea Kenya lakini azuiliwa uwanja wa ndege wa JKIA. Baadaye usiku, anusurika jaribio la kumpeleka Dubai.
28 Machi: Miguna apelekwa Dubai kwa nguvu. Asema anafahamu mipango ya kumpeleka hadi London.
Presentational grey line

Miguna Miguna ni nani?

Miguna alizaliwa katika kijiji cha Magina, katika jimbo la Kisumu, magharibi mwa Kenya.
Bw Miguna amekuwa kiongozi wa kundi linaloitwa National Resistance Movement (NRM, Vuguvugu la Taifa la Kupinga Serikali), ambalo liliundwa na muungano wa upinzani wa National Super Alliance siku moja kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio ambao Bw Odinga alisusia mnamo 26 Oktoba mwaka jana.
"Utakuwa ni muungano wa ukombozi," alisema Bw Odinga akitangaza kuundwa kwa vuguvugu hilo.
"Tumesema hatutaheshimu serikali dhalimu."
Bw Miguna baadaye alijitangaza kuwa Jenerali wa NRM.
Mnamo 30 Januari, siku ya kuapishwa kwa Bw Odinga kuwa 'Rais wa Wananchi', muungano huo uliorodheshwa kuwa kundi haramu na waziri wa usalama Dkt Fred Matiang'i.
Hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa Bw Miguna kujipata akikabiliana na serikali na nguvu zake.
Mwaka 1988, alikamatwa na serikali ya wakati huo ya Rais Daniel arap Moi.
Bw Miguna baadaye alitorokea Kenya ambapo alipata hifadhi kama mkimbizi wa kisiasa.
Alirejea nchini Kenya na akashiriki katika kampeni za uchaguzi za Bw Odinga na chama chake cha Orange Democratic Movement (ODM) mwaka 2007.
Uchaguzi wa mwaka huo ulikumbwa na utata na baada ya serikali ya muungano kati ya Bw Odinga na Rais Mwai Kibaki kuundwa, ambapo Bw Odinga aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu, Bw Miguna alihudumu kama mmoja wa washauri wake kati ya 2009 na 2011
Wawili hao walizozana na Bw Miguna akawa mmoja wa wakosoaji wakuu wa Bw Odinga.
Aliandika kitabu kwa jina Peeling Back the Mask ambapo alimkosoa sana Bw Odinga na uongozi wake.
Mwaka 2013, alimuunga mkono Bw Kenyatta katika uchaguzi wa urais mwaka huo.
Lakini alibadilisha tena msimamo wake na kurejea upande wa Bw Odinga mwaka 2017, mwaka ambao aliwania pia wadhifa wa Gavana wa Nairobi katika uchaguzi uliofanyika Agosti ingawa kama mgombea ambaye hakuwa na chama.
Januari 30 mwaka huu, ndiye aliyetia saini hati ya kiapo cha Bw Odinga kuwa 'Rais wa Wananchi'.
Bw Odinga alipokutana na Bw Kenyatta mnamo 9 Machi na wakaahidi kuunganisha Kenya, Bw Miguna ni miongoni mwa waliomkosoa kiongozi huyo wa upinzani kwa hatua hiyo akisema huo ulikuwa sawa na usaliti.